WATU
tisa wanashikiliwa na Polisi Dar es Salaam kwa tuhuma za kuvamia
nyumbani na kumjeruhi Mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na
mwanasheria mkongwe, Dk Sengondo Mvungi.
Waziri
wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Emannuel Nchimbi alisema jana Dar es
Salaam kuwa baadhi ya watuhumiwa hao walikutwa na simu iliyoporwa
nyumbani kwa Dk Mvungi pamoja na mapanga yanayodaiwa kutumika katika
shambulizi hilo.
Dk
Mvungi alivamiwa na kushambuliwa wiki iliyopita nyumbani kwake Kibamba
na kupoteza fahamu kukimbizwa katika Hospitali ya Tumbi, Kibaha kabla ya
kuhamishiwa Muhimbili ambako alilazwa katika Taasisi ya Mifupa (MOI) na
kishsa kupelekwa Milpark, Afrika Kusini ambako anatibiwa.
Waziri
Nchimbi alisema baada ya mahojiano ya kina washukiwa hao walikiri
kushiriki tukio hilo na walitoa ushirikiano wa kutosha hadi kupatikana
kwa mapanga hayo na kigoda.
“Uchunguzi
wa Polisi katika tukio hili umekamilika kwa asilimia 80, tumebakiza
watu wachache walioshiriki na tunawahakikishia wananchi kuwa
tutawakamata hivi karibuni,” alisema Nchimbi ambaye alifuatana na Naibu
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Pereira Ame Silima na Mkuu wa Polisi
Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova.
Kova
alitaja waliokamatwa kuwa ni Msigwa Mpopera ambaye ni mlinzi nyumbani
kwa Dk Mvungi ambaye kwa mujibu wa Kova ndiye alikuwa kiongozi wa tukio
hilo na kwamba aliongoza wenzake kufanya shambulio hilo.
Mwingine
ni Chibango Magozi ambaye alikamatwa akiwa na simu iliyoibwa nyumbani
kwa Dk Mvungi. Kamanda Kova alisema baada ya watuhumiwa hao kubanwa
walitaja wenzao na kukubali kwenda kuonesha mapanga waliyotumia kutenda
uhalifu huo.
Wengine
wanaoshikiliwa ni Ahmed Ali, Zakaria Msesa, Manda Saluwa, Paul Jailos
na Juma Khamis ambao wote ni wakazi wa Vingunguti; Longishu Semariki
mwuza tumbaku (ugoro) katika eneo la Msimbazi na Msunga Makenza dereva
wa bodaboda Kitunda.
“Upelelezi
wa tukio hili umefanywa kwa kiwango cha juu na tunashukuru ushirikiano
uliooneshwa na familia na vyombo vya habari,” alisema Kamanda Kova.
Alisema
kazi iliyobaki sasa ni kukamilisha upelelezi na kupeleka jalada kwa
Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) ili atoe kibali cha kesi hiyo kwenda
mahakamani.
Akijibu
maswali ya waandishi wa habari, Kova alisema uhalifu aliofanyiwa Dk
Mvungi hauhusiani na siasa kwani ushahidi unaonesha kuwa watuhumiwa
walikuwa wanatafuta kipato.
Ulimboka, Kibanda
Alipoulizwa
sababu ya upelelezi wa tukio la Dk Mvungi kuharakishwa, wakati kuna
matukio kama ya Mhariri Mtendaji wa New Habari, Absalom Kibanda na
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Madaktari, Dk Steven Ulimboka hadi leo Polisi
iko kimya, Kova alisema watuhumiwa wa Dk Mvungi walipatikana haraka
kutokana na ushirikiano wa vyombo vya habari na familia.
“Unajua
katika tukio hili hazikuwapo habari za Polisi kuhusika au mhusika ni
nani, haya mambo ya upelelezi ukishamtuhumu polisi wakati ndiye anafanya
upelelezi wakati mwingine inakatisha tamaa,” alisema Kova.
Dk Nchimbi alifafanua kuwa matukio ya Dk Ulimboka na Kibanda yanaendelea kufanyiwa uchunguzi.
“Katika
nchi zinazoendelea, upelelezi wa matukio mengine unafanyika hata miaka
mitatu au minne na baadaye watuhumiwa wanakamatwa kirahisi.”
Wakati
huo huo, Dk Nchimbi alisema katika kupambana na uhalifu nchini, Polisi
itasambaza maofisa wake wapatao 200 kila tarafa ambao watashirikiana na
Polisi Jamii kupambana na uhalifu.
-Habari leo