Like Us On Facebook

JESHI LA POLISI LAOMBWA KUWEKA ASKARI WA KUWAVUSHA WALEVI BARABARANI ILI WASIGONGWE NA MAGARI WAKITOKA KUCHAPA ULABU NYAKATI ZA USIKU.


KATI ya vitu vilivyoonesha kushangaza wengi wakati wa kilele cha wiki ya usalama barabarani kilichofanyika hivi karibuni mkoani Dodoma ni baadhi ya wakazi za eneo la Chaduru kutaka Kikosi cha Usalama Barabarani cha Jeshi la Polisi kuweka askari wa kuvusha walevi ili wasiendelee kufa kwa kugongwa na magari hasa nyakati za usiku katika eneo hilo.
Eneo hilo pamoja na lile la Kizota limekuwa na ajali nyingi kutokana na kuwa na vilabu vya pombe za kienyeji karibu na barabara kuu.
 
Si binadamu pekee wamekuwa wakigongwa katika eneo la Kizota bali hata mbwa na paka ambao wamekuwa wakifika vilabuni kwa ajili ya kutafuta makombo ya nyama kutokana na eneo hilo kuwa maarufu kwa uchomaji wa nyama na utumbo.
“Eneo hili watu wengi wanaogongwa ni walevi wanaotoka vilabuni wakiwa wamelewa. Kutokana na ulevi, mtu anaingia barabarani akiwa hatambui kama anavuka barabara na gari kama liko kwenye mwendo kasi,” anasema mkazi wa Chaduru, Juma Shabani Shabani anasema ni bora kungekuwa na alama za madereva kupunguza mwendo wanapofika kwenye maeneo hayo kwani kukosekana kwa vibao vya tahadhari imekuwa ikisababisha ajali hata nyakati za mchana.
Wakazi hao ambao walikuwa wakizungumza na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma ambaye alitembelea eneo la Chaduru na Kizota manispaa ya Dodoma akiwa na Mkuu wa Kikosi cha Usalama barabarani Mkoa wa Dodoma, Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Peter Sima na wadau wengine, walisema Jeshi la Polisi linatakiwa kutoa elimu za mara kwa mara ili kupunguza tatizo la ajali ambazo zinaweza kuzuilika.
Naye Athumani Abdalah anasema ajali nyingi zinazotokea katika eneo la Chaduru lenye vilabu vingi vya pombe za kienyeji zinaweza kuepukwa endapo hatua zitachukuliwa kwa kugundua nini kinaendelea mahala hapo, hususan nyakati za usiku.
Tunaomba Serikali kuweka askari ili kuvusha walevi katika eneo hili ili wasiendelee kupoteza maisha kutokana na kugongwa na magari... Wakishautwika mtindi wanavuka bila tahadhari,” anasema mkazi huyo.
Anasema hakuna ubishi kwamba ulevi umekuwa chanzo kikubwa cha ajali eneo hilo na kwamba jambo hilo linatakiwa kuangaliwa kwa makini kama kweli mkoa wa Dodoma umedhamiria kupunguza ajali za barabarani zinazosababisha vifo.
Anasema askari wa usalama barabarani wakiwekwa kwenye maeneo hatarishi kama hilo la Chaduru itapunguza tatizo laajali. Kutokana na kauli hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk Rehema Nchimbi anasema hilo ni jambo lisilowezekana kwani hakuna utaratibu wowote duniani unaoruhusu kuvusha walevi barabara.
Anasema serikali haiwezi kufanya kitu kama hicho na hakuna Serikali yoyote duniani yenye utaratibu wa kuvusha walevi bali kinachotakiwa ni walevi kuwa makini wanapovuka barabarani.

 Mkuu wa mkoa aliwataka wananchi wa eneo hilo kuachana ama kupunguza ulevi kwani mbali na kugongwa, pombe zina madhara ya kiafya kwa wale wanaoendekeza sana pamoja na kupunguza kipato kwa ajili ya ustawi wa familia.
Muwe mnakunywa kwa kiasi si kwa kupitiliza. Mtu analewa hadi anakosa kumbukumbu na kufahamu kuwa hii ni barabara na anatakiwa kupita kwa uangalifu,” anasema.
Aliwataka wananchi hao kuheshimu michoro ya usalama barabarani na hata kulinda alama hizo badala ya kuzitoa hali inayofanya magari kukosa ishara ya kutambua kama kuna alama au michoro katika eneo hilo.
Anasema askari wa usalama barabarani wanatakiwa kuvusha watoto, wenye ulemavu, wenye mahitaji maalumu lakini si walevi.
Dk Nchimbi anasema jambo lingine linalochangia ajali ni pamoja na wananchi kufanya biashara kwenye maeneo ya hifadhi ya barabara. Anasema katika eneo la Kizota wengi wamepanga bidhaa zao za vyuakula, nguo na hata nyama kando ya barabara na kusababisha njia ya waenda kwa miguu kukosekana, kitu ambacho ni hatari.
Mkuu wa Mkoa anataka ugumu wa maisha na hata umasikini usiwe sababu ya watu kuvunja sheria kwa kufanya biashara katika maeneo hatarishi.
Anasema ni muhimu kwa viongozi wa Serikali za Mtaa kukaa na wananchi na kutafuta maeneo mengine ya kufanyia biashara na kuepusha idadi kubwa ya watu wanaopoteza maisha katika eneo hilo.
Katika eneo la Kizota, takwimu zinaonesha kuwa katika kipindi cha miaka mitatu jumla ya watu 49 walipoteza maisha kutokana na kugongwa na magari.
“Hapa Kizota tatizo ni kilabu kuwa karibu na barabara, mtu akilewa anatimka haangalii kama kuna gari linakuja au vipi anajitosa barabarani na kujikuta akigongwa na kufa,” anasema mkazi wa eneo hilo, John Mapiga Anasema ajali nyingi zimekuwa zikitokea nyakati za usiku na kwamba mtu akiwa amelewa, tena peke yake anakosa maamuzi sahihi na kujikuta akigongwa.
Ukilewa hata gari ikiwa karibu unaliona kama liko mbali si kwa vile ni usiku na taa inamulika. Ulevi ni mbaya lakini huwezi kumzuia mtu kunywa pombe kwa vile atagongwa na gari dawa ni kunywa kwa kiasi unatoka kilabuni na unafika nyumbani salama,” anasema. Anasema hakuna anayeweza kumzuia mtu kunywa pombe lakini inawezekana kumfundisha mtu kuchukua tahadhari pindi anapovuka barabara akiwa amelewa.

 
Kwa upande mwingine, Mkuu wa Mkoa anataka kuwe na mikakati ya kuweka rekodi za madereva wa magari na waendesha pikipiki ambao mara kwa mara wamekuwa wakisababisha ajali ili ikibidi sheria zilizopo zitumike kuzuia leseni zao.
Kwa mujibu wa takwimu, jumla ya watu 727 wamepoteza maisha mkoani Dodoma kutokana na ajali za barabarani katika kipindi cha mwaka 2010 hadi Septemba mwaka huu.
Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani mkoani Dodoma, Peter Sima anasema watu hao walipoteza maisha katika ajali 585 zilizotokea zikahusisha vifo hivyo katika maeneo mbalimbali mkoani Dodoma.
Anasema mbali na ajali hizo za barabarani pia jumla ya ajali 784 zilizotokea katika kipindi hicho zilizosababisha watu 1919 kujeruhiwa.
Pamoja na hayo, Sima anasema Kikosi cha usalama barabarani kimekusanya jumla ya Sh milioni 670.6 kutokana na faini mbalimbali walizotozwa madereva waliokiuka sheria za usalama barabarani katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka huu.
Aidha katika kipindi hicho jumla ya madereva 21,680 walikamatwa kutokana na makosa mbalimbali ya kuvunja sheria za usalama barabarani ambapo walilipa faini jumla ya Sh milioni 670.6. Sanjari na madereva wa magari waliokamatwa madereva wa pikipiki maarufu kama bodaboda walikuwa 3,036.
Anabainisha kuwa jeshi hilo kwa kushirikiana na Chuo cha Ufundi Stadi (VETA) na shule ya Udereva ya Dodoma katika kipindi cha Januari hadi Septemba waendesha pikipiki wapatao 2292 walipata mafunzo na kati ya hao 1,140 walipata leseni za kuendesha pikipiki.
Sima anasema katika kupambana na ajali za barabarani katika mkoa wa Dodoma, Jeshi la Polisi kwa kushirikiana na wadau mbalimbali limejipanga katika mpango mkakati ikiwemo kurusha kipindi maalumu cha usalama barabarani katika vituo mbalimbali vya redio vya mkoani Dodoma.
Anasema mpango mwingine ni kuendelea kutoa elimu katika mikusanyiko ya watu kama vituo vya mabasi na vituo vya waendesha pikipiki pamoja na kutoa vipeperushi vya safari salama kwenye shule za msingi na sekondari.
Anasema katika kipindi cha Januari hadi Septemba mwaka huu jumla ya wanafunzi 3,055 wamepewa elimu ya usalama barabarani na kati yao wanafunzi wa shule za msingi ni 1,764 na za sekondari ni 1,309.

Sima anasema mikakati mingine ni kufanya ukaguzi wa magari hususani mabasi yanayosafiri mikoani na Wilayani kuhakikisha yako salama kabla ya kuanza safari.
Aidha kuwapima madereva ulevi kabla ya kuanza safari na kufanya ukaguzi wa kushtukiza katika barabara kuu za mkoa na barabara nyingine kwa kutumia vipima mwendo kasi kwa lengo la kuwabaini madereva wanaokwenda mwendo kasi na kuwachukulia hatua za kisheria.
Anasema licha ya wanaofanya makosa kutozwa faini, hatua hiyo imeonekana haitoshi bali kinachohitajika ni kupiga hatua zaidi ya hiyo ikiwa ni pamoja na elimu.



Pia watumiaji wote wa barabara wana wajibu kuzingatia sheria ikiwemo utunzaji wa hifadhi za barabara kwani kuna tatizo la watu kuvamia hifadhi za barabara na kuzitumia kwa matumizi binafsi kama gereji ama kufanya biashara mbalimbali.
“Uvamizi huo ni kosa kwa mujibu wa sheria za usalama barabarani pia ni kikwazo inapotokea barabara inayotumika imefungwa kwa namna moja au nyingine,” anasema.

Hifadhi za barabara eneo la Dodoma Inn, barabara ya mzunguko ya barabara za Arusha hadi ya Bahi ni baadhi ya sehemu ambazo hifadhi za barabara zimevamiwa.
Anasema kamati ya usalama barabarani inatoa ushauri kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu (CDA) na Manispaa kuona uwezekano wa kujenga stendi ya mabasi ya masafa marefu nje ya mji ili kuondoa msongamano wa magari mjini ambao tayari umeshaonekana kutokana na kuongezeka kwa magari. Aidha wadau wanashauri ziwekwe alama za barabarani, ikiwa ni pamoja na alama za vituo vya daladala katika barabara za manispaa na barabara kuu.
Wanadi wanataka pia wakala wa barabara waone uwezekano wa kuweka taa za kuongoza magari katika makutano ya barabara eneo la Ndasha, Chuo cha Biashara na Kilimo/Relini.
Kadhalika halmashauri ya manispaa ya Dodoma inashauriwa kujenga stendi muafaka za daladala kwani stendi ya Jamatini ni ndogo na isitoshe haiko kwenye mazingira rafiki ya mahitaji.
----Habari Leo

TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari