Akizungumza na Mwanaspoti, Lina anasema kuwa anapenda viatu kuliko kitu kingine chochote kiasi kwamba anaweza kushuka kwenye gari sehemu yoyote kama ameona kiatu kizuri dukani.
Anasema kuwa hata kama akivaa nguo ya siku nyingi kiasi gani, lakini kama miguuni amevaa kiatu kipya hujisikai huru na mwenye furaha, kuliko akikosa kiatu anachokipenda.
Anasema chumbani kwake ana jozi 50 ya viatu anavyovivaa, lakini pia anazo jozi nyingine 30 za viatu ambavyo bado hajavivaa kabisa kwani bado anatafuta nguo za kuvalia viatu hivyo.
“Yaani hapa naona bado kabisa. Ninaongeza viatu karibu kila siku maana ninavyoviona madukani vipo vya kila aina nami napenda sana viatu, ” anasema.
Aliongeza kuwa hajawahi kuishi bila kutamani kununua kiatu ambacho amekiona mahali na kila akinunua anakutana na kingine, hivyo siku zote ameishi akinunua viatu bila kujali idadi ya alivyo navyo.
Kwa upande mwingine, Lina anasema kuwa kama akiambiwa achague kati ya kusafiri, kuangalia luninga na kusoma vitabu, atachagua kusafiri kwa kuwa akiwa safarini anajifunza vitu vingi kwa kuona na si kuhadithiwa. Aidha anasema kuwa awapo safarini, husinzia kwa bahati mbaya tu lakini ingekuwa ni uwezo wake asingekuwa akisinzia hata kidogo ili aweze kuona kila kilichopo njiani.
“Kama nimelala safarini ujue ni kwa bahati mbaya, lakini mimi mwenyewe huwa sitaki kabisa. Huwa ninataka nione kila kitu cha njiani, ni raha yangu pia,” anasema.
Anaendelea kueleza baadhi ya vitu anavyovipenda katika maisha yake kuwa ni pamoja na kuvaa magauni ya mtindo wowote, iwe mafupi au marefu.
Anasema kwa kuwa ana umbo la kuvutia, haoni haja ya kujibana kwa kupenda kuvaa suruali kama wasichana wengi wa siku hizi.
“Huwa navaa suruali sikatai, lakini sipendi sana kwa kuwa sipendi kujibana na ndiyo maana napenda kuvaa magauni ambayo kama una shepu nzuri hayana shida. Kwa jinsi nilivyo, kila nguo nikivaa naiona sawa kwa kuwa nipo poa,” anasema.
Anafafanuwa kuwa siyo kwamba havai nguo nyingine, anavaa kwa kuwa hawezi kuvaa nguzo za aina moja kila siku, lakini ili awe huru na kuona amependeza, huvaa gauni.