Mamlaka ya vitambulisho vya Taifa (Nida)
Mamlaka
ya vitambulisho vya Taifa (Nida) iko katika hatua ya mwisho ya uhakiki
wa usahihi wa taarifa za waliojiandikisha ili kuwawezesha wananchi
kupata vitambulisho kuanzia Januari mwakani.Zoezi hilo la uhakiki wa mwisho wa taarifa limeanza katika Wilaya ya Temeke jijini Dar es Salaam na ambao watakamilisha zoezi hilo watapatiwa vitambulisho katika muda mwafaka.
Akizungumza na NIPASHE jana, Afisa Uhusiano wa Nida, Thomas William, alisema zoezi la uandikishaji limekuwa na changamoto mbalimbali ikiwamo ya watu kutoelewa majina sahihi ya mitaa na kata zao.
William alisema tatizo la watu kukosa majina katika vituo vyao ni kutokana na wananchi wengi kukosea majina ya kata na mitaa yao, hivyo majina mengi hupelekwa kulingana na jina la mtaa aliojiandikishia katika usajili wa mwanzo.
“Nitoe wito kwa wananchi ambao bado hawajakamilisha taarifa zao ili waweze kupatiwa vitambulisho kwa muda husika na wale ambao bado wafike katika vituo vyetu kwani kwa kila mkoa kuna kituo cha Nida kwa kila wilaya na vituo hivi ni vya kudumu kwa nchi nzima,” alisema William.
Zoezi la kujiandikisha halina mwisho ila kwa sasa kinachositishwa ni uandikishwaji wa watu wengi badala yake wataotaka kujiandikisha baada ya Disemba mwaka huu watalazimika kufika katika vituo vilivyowekwa.
Usajili kwa Dar es Salaam unatarajia kukamilika kati ya Disemba, 2013 na Januari 2014 huku katika mikoa mingine likianza baada ya Dar kumalizika na utaenda kwa kanda moja au zaidi kulingana na ukubwa au udogo wa kanda husika.
Alisema utaratibu wa vituo na ofisi kwa mikoa mingine umekwishakamilika, hivyo wananchi wa nje ya Dar es Salaam wajiandae na kutoa ushirikiano wakati zoezi hilo litakapoanza katika mikoa yao.
-NIPASHE