Like Us On Facebook

MADUDU YA NECTA:MASWALI HADI YA CHUO KIKUU YATOLEWA KWENYE MTIHANI DARASA LA SABA



           DOGO WA PILI KUTOKA MBELE AKIFIKIRIA SWALI BILA KUONA JIBU
MBUNGE wa kuteuliwa, James Mbatia (NCCR-Mageuzi), ameibua madudu mapya katika sekta ya elimu, ambao umebaini kwamba kwenye mitihani ya majaribio ya darasa la saba, baadhi ya maswali ya kuchagua, hayakuwa na majibu.


Mitihani hiyo ya majaribio ya programu maalum ya matokeo makubwa sasa, kwa mujibu wa Mbatia ilifanywa na wanafunzi wa darasa la saba hivi karibuni katika masomo ya Hisabati, Kiswahili na Kiingereza katika wilaya 40 nchini.

Katika uozo huo ambao ameutaja kama kuwakatisha tamaa wanafunzi katika somo la Hisabati, Mbatia alisema maswali sita yalibainishwa na wataalamu wa Hesabu kuwa hayana majibu huku swali moja likiwashinda maprofesa waliofanya mtihani huo.

Alisema katika swali moja, namba 33 walimu wa hisabati katika shule kubwa za msingi walishindwa kulifanya na baadaye kubainika kuwa ni swali la mwanafunzi anayechukua fani ya uhandisi katika vyuo vya elimu ya juu.

Mbatia alisema katika mitihani hiyo, kunamakosa mbalimbali ya lugha pamoja na usahihi wa masuala mbalimbali, ikiwemo programu hiyo kuainishwa kama matokeo makubwa sasa huku jina la wizara likiandikwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi.

Alisema katika mtihani huo wa hisabati,ambao wanafunzi wa darasa la saba walitakiwa kufanya kwa saa mbili, mtaalamu wa aligebra aliufanya kwa saa 2:10 na profesa saa 2:03 huku yeye akifanya kwa saa 2:19.

“Matokeo haya ni kuwakatisha tamaa na kuwaua wanafunzi kabla ya kufanya mitihani, ni lazima hatua madhubuti zichukuliwe kuokoa mapigo haya ya moyo wa Taifa ambayo yakizimika, Taifa linakufa,” alisema.

Mbatia alitoa mapendekezo yake ili kuokoa janga hili la elimu ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa Tume ya Kudumu ya Elimu, itakayoshughulikia kuhakikisha ubora wa elimu nchini. Tume hiyo kwa mujibu wa Mbatia, inatakiwa kuwa na mamlaka ya kuhakiki utendaji wa taasisi mbalimbali za elimu, ambazo hadi sasa zimeonekana kutotimiza vyema wajibu wake.

“Ninaamini kwamba,tume hiyo itakapoundwa itasaidia kubainisha wazi nini falsafa na malengo hasa ya utoaji wa elimu nchini, kulingana na wakati tulionao, jambo ambalo halitakuwa geni kwani katika uongozi wa awamu ya kwanza, kulitungwa falsafa na miongozo mbalimbali,”alisema

Alisema kwa mamlaka aliyonayo Rais na na kwa mujibu wa katiba na kwa kadri anavyoona inafaa, anaweza kuunda tume na kuipatia majukumu ya utendaji stahiki, ikiwemo kutoa idhini ya matumizi ya mitaala mingine.

Pia alipendekeza tume hiyo ihariri na kupitia vitabu vya kiada kwa shule nchini na kufanya utafiti za kisayansi kuhusu masuala mbalimbali ya elimu kwa lengo la kuinua ubora wa elimu.

Akizungumza na gazeti hili, Msemaji wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Bunyanzu Ntambi alikiri kuwa jinala wizara limekosewa katika mitihani hiyo. Alipoulizwa kuhusu uozo uliopo katika mitihani hiyo ya majaribio, alisema atafuatilia na atatoa taarifa kwa umma baadae

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari