MMOJA wa mawaziri wa Serikali ya Awamu ya Tatu na mbunge anayetoka Mkoa wa Tabora, anatuhumiwa kumbaka na kisha kutishia kumuua msichana yatima mwenye umri wa miaka 16 (jina limehifadhiwa) anayesoma Shule ya Sekondari Turiani iliyoko Magomeni jijini Dar es Salaam.
Waziri huyo (jina lake linahifadhiwa kwa sasa), ametoa tishio hilo la
mauaji kwa njia ya ujumbe mfupi kupitia namba iliyosajiliwa kwa jina
lake kwa kile alichodai kukaidi amri ya kutaka wasifichue uchafu wake
kwa waandishi wa habari.
Akizungumza kwa uchungu na gazeti la Tanzania Daima, mwanafunzi huyo alisema kuwa
waziri huyo alimbaka kwenye hoteli moja ya kitalii iliyoko jijini Dar
es Salaam mwaka 2011, na kurudia tena kitendo hicho katika Jengo la
Biashara Complex lililoko Mwananyamala Juni 3, 2012.
Mwanafunzi huyo alisema alifikwa na ukatili huo alipoitwa na kiongozi
huyo kwenda kuchukua fedha za ada na matumizi mengine, ambapo mara ya
kwanza alimpa sh 700,000 na mara ya pili sh 350,000.
Yatima huyo anayeishi na dada yake, alikutanishwa na waziri huyo wa
zamani na baba wa mwanafunzi mwenzake, kutokana na msaada mkubwa
aliompa akiwa mgonjwa, ili aweze kumsaidia fedha za ada kama ishara ya
shukurani.
Mwanafunzi huyo alisema baada ya kutambulishwa, aliitwa katika hoteli
hiyo ambako baada ya kufika mapokezi wafanyakazi walimkataza kuingia
chumbani kutokana na umri wake kuwa mdogo (mwaka 2011 alikuwa na miaka
14), lakini waziri huyo wa zamani aliamrisha aruhusiwe.
Akiwa chumbani, mwanafunzi huyo alilazimishwa kulala naye kisha kumpa
sh 700,000, badala ya shilingi 67,000 alizohitaji kwa ajili ya ada.
Mwanafunzi huyo alisema baada ya muhula mmoja aliitwa tena na
kiongozi huyo katika Jengo la Biashara Complex lililoko Mwananyamala
Juni 3, 2012, ambapo pia alimlazimisha kulala naye kwenye zulia la
ofisi yake, kisha kumpa sh 350,000.
Mwanafunzi huyo alisimulia kwamba wakati anatoka kwa huzuni ofisini
kwa mbunge huyo, mmoja wa wahudumu alimuuliza sababu ya huzuni yake na
akalazimika kumweleza kisa hicho, ndipo mhudumu alitokwa machozi huku
akimwambia kwamba, atakufa kwa sababu “baba huyo ni muathirika wa
ukimwi”.
Aliongeza kuwa baada ya kuambiwa vile alilia na kufanya fujo hapo
mapokezi, hadi alipokamatwa na walinzi, kisha kupelekwa kituo cha
polisi kufunguliwa mashitaka.
Hata hivyo, alisema polisi waliposimuliwa kisa chote, walilazimika
kumwita waziri huyo wa zamani na alipofika alikiri na kuomba mambo
yaishie hapo.
“Alikubali na akaahidi kunilipia ada na pesa za matumizi kiasi cha sh
300,000 kila mwezi, jambo ambalo amekuwa akilitekeleza kupitia simu
yake ya mkononi (namba za simu tunazo),” alisema.
Kwa mujibu wa mwanafunzi huyo, Januari 24, mwaka huu walitishiwa
maisha na kiongozi huyo, lakini mwezi uliofuata, mtu asiyefahamika
alienda nyumbani kwao na kuacha gari (namba tunazo) aina ya Mercedes
Benz yenye rangi ya bluu wakati akiwa shuleni, kisha kuacha ufunguo kwa
jirani yao kwa maelekezo kuwa akifika apewe.
Wamesema baadaye kiongozi huyo aliwapigia simu kuwaarifu kuwa amempa
zawadi ya gari kwa ajili ya matumizi, na wanaruhusiwa kuliuza ili
wapate pesa za mahitaji yake siku zilizosalia, kwani baada ya uchaguzi
mkuu 2015, atakuwa Waziri Mkuu, hivyo itakuwa ngumu yeye kumtumia huyo
binti pesa kama alivyoelekezwa na Jeshi la Polisi kituo cha Oysterbay.
Hata hivyo, wasichana hao walishindwa kulitumia gari hilo hivyo kutoa taarifa polisi ili kesi ipelekwe mahakamani.
Wamedai kuwa polisi walikubali kulipeleka tatizo hilo kwa katibu wa
Bunge, ambaye alimwita mwanafunzi huyo na nduguye Dodoma kukutana na
Kamati ya Haki na Maadili ya Bunge.
Hata hivyo, walipofika Dodoma hawakuweza kupata ufumbuzi kwa maelezo
kuwa waziri huyo wa zamani hakuwepo hadi Bunge lilipoisha. Kwa muda
wote, wasichana hao walisema waligharimiwa kila kitu na Ofisi ya Bunge.
Kabla ya kurudi Dar es Salaam, mabinti hao walisema waliitwa na
kiongozi mmoja wa juu wa CCM aliyewalekeza kwenda kumwona Makamu
Mwenyekiti wa chama hicho, Philip Mangula.
Kwa mujibu wa mawasiliano, kiongozi mwingine (jina tunalo) alimpigia
binti huyo simu majira ya asubuhi, akimtaka aende ofisi za CCM, lakini
hakupata msaada wowote zaidi ya kuombwa asubiri hadi wakati wa kipindi
cha Bunge ili apate msaada kwa kuwa ni suala binafsi.
Hata hivyo, wakati akiwa njiani kuelekea katika kituo kimoja cha
runinga kwa ajili ya kutoa kilio chake, mwanafunzi huyo na dada yake
walifuatiliwa na watu wasiowajua, jambo lililowalazimisha kuomba msaada
wa wapita njia.
Hata alipofika katika ofisi za kituo hicho cha runinga, watu watatu
akiwemo mwanamke mmoja walifika wakidai kuwa ndugu wa wasichana hao na
kuwakataza waandishi wasikubali kusikiliza neno lolote, wakati sio
kweli.
Aidha, walitumiwa ujumbe kutoka katika namba ya mmoja wa wafanyakazi
wa makao makuu ya CCM, akiwasihi kufumba mdomo kwa kuwa anawapenda na
hataki wadhurike.
Baada ya jitihada za kuwanyamazisha wasichana hao kushindikana, ndipo
mwathirika alipoanza kupokea ujumbe wa kutishia maisha kupitia katika
namba ya simu ya 078499…. Ikisema: “Waandishi hawatakusaidia kamwe,
Bunge la Katiba likianza watu watakusahau kama uliuawa.
Mtasahaulika
kabisa, subirini mje mzikwe leo usiku kwenu, sitanii, hakuna wa
kunifanya lolote, serikali ndio sisi, salini kabisa.”
Jitihada za kumpata waziri huyo wa zamani na mbunge wa CCM, ziligonga
mwamba. Mara ya kwanza simu yake moja ilipokelewa na mtu
aliyejitambulisha kama dereva wake, na akataka aambiwe sababu za
kumuhitaji kiongozi huyo.
Hata aliposisitizwa kuwa anayehitajika ni mkubwa wake, alitoa namba
nyingine ya kumpata, lakini ilikuwa ikikatwa mara zote ilipokuwa
ikiita.
Mbali ya ujumbe huo wa vitisho, binti huyo alikuwa akitumiwa ujumbe
mbalimbali na watu asiowafahamu, na wengine kumpigia simu wakimwambia
wanajua amejificha wapi na kwamba hawezi kutoka.
Naibu Spika wa Bunge, Job Ndugai, alipoulizwa kuhusiana na tuhuma
hizi nzito, alionyesha kushangaa na kuhoji; “na wewe umeanza kuandika
mambo kama haya?”
“Hilo ni jimbo binafsi zaidi na mimi siwezi kuongea lolote,” alisema na akakata simu.
Tanzania Daima Jumatano, liliwasiliana na Mbunge wa Kilindi, Beatrice Shelukindo, ambaye anadaiwa kulielewa vema suala hilo.
Shelukindo, hata hivyo, licha ya kukubali kuwa alikuwa anajua tatizo
hilo, aliomba asiongee kwa kirefu kwa madai kuwa alikuwa kwenye kikao.
Kamanda wa zamani wa polisi Mkoa wa kipolisi wa Kinondoni, Charles
Kenyela alipulizwa namna alivyoshughulikia jambo hilo, alikana kujua
chochote kwa madai kwamba, mambo kama hayo yanashughulikiwa na dawati
maalumu.
Credit: Tanzania Daima
Credit: Tanzania Daima