STAA wa sinema Bongo, Aunt Ezekiel amejikuta akizichapa na mwanamke
aitwaye Sarah Mwakapala ambaye miaka mitano iliyopita waliwahi kugombea
penzi la mwanaume anayejulikana kwa jina la Mwilu Mwilola ‘Silva’.
Tukio
la ugomvi huo lilichukuwa nafasi juzi katika Ukumbi wa Letasi Lounge
uliopo Victoria jijini Dar ambapo kulikuwa na sherehe ya kuzaliwa ya
rafiki yao aliyetambulika kwa jina la Jamila.
Ilielezwa kuwa, wakati sherehe ikiendelea, Sarah alisimama na kwenda
mahali alipokaa Aunt na kuanza kumfanyia fujo huku wageni waalikwa
wakishind
wa kujua chanzo.Chanzo kilichoshuhudia sekeseke hilo kilibainisha
kuwa, Aunt alionekana kujishusha akimwomba Sarah kuacha mambo ya ugomvi,
lakini Sarah hakukubali ndipo mtiti ulipozidi kuwa mkubwa na
kusababisha wavuane mawigi yao yaliyokuwa yamewapendeza.
“Ghafla tulishangaa Sarah anainuka na kwenda kumvamia mwenzake pasipo
kujua nini chanzo. Sijui wenyewe bado wana mabifu yale ya kipindi kile
au vipi!” kilisema chanzo hicho.
Hata hivyo, mdau maarufu wa mastaa wa Kibongo, Nice Chande ambaye
alikuwa karibu na Aunt, aliingilia ugomvi huo na kutuliza hali ya hewa
kwa kumdhibiti Sarah.
“Unajua kuna watu hawajifunzi kwa wenzao kuhusiana na vifo vya siku
hizi, we unakuja kumfanyia fujo mwenzako, mnapigana bila sababu yoyote.
Je, ghafla mwenzio siku zake za kuishi kumbe zimeisha unapata kesi la
ajabu, unaanza kujilaumu,” alisema Nice.
Baada ya hali ya hewa kutulia, paparazi wetu alimfuata Sarah kutaka
kujua kulikoni amuanzishie fujo mwenzake, hakuweza kujibu chochote huku
akiingia kwenye gari na kukimbilia Kituo cha Polisi Oysterbay kufungua
kesi.
Taarifa zilizopatikana baadaye wakati gazeti hili linakwenda
mitamboni zinadai kuwa, Aunt naye alikimbilia polisi na kukuta Sarah
ameshafungua malalamiko lakini waliyamaliza palepale kituoni na msala
ukaishia hapo