Akizungumza kwa machungu, mama wa kijana huyo, Rehema Omar alisema tukio hilo lilitokea hivi karibuni ambapo siku nne kabla ya kukutwa akiwa amejinyonga, Kulwa aligombana na baadhi ya marafiki zake ambao walichukua tofali na kumpiga nalo mdomoni na kusababisha meno mawili kung’oka.
“Tulimpa fedha kwa ajili ya kwenda kujitibia kisha alirejea nyumbani na kuendelea kujiuguza majeraha kwani yalikuwa ni makubwa,” alisema Rehema.
Mama huyo aliendelea kusema wakati mwanaye akiendelea kuuguza kidonda ndipo alipopatwa na maswahibu hayo baada ya kwenda disko na wenzake.
“Siku hiyo niliingia kulala na ilipofika saa tisa usiku niligongewa mlango na watu wawili na kuambiwa hali ya mtoto wangu ni mbaya pasipo kubainisha amefanya nini,” alisema mama huyo.
Chanzo kingine kilipenyeza madai kuwa, siku ya tukio Kulwa alikutwa amejinyonga mwenyewe baada ya kutoka disko lakini mama yake mzazi hakukubaliana na madai hayo.
“Nimeumia sana kwani mwanangu hawezi kujinyonga kwa sababu hakuwa na tatizo lolote ukizingatia nguo aliyokuwa ameivaa tuliikuta imechanwachanwa, mwanangu amekufa kifo kibaya sana,” alisema mama huyo huku akidondosha machozi.
Marehemu Kulwa alizaliwa na pacha wake, Doto ambaye walikuwa wakitembea naye mara kwa mara isipokuwa siku hiyo ambayo mwenzake alikutwa na umauti.