ASKARI
Polisi saba wa kiume na mmoja wa kike, wanakabiliwa na tuhuma za
kumtesa mahabusu mwanamke kwa kumvua nguo na kumwingizia chupa ya bia
katika sehemu za siri.
Akizungumza
mbele ya Hakimu Mkazi wa mjini Sumbawanga, Rosalia Mugissa, mshitakiwa
katika kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha, Clara God (32), alidai
kufanyiwa unyama huo na askari wa kiume mbele ya askari mwanamke.
Clara,
ambaye ni mfanyabiashara na mkazi wa kitongoji cha Chanji na washtakiwa
wengine watatu wa kiume akiwemo mganga wa kienyeji, wanakabiliwa na
kesi ya unyang’anyi wa kutumia silaha na wako rumande kwa kuwa kesi hiyo
haina dhamana.
Kabla
ya kutoa madai hayo, kesi hiyo ililetwa jana kwa ajili ya kutajwa na
Mwendesha Mashitaka, Wakili wa Serikali, Simoni Peresi aliomba shauri
hilo liahirishwe kwa kuwa upelelezi wake bado haujakamilika.
Hata
hivyo, Hakimu Mugissa aliwauliza washtakiwa iwapo wana hoja yoyote ile
ya kueleza mahakamani hapo, ndipo Clara alipoieleza mahakama hiyo kuwa
ana hoja.
Kukamatwa
Huku
akibubujikwa na machozi alidai kuwa usiku wa Desemba 11 mwaka jana,
askari Polisi walifika nyumbani kwake katika kitongoji cha Chanji na
kumtaka aeleze alipomficha mumewe ambaye alikuwa akituhumiwa na kesi ya
unyang’anyi wa kutumia silaha.
“Mie
niliwajibu kuwa mume wangu yupo mjini Namanyere (wilayani Nkasi) kwa
mke mwenzangu, ndipo wakanichukua kwa nguvu na kunibambikia kesi hii ya
unyang’anyi wa kutumia silaha,” alidai.
Alipofika
mahabusu kabla ya kuanza kuhojiwa, Clara alidai alipekuliwa na askari
saba wa kiume ambao walimlazimisha kuvua nguo zote pamoja na za ndani.
Alidai
askari hao walianza kumwingizia vidole katika sehemu zake za siri kwa
zamu huku wakimlazimisha ataje mahali alipojificha mumewe, na yeye
akubali kuwa alishiriki katika uhalifu huo wa unyang’anyi wa kutumia
silaha.
Huku
baadhi ya watu waliohudhuria mahakamani kusikiliza shauri hilo
wakidondokwa na machozi, Clara alidai askari wote saba wanaume na askari
mmoja mwanamke anawakumbuka.
“Mheshimwa
Hakimu askari wote saba wa kiume pamoja na askari mmoja wa kike wote
waliokuwa wakinifanyia ukatili huo nawafahamu kwa sura … hata
wakijipanga mstari na kuchanganyika na wengine nawafahamu,” alidai.
Aliendelea
kueleza kuwa akiwa amewekwa katika chumba maalumu akiwa uchi wa mnyama,
askari hao wa kiume walimwamuru akalie chupa ya soda huku ikiingia pole
pole sehemu zake za siri na askari huyo wa kike akishuhudia, alikuwa
akipigwa kwa nguvu mabegani.
“Nilipata
uchungu mkali wakati mdomo wa chupa hiyo ukiingia, lakini ilishindikana
chupa nzima kuingia ndipo wakaamuru nipumzike baadae wakanilazimisha
niingize chupa ya bia zile za zamani zenye shingo ndefu huku nikiwa
nimeikalia, damu zilitoka nikaumia vibaya na kusikia maumivu makali
sana,” alidai.
Aliongeza
kuwa askari hao kila waliposikia sauti za watu nje, walimwamuru avae
nguo zake na baadae walimwamuru avue nguo zake zote baada ya kuhakikisha
hakuna mtu anayeweza kuingia humo, na kuendelea kumdhalilisha huku
wakimtukana matusi ya nguoni.
Mumewe alipo
Clara
aliendelea kudai mahakamani hapo kuwa mumewe hatimaye alikamatwa mjini
Namanyere wilayani Nkasi na kusafirishwa hadi mjini Sumbawanga na
kuwekwa mahabusu ambapo alikufa akiwa mikononi mwa askari Polisi.
Alidai
kuwa mumewe pia alilazimishwa kuingiza chupa sehemu zake za siri ambazo
zilichanika na kumsababishia kifo kutokana na kupoteza damu nyingi na
haijulikani hadi sasa wapi alipozikwa.
Baada
ya Clara kutoa hoja yake hiyo mbele ya Mahakama, Hakimu Mugissa
aliahirisha shauri hilo ambalo litatajwa tena Februari 18, mwaka huu na
kuamuru washitakiwa wote kurejeshwa rumande kwa kuwa shauri hilo
kisheria halina dhamana.
Mshitakiwa
Clara na wenzake watatu, Daniel Mangi (28), mkulima na mganga wa
kienyeji mkazi wa Kaswepepe, Hassan Ahmid (24), mkazi wa Jangwani na
Magembe Masanja ‘Msukuma’ (39) mkazi wa kijiji cha Majimoto wilayani
Mlele katika mkoa wa Katavi, wanadaiwa kutenda kosa hilo Desemba 11 ,
mwaka jana.
Inadaiwa
kuwa siku ya tukio washitakiwa hao kwa pamoja walimvamia na kumtishia
kwa kisu John Mazimba mkazi wa Jangwani na kumpora simu ya mkononi yenye
thamani ya Sh 60,000.
SOURCE:HABARI LEO