WATU wanne wamepandishwa kizimbani katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, wakikabiliwa na mashitaka ya kuwa wanachama wa kundi la kigaidi la Al Shabaab. Washitakiwa hao waliofikishwa mahakamani jana ni Ally Rashid, Shaban Waziri, Faraji Ramadhani na Mussa Mtweve.
Wakili
wa Serikali, Peter Maugo alidai mbele ya Hakimu Mkazi Sundi Fimbo, kuwa
kati ya Januari 11 mwaka jana na Septemba 16 mwaka huu, eneo la
Kibaoni, Dar es Salaam, Rashid alisajili washitakiwa wenzake kuwa
wanachama wa kundi hilo.
Aliendelea
kudai, kuwa katika siku hizo, washitakiwa walikamatwa kwa kuwa
wanachama wa kundi la kigaidi la Al Shabaab ndani ya Jamhuri ya Muungano
wa Tanzania, ambalo pia linafanya shughuli zake Kenya na Somalia.
Washitakiwa
hao hawakutakiwa kujibu mashitaka kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka
ya kusikiliza kesi hiyo isipokuwa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Aidha,
upande wa mashitaka ulidai kuwa upelelezi wa kesi hiyo bado
haujakamilika na washitakiwa walirudishwa rumande hadi Desemba 5 kesi
hiyo itakapotajwa.
Kesi hiyo imefunguliwa katika Mahakama ya Kisutu katika hatua ya upelelezi na baadaye itahamishiwa Mahakama Kuu kusikilizwa.
Wanavyosajiliwa
Septemba, Shirika la Habari la Uingereza (BBC), lilitoa taarifa fupi ya
namna vijana walivyokuwa wakisajiliwa kujiunga na kundi la kigaidi la
Al Shabaab katika pwani ya Kenya.
Taarifa
hiyo ilitoka baada ya Al Shabaab kukiri kufanya shambulizi la kigaidi
katika jengo lenye maduka makubwa la Westgate jijini Nairobi, ambako
zaidi ya watu 60 waliuawa na mamia kujeruhiwa.
Uchunguzi
wa BBC, ulibaini kuwa vijana hao kabla ya kusajiliwa walikuwa wakipitia
mafunzo yanayopotosha itikadi za dini katika kuwaandaa kujiunga na
kundi la Al Shabaab.
Vikao
vya kusajili vijana hao ilidaiwa huanza na viongozi wa dini walio
tayari kutoa mafunzo hayo, ili watoe hotuba za namna hiyo kwa vijana.
Uchunguzi
huo umebaini kuwa vijana hao, hufundishwa kujitolea kupigania kile
wanachosema ni dini, na baadaye hupelekwa vijijini katika maeneo
yanayopakana na fukwe za bahari kujiandaa na safari kwenda Somalia.
-Habari leo
-Habari leo