Aidha katika tukio la wilayani Tarime mkoani Mara, mtuhumiwa wa ujambazi wa kutumia silaha , Senso Mwita ameuawa katika kile kilichoelezwa ni kwenye majibizano ya kurushiana risasi na polisi.
Kuhusu anayetuhumiwa kuiba kuku, Polisi imemtaja ni Ngaga Shija ambaye alipewa kipigo na kisha mwili wake kuchomwa moto, alikuwa akituhumiwa kuiba kuku hao katika kijiji cha Ikonda.
Kwa mujibu wa Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Shinyanga, Evaresti Mangala, kabla ya kifo, Shija alikuwa nje kwa dhamana katika kesi iliyokuwa ikisikilizwa Mahakama ya Wilaya ya Shinyanga, akikabiliwa na mashitaka ya unyang’anyi wa kutumia silaha na kupatikana na mali ya wizi.
Aliuawa juzi saa 2 asubuhi katika Kijiji cha Isagala Kata ya Mwamashele wilayani Kishapu. Hata hivyo Kamanda alisema mmiliki wa kuku wanaodaiwa kuibwa, hajafahamika.
Katika tukio la wilayani Tarime, mkoani Mara, mtuhumiwa wa ujambazi wa kutumia silaha , inadaiwa alikuwa na wenzake wawili ambao walijibizana na polisi kwa kurushiana risasi.
Mwita anayekadiriwa na umri wa miaka kati ya 25 na 30, inadaiwa alikuwa akisakwa na Polisi muda mrefu kwa kuhusika na matukio ya unyang’anyi wa kutumia silaha na mauaji katika Tarafa ya Ingwe.
Kamanda wa Polisi Tarime / Rorya, Justus Kamugisha alisema mwezi uliopita kulikuwa na matukio ya mauaji ya watu katika vijiji vya Keisangura , Nyamwaga , Genkuru, Mriba na Nyarero.
Alisema usiku wa kuamkia Januari 5, Polisi ilipata taarifa kutoka kwa raia wema juu ya kuwepo na kuonekana kundi la majambazi katika kitongoji cha Ntarechagini Kijiji cha Nyamwaga.
“Wakati askari wetu wakiwa njiani kuelekea katika kitongoji hicho, ghafla walishambuliwa kwa kurushiwa risasi na majambazi watatu na hapo ndipo askari wetu walianza kujibu mapigo na kufanikiwa kumjeruhi mmoja wao kwa jina la Senso Magabe Mwita,” alisema Kamanda.
Kwa mujibu wa Kamanda, Mwita alikuwa na silaha aina ya SMG iliyofutwa namba zake na risasi 21. Wenzake walitoroka na yeye alifariki kutokana na majeraha ya risasi akiwa njiani kupelekwa hospitali ya wilaya.HABARILEO.