Like Us On Facebook

MIHADHARA YA SHEIKH PONDA YAPIGWA MARUFUKU KATIKA ARDHI YA ZANZIBAR


Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imempiga marufuku Katibu wa Jumuiya ya taasisi ya Kiislamu shekhe Issa Ponda Issa kuendesha mihadhara ya kidini katika ardhi ya Zanzibar yenye muelekeo wa kuleta mifarakano, chuki na uhasama.


Makamo wa pili wa rais balozi Seif Ali Iddi alisema hayo wakati akiahirisha kikao cha Baraza la Wawakilishi cha bajeti kwa mwaka wa fedha 2013-2014.

Balozi Seif alisema mahubiri ya sura ya uchochezi kamwe hayawezi kuvumiliwa yakiwa na lengo la kuiingiza nchi katika machafuko ya kidini ambayo madhara yake ni makubwa.

Aidha balozi Seif alisema Serikali kamwe isilaumiwe kwa hatua itakazochukuwa kwa viongozi wa aina hiyo na kuwataka wananchi wasiunge mkono juhudi hizo.

'Mheshimiwa Spika wa Baraza la Wawakilishi Serikali inapiga marufuku mahubiri ya kiongozi huyo ambayo yanaonekana kuwa na muelekeo wa kuleta chuki na uhasama... Serikali isilaumiwe kwa hatua itakazochukuwa kwa viongozi wote wa aina hiyo''alisema.

Balozi Seif alisema Zanzibar haina migongano ya kidini pamoja na waumini wake ambao wamekuwa


wakishirikiana kwa pamoja na waumini wengine wenye dini tofauti.

Lakini alisema zipo dalili zinazofanywa na baadhi ya viongozi wa dini za kutaka kuwagawa wananchi wa Unguja na Pemba kwa kutumia visingizio na misingi ya kuendeleza dini ya Kiislamu.

Kwa mfano alisema Shekhe Ponda amekuwa akiwatumiya wananchi wa Zanzibar kwa ajili ya kuendesha mihadhara yake yenye muelekeo wa kuleta vurugu na chuki, lakini wananchi wanatakiwa kufahamu kwamba vurugu zinapoibuka waathirika ni Wazanzibari wakati yeye anakimbilia Tanzania Bara.

'Huyu shekhe yeye anakaanga mbuyu kuwaachiya wenye meno watafune... yakizuka machafuko yeye hayupo nchini kazi ipo kwa wananchi wa Zanzibar ambao ndio waathirika wakubwa,' alisema.

Balozi Seif alifafanua na kusema Wazanzibari wamechoka na mifarakano iliyotokana na mivutano ya kisiasa ambayo ilizuka tangu ulipoingia mfumo wa vyama vingi katika mwaka 1992. Alisema juhudi za kuleta amani na utulivu zimechukuwa muda mrefu huku zikiacha makovu kwa wananchi wa Zanzibar na hivyo kamwe wananchi wasikubali kurejea kwa matukio hayo.

Hivi karibuni Shekhe Ponda alikuwepo Zanzibar na kuendesha mihadhara katika misikiti mbali mbali ikiwemo vijijini ambayo inadaiwa kuwa na sura ya uchochezi.

Aidha balozi Seif alikemea vikundi vya watu vinavyopita sehemu mbali mbali Unguja na Pemba wakifanya sensa kujuwa idadi ya wafuasi wa CCM na CUF. Balozi alisema hakuna sensa ya aina hiyo na kutoa agizo kwa masheha kutoa taarifa katika vyombo vya ulinzi mara watakapowakuta watu wa aina hiyo.

'Serikali haina zoezi la sensa la kujuwa idadi ya wafuasi na wanachama wa CCM na CUF katika shehia zake... hilo zoezi ni batili na halitambuliwi na taasisi za Serikali' alisema.

Kikao cha Baraza la Wawakilishi ambacho kimechukuwa takriba miezi miwili kikijadili makadirio mapato na matumizi ya bajeti za Wizara mbali mbali kwa mwaka wa fedha 2013-2014 kimeahirishwa hadi Oktoba 9 mwaka huu.

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari