Like Us On Facebook

VIJANA 800,000 (LAKI NANE) KUPATA AJIRA KUANZIA MWAKANI..

SERIKALI inatarajia kutoa ajira 800,000 kwa vijana kuanzia mwakani kuliwezesha kundi hilo kuondokana na utegemezi katika jamii na kuchangia uchumi wa nchi. 

Akizungumza Dar es Salaam jana wakati wa kongamano la taifa la ajira, Makamu wa Rais, Dk. Gharib Mohamed Bilal alisema programu hiyo itatekelezwa kwa awamu na awamu ya kwanza ya miaka mitatu itaanza kutekelezwa katika mwaka wa fedha wa 2014/2015.



Licha ya uchumi kukua kwa kiwango cha kuridhisha cha asilimia 6.5 kwa mwaka, bado kasi hiyo haijaweza kuzalisha ajira ya kutosha ikilinganishwa na idadi ya wanaoingia katika soko la ajira, alisema.

Alisema soko la ajira nchini lina uwezo wa kuzalisha ajira 300,000 kwa mwaka katika sekta rasmi ikilinganishwa na wastani wa wahitimu 600,000 hadi 800,000 wanaoingia katika soko la ajira nchini.

“Vijana wasiofanya kazi wanaongeza utegemezi katika jamii na familia na kuathiri uchumi na wengine wanajiunga na makundi ya uchochezi na uvunjifu wa amani.

“Wengine wanaweza kujiingiza kwenye vitendo vya wizi, kutumia madawa ya kulevya na biashara ya ngono hivyo ni muhimu kwa serikali na jamii kwa ujumla kuchukua hatua zitakazowezesha kuongeza fursa za ajira kwa vijana kujiajiri au kuajiriwa,”alisema Dk. Bilal.

Hata hivyo, alisema kati ya mwaka 2010 hadi 2013 ajira 610,285 zimepatikana na kwamba kati ya hizo ajira 185,929 zilizalishwa kupitia miradi ya uwekezaji 1,845 iliyosajiliwa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC).

Alisema tatizo jingine linaloikabili sekta ya ajira nchini ni vijana kutoweza kubaini fursa zilizopo na kuzitumia katika kujiajiri katika sekta mbalimbali nchini na kuondokana na dhana ya kuwa ajira ni kuajiriwa.

Naye Waziri wa Kazi na Ajira, Gaudensia Kabaka alisema umeanzishwa a mtandao utakaosaidia vijana kujifunza ni taaluma ipi inahitajika kwenye soko la ajira. 

-MTANZANIA

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari