Habari
zinasema Maregesi alikutwa na mkasa huo wilayani Bunda juzi saa 12:30
jioni, wakati akipiga picha tukio la vijana wa chama hicho kumteka na
kumpiga kijana anayedaiwa kuwa kada wa Chadema.
Akisimulia mkasa huo akiwa katika wodi ya wanaume Hospitali ya Bunda, Maregesi anadai kuwa alikabwa na viongozi wa chama hicho wakati akipiga picha za tukio la kada huyo wa Chadema aliyeshushwa kutoka ndani ya gari na kuanza kushambuliwa na vijana waliokuwa pamoja na viongozi hao.
Anafafanua wakati akiendelea kupiga picha tukio hilo, ghafla Mwenyekiti wa chama hicho wa mkoa alimkaba kwa madai kuwa atawaumbua na kusaidiana na kiongozi mwenzake ambaye alichukua kamera na ghafla kundi la vijana wa chama hicho wakamvamia,kuanza kumpiga na kumpora mkoba aliokuwa nao, kisha wakamfungia ndani ya chumba
cha ofisi yao.
"Ndani ya chumba nikaingizwa mimi na huyo kijana anayedaiwa kada wa Chadema na kuanza kutupiga, ndipo mtu mmoja akasema mtawaua hawa iteni polisi baadaye askari wa JKT walioletwa maalumu wilayani Bunda kulinda Kata ya Nyansura ndiyo waliotufikisha Kituo cha Polisi Bunda," alibainisha Maregesi.
Anataja vitu alivyoporwa kuwa ni kamera aina ya Sony digital, risti zake, daftari la kuandikia habari (Note Book), Katiba ya Jamhuri ya Muungano ya mwaka 1977, simu ya mkononi aina ya Adio pamoja na vitu vingine mbalimbali.
Akizungumzia hali ya Maregesi mmoja wa madaktari wa Hospitali ya Bunda, Dk Nimrod Mzuma alisema mwandishi huyo anakabiliwa na maumivu makali katika uti wa mgongo, kichwani na mkono wa kulia na kwamba alifikiswa hospitali hapo akiwa na watu wengine wawili waliojeruhiwa katika tukio hilo pia.
Akizungumzia tukio hilo, Emanueli Imanani Katibu wa Chadema wilaya anavitaka vyama vya
siasa kuheshimu taaluma ya uandishi wa habari.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mara Fernandi Mtui,alikanusha kuumizwa kwa Maregesi na kueleza kuwa ameonana na mwandishi huyo kwenye mkutano wa kampeni ya uchaguzi akiwa hana majeraha yoyote.
Mwenyekiti wa chama cha waandishi wa habari Mkoa wa Mara (MRPC) Emanuel Bwimbo,alilaani tukio hilo akisema linavunja haki ya upatikanaji habari na kwamba limefanywa na viongozi waliopaswa kuwa mfano wa kuigwa.
"Tunaomba wamuombe radhi Maregesi na waandishi wote, pia wamrudishie vifaa vyake haraka ili aendelee na majukumu yake. Wasipotekeleza hayo chama kitachukua hatua ikiwa pamoja na kumsaidia kuendesha kesi mahakamani ili kupata haki yake,"alisema Bwimbo.
source: mwananchi.