Like Us On Facebook

HALI BADO NI MBAYA CHADEMA ..Zitto Kabwe amburuza polisi katibu wa chama hicho akimtuhumu kuusambaza waraka wa siri uliomchafua



WAKATI Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kikimwandikia Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe barua ya kumtaka ajieleze dhidi ya tuhuma zinazomkabili, yeye ameamua kukimbilia polisi akimshitaki mmoja wa viongozi wenzake.
 
Habari za kuaminika zimedai kuwa Zitto ambaye hivi karibuni alivuliwa cheo chake cha unaibu katibu mkuu wa CHADEMA, inadaiwa amefungua mashitaka polisi akimtuhumu Katibu wa CHADEMA Mkoa wa Dar es Salaam, Henry Kileo kwa madai ya kusambaza waraka katika mitandao ya kijamii.
 
Akithibitisha tukio hilo, wakili wa Kileo, Peter Kibatara, alisema kuwa mteja wake amemriwa kufika makao makuu ya Jeshi la Polisi leo Jumatano saa nane mchana na kuonana na mmoja wa maofisa wa juu wa jeshi hilo, aliyetajwa kwa jina moja tu la Mbutta, kufuatia mashitaka yaliyofunguliwa na Zitto dhidi yake.
 
Akizungumza kwa njia ya simu na mwandishi wetu, Kileo alikiri kuitwa polisi, ingawa alidai hajui ni waraka gani anaotuhumiwa kuusambaza unaomchafua Zitto.
 
“Kwa kweli sijui hata mimi ni waraka gani, ingawa hivi karibuni kulikuwa na waraka wa siri uliodaiwa kutoka CHADEMA, na ambao ulijaa tuhuma za usaliti. Lakini huo tuliishaukana siku nyingi. Labda kuna mwingine,” alisema Kileo.
 
Zitto kutwa nzima ya jana hakuweza kupatikana kwa njia ya simu kufafanua mashitaka aliyofungua polisi. Simu zake zote za kiganjani zilikuwa zimezimwa.

-Tanzania daima.
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari