Like Us On Facebook

AMUUA MKEWE KWA KUMCHOMA KITU CHENYE NCHA KALI NA KUMTOBOA KOROMEO


            Polisi Jamii na wakazi wa Kawe Ukwamani jijini Dar es Salaam, wakiupakia kwenye gari la polisi, mwili wa mwanamke Yusta Mkali jana. Mwanamke huyo alikutwa amekufa katika chumba walimokuwa wakiishi 

Mkazi wa Kawe jijini Dar es Salaam Musa Senkando , anatafutwa na polisi kwa tuhuma za kumuua mkewe, Yusta Mkali , baada ya kumchoma na kitu chenye ncha kali na kumtoboa koromeo.
Mauaji hayo yalitokea jana asubuhi eneo la Kawe Kanisani jijini 

dar es Salaam ambapo mwandishi wetu alifika eneo la tukio na kuushuhudia umati mkubwa uliokuwa nje ya nyumba ya Senkando na familia yake.
Aidha baada ya mauaji hayo,  mtuhumiwa aliuacha mwili wa mkewe kitandani na kukimbilia kusikojulikana.

Akithibitisha tukio hilo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camillius Wambura,  alisema uchunguzi wa awali umebaini kuwa mauaji hayo yalitokea usiku wa kuamkia jana.
Wambura alisema muuaji anasadikiwa kutumia kitu chenye ncha kali na kumshambulia mkewe kwenye koromeo.

Mtoto wa marehemu Yusta, Joshua Zebedayo anayekadiriwa kuwa na zaidi ya miaka 15 alisema hakufahamu juu ya mauaji hayo na kwamba  alishtushwa  alipouona  mwili wa mama yake ukiwa kitandani, wakati huo alipoingia kusafisha chumba cha wazazi wake saa mbili asubuhi .

Alieleza kuwa ni kawaida yake kuwasaidia usafi kwa kuwa wazazi wake huenda kazini alfajiri.

“Nilikuta mlango umefungwa, nikaufungua ila cha kushangaza nilimkuta mama amelala wakati alipaswa kuwa kazini, nilivyofunua shuka nikamuona amelowa damu . Hali aliyokuwa nayo ilinifanya nihofu kuwa amefariki dunia. Sikuweza kukaa kimya nilianza kupiga kelele,” alisema kijana huyo, kwa huzuni akilia .

Joshua alisema kabla ya kifo hicho hali ya nyumbani kwao ilikuwa shwari kwani wazazi wake walikuwa wanaishi kwa furaha kama kawaida .

“Jana mama alitoka kazini kama kawaida saa  12 jioni tukala na niliwaacha wakiwa wanazungumza na kuwasiliana vizuri na walikuwa wanacheka , ”alisema.

Mwenye nyumba walikopanga familia hiyo,  Watatu Hadija, aliliambia gazeti hili kuwa haelewi kama wenza hao walikorofishana au nini kilitokea kwa kuwa mlango  wa vyumba vyao ulikuwa umefungwa na hawakusikia kelele zozote.

“Asubuhi hii sisi tulisikia kijana Joshua akipiga makelele ndipo tulipotambua kuwa Yusta amefariki,” alisema.

Hadija alisema marehemu kabla ya kifo chake alirudi kutoka kazini na kutaniana naye kama ilivyokuwa  kawaida yao.

“Yusta alikuwa ni mpole na amekaa hapa kwa miaka mitano. Nilikuwa naishi naye vizuri  kama mwanangu,”aliongeza Hadija.

Hassan Kihelelo, mmoja wa majirani wa mtuhumiwa alidai Musa alikuwa na mazoea ya kumfanyia visa mkewe na kudai mwaka jana alimpiga Yusta na kumchana mkono.

Alidai ulichanika  baada ya kupigwa na stuli lakini alinyanyua mkono huo  kuizuia isimuumize kichwani.

Wakati wa uhai wake, marehemu Yusta alikuwa mfanyakazi  wa kampuni ya mawasiliano ya umma ya Frontline Porter Novelli.


SOURCE: NIPASHE
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari