Like Us On Facebook

Kauli ya Serikali baada ya wafanyabiashara wa Kariakoo kugoma jana.


SERIKALI imesema imezungumza na wasambazaji wa mashine za kutolea risiti za elektroniki (EfDs) ili kila aina iuzwe kwa bei yake.
 
Naibu Waziri wa Fedha, Saada Mkuya Salum alisema hayo jana Dar es Salaam akizungumzia mgomo wa wafanyabiashara wa eneo la Kariakoo. Kwa sasa mashine moja ya EfDs huuzwa Sh 800,000.
 
Alisema suala la mashine hizo litafanyiwa kazi lakini pia akasisitiza kutolewa kwa elimu kwa wafanyabiashara hao kuhusu umuhimu wa mashine hizo.
 
“Ninaamini kuwa hilo litafanyiwa kazi… wananchi wa kawaida hawajaridhishwa nazo, lakini ifahamike kuwa mfumo wa kutolea risiti utasaidia kuweka kumbukumbu za hesabu,” alisema Saada.
 
Alisema mfumo huo umeunganishwa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ili kufanya tathmini ya mapato na nchi iweze kuendelea kutokana na mapato yake ya ndani.
“Wiki iliyopita tulizungumza na wasambazaji kuhusu bei za mashine hizo… Sh 400,000 kwa kila mashine ilikuwa ni bei kikomo, lakini tumewaambia kuwa kila aina iwekwe bei ili mfanyabiashara aangalie anayoweza kumudu.
 
Aidha, alisema ununuzi wa mashine hizo kulikuwa na uwazi zaidi lakini amekuwa akishangaa kuona wafanyabiashara katika baadhi ya mikoa wakizuia wengine kuzinunua.
 
Hizi mashine za Efds zinazouzwa hapa ziko katika mfumo wa Tanzania na zinatumia mifumo ya TRA,” alisema Saada na kuongeza kuwa kila mfanyabiashara atakayenunua mashine mwisho wa mwaka mapato yake yataangaliwa.
 
Alisema ununuzi wa mashine hizo ulikuwa ni mpango mzuri wa Serikali kukusanya mapato yake ya ndani ili kuacha kutegemea wafadhili na kuwapo haja ya kuzidisha elimu kuhusu umuhimu wa hizo mashine.
 
Jana, mamia ya wafanyabiashara wa Kariakoo waligoma kufungua maduka na kusababisha shughuli zote za biashara kusimama wakipinga matumizi ya mashine hizo.
 
Hatua hiyo mbali na kusababisha adha kwa wananchi wa ndani na nje ya Jiji na nchi za jirani waliofika kununua bidhaa mbalimbali kutoka maduka hayo, pia ilitajwa kuathiri uchumi wa wananchi kutokana na mzunguko wa fedha kusimama.
 
Wazungumza
Wakizungumza juu ya mgomo huo, baadhi ya wafanyabiashara walisema kilichosababisha mbali na suala la EFDs, pia wanapinga uwepo wa kodi mbalimbali walizodai hazina msingi wowote.
 
Mmoja aliyejitambulisha kuwa ni Hussein Rashid alisema utumiaji wa mashine hizo ni sawa na kuendelea kukandamizwa kwa madai kuwa wakati bado wanapigana na mateso ya kodi nyingi katika biashara zao wameongezwa kodi zingine.
 
Akizungumza na gazeti hili mmoja wa wafanyabiashara ambao walilazimika kufunga maduka, Mahmoud Khalfan alisema mashine hizo ni ghali. Alisema haoni faida ya kuzitumia kwa kuwa hawakupewa muda wa kujifunza mambo mengi.
 
“Mimi naona huu ni mradi wa watu kwa kuwa kwanza biashara gani inakwenda kienyeji namna hii yaani wanatupangia tu na kutulazimisha wakati ilikuwa inatakiwa kwanza elimu kidogo,” alisema.
 
Mfanyabiashara wa vifaa vya umeme, Sultan Haroun alisema hakubaliani na matumizi ya vifaa hivyo.
 
Alisema kuwa akitumia kifaa hicho inakuwa vigumu kushusha bei kwa wateja kwa kuwa hata kama akiuza kifaa cha Sh 30,000 kwa Sh 25,000 mashine hiyo itaandika Sh 25,000 na kutozwa ushuru huo huo na mwisho wa siku atakuwa amepata hasara.
 
Mgomo batili
Hata hivyo, Mshauri wa Jumuiya ya Wafanyabiashara katika Soko Kuu la Kariakoo Johnson Minja, alisema Jumuiya hiyo ilishapata taarifa kutoka TRA ikiwataka kujiandaa na mfumo wa kutumia mashine hizo kuanzia Novemba 15.
 
Alisema baada ya kupewa taarifa hiyo Jumuiya ilimwandikia barua Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdalla Kigoda Novemba 4 kuomba kukutana naye na kuongeza kuwa cha kushangaza “kabla hilo halijatimia wafanyabiashara hao wameamua kugoma.
 
“Hadi leo bado mipango yetu ya kuonana na Waziri ilikuwa ikiendelea kwa bahati mbaya imekuwa ikishindikana kutokana na ratiba za Waziri kuwa ngumu kama mtakumbuka hivi karibuni alikuwa katika msafara wa Waziri Mkuu uliokuwa China, hivyo ukweli bado jitihada zetu zinaendelea,” alisema Minja.
 
Alisema mgomo huo hauna baraka zozote za Jumuiya hiyo na kwamba suala hilo limetokea kutokana na mikakati iliyokuwapo kwa wafanyabiashara hao kupitia mtu mmoja mmoja na hasa ikizingatiwa kuwa walitakiwa kuanza kuzitumia mashine hizo Ijumaa iliyopita.
 
Taarifa kutolewa
Kaimu Mkurugenzi wa Huduma na Elimu kwa Walipakodi wa TRA, Diana Masalla, alisema watatoa taarifa rasmi kuhusu suala hilo wakati wowote na kwamba kuna vikao vinaendelea kati ya TRA na Wizara ya Viwanda na Biashara.
 
Pamoja na mgomo huo, hakukuwa na vurugu zozote kutoka kwa wafanyabiashara hao huku magari ya Polisi yakiranda hapa na pale kudhibiti usalama.

-Habari Leo
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari