Pamoja na ukweli kuwa kulikuwa na
ajenda kadhaa zilizokuwa zimepangwa kujadiliwa katika kikao hicho cha siku
mbili kilichofanyika Dar es Salaam, suala la Zitto ndilo lililochukua muda
mrefu zaidi kujadiliwa.
Habari za kuaminika kutoka ndani ya
kikao hicho zilieleza kuwa wajumbe waligawanyika makundi mawili, baadhi
wakipendekeza Zitto avuliwe nafasi yake ya Naibu Katibu Mkuu kwa maelezo kuwa
anakwenda kinyume na taratibu za chama hicho na wengine wakipinga hatua hiyo
kwa maelezo kuwa haina tija.
Tuhuma zilizokuwa
zikimkabili Zitto Kabwe:
Zitto ambaye pia ni Mbunge wa Kigoma
Kaskazini, mwanzoni mwa Novemba mwaka huu aliingia katika malumbano na Mbunge
wa Arusha Mjini, Godbless Lema kuhusiana na masuala ya posho, akituhumiwa na
Lema kuwa anakataa posho za vikao bungeni, lakini anapokea posho kutoka
mashirika mbalimbali nchini.
Pia, aliingia katika malumbano na
chama chake baada ya kutumia kofia yake ya Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya
Hesabu za Serikali (PAC), kutuhumu vyama vya siasa kuwa hesabu zake
hazikaguliwi na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG).
Kauli ambayo jana Kigaila aliitolea
ufafanuzi na kueleza kuwa Chadema kimekaguliwa na hesabu zake tayari zipo kwa
Msajili wa Vyama vya Siasa.
Mvutano wa jana:
Mvutano wa jana ulianza baada ya
Mbowe kufungua kikao hicho saa 4:00 asubuhi.
Habari kutoka ndani ya kikao hicho zilieleza kuwa baadhi ya
wajumbe, wakiwamo wabunge, walitaka Zitto avuliwe nafasi aliyonayo na kuwa
mwanachama wa kawaida, huku wengine wakipinga hatua hiyo kwa maelezo kuwa Zitto
hakuwepo katika kikao hicho na kwamba alipaswa kusikilizwa.
“Baada ya hali kuwa hivyo, Mbowe
alipendekeza kuwa Zitto asijadiliwe kwa kuwa hakuwepo katika kikao hicho,”
kilieleza chanzo cha habari hizo.
Zitto alikuwa katika safari ya
kikazi huko Sudan Kusini akiwa amefuatana na wajumbe wa PAC.
Taarifa zaidi zinaeleza kuwa Zitto
alitafutwa na alituma salamu kwa wajumbe wa kikao hicho akiwaeleza kuwa alikuwa
njiani na kuahidi kuwa angehudhuria mara tu baada ya kuwasili.
“Zitto alituma ujumbe kuwa anakuja
katika kikao, kilikuwa na ajenda nyingi lakini suala lake lilijadiliwa kwa
kirefu sana,” kilieleza chanzo chetu. Licha ya ombi la Mbowe, bado wajumbe
walishinikiza kuendelea kumjadili Zitto hivyo kusbabisha kuchelewa kujadiliwa kwa
ajenda nyingine.
Tangu juzi, siku ya kwanza ya kikao
hicho, ulinzi uliimarishwa nje ya Jengo la Ubungo Plaza na jana walinzi wa
chama hicho, Red Brigade waliwatimua waandishi wa habari waliokaribia eneo hilo
wakisema hayo ni maagizo kutoka kwa uongozi wa juu.
Yaliyojadiliwa ndani
ya kikao:
Katika ufafanuzi wake kwa waandishi
wa habari jana jioni, Kigaila alisema kikao hicho kilichoanza juzi, kimejadili
mambo mbalimbali. Alisema juzi kikao hicho kilijadili muhtasari wa vikao viwili
vya dharura vya Kamati Kuu vilivyofanyika hivi karibuni.
“Tumejadili taarifa ya uchaguzi
mdogo wa Jimbo la Kiembesamaki, Zanzibar unaotarajiwa kufanyika hivi
karibuni... tunathibitisha kuwa tutashiriki,” alisema.
“Kulikuwa na taarifa ya hesabu za
chama zilizokaguliwa na kupelekwa kwa Msajili wa Vyama vya Siasa na taarifa za
fedha za utendaji kuanzia Kamati Kuu iliyopita mpaka Kamati Kuu ya sasa,”
alisema Kigaila.
Huku akionyesha kitabu cha ukaguzi
wa fedha mwaka 2010/11 na 2011/12 alisema: “Kamati Kuu imeridhika kuwa chama
kimekaguliwa na hatuna deni kwa msajili.
Ajenda za kuhitimisha kikao
jana:
Alisema kikao cha jana kilijadili ajenda za uboreshaji wa
jengo la makao mkuu pamoja na kupanga upya kurugenzi za chama hicho pamoja na
nguvu kazi ya makao makuu ili kuweza kutekeleza vizuri majukumu yake.
“Ajenda inayoendelea hivi sasa ni ya
uundaji wa programu ya `Chadema ni Msingi’, ambayo lengo lake ni kukijenga
chama katika ngazi za chini kabisa. Huu ni mpango mkuu wa chama wa `Vuguvugu la
Mabadiliko’ (M4C). Ajenda ya mwisho itakuwa ni kujadili hali ya kisiasa
nchini.”
Zitto awasili ukumbini usiku
na kuzua malumbano makali:
Zitto alifika katika kikao hicho
jana saa 2.24 usiku akiwa na walinzi wanne na habari kutoka ndani zinasema
kwamba mara baada ya kuingia, ajenda ya kumjadili ilirejea. Ilielezwa kwamba
alipewa nafasi ya kujitetea baada ya kusomewa mashtaka yaliyokuwa
yakimkabili.
Baada ya kurejeshwa kwa agenda hiyo
malumbano makali yalizuka kwani wajumbe walikuwa wazungumza kwa sauti za juu na
jazba kiasi cha kusikika nje.
Taarifa zaidi zinaarifu kuwa malumbano hayo yalifikia tamati kwa kumvua Zitto Kabwe nafasi zote za uongozi ndani ya CHADEMA ikiwemo ile ya Naibu Katibu Mkuu wa chama pamoja na nafasi ya Naibu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.
( Habari kwa hisani ya mdau Albert Robert na gazeti la Mwananchi.)