Absalom Kibanda |
Pamoja na tuzo hiyo, Kibanda pia alipata zawadi ya fedha taslimu ya kiasi cha Sh10 milioni kwenye shughuli hiyo iliyoandaliwa na Umoja wa Klabu za Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC).
Tuzo hiyo ilianzishwa ikiwa ni heshima kwa Mwandishi wa habari wa zamani wa Kituo cha Televisheni cha Channel 10, Daudi Mwangosi, ambaye aliuawa Septemba 2, mwaka 2012 na askari polisi waliokuwa wanatawanya wafuasi wa Chadema huko Mafinga mkoani Iringa.
Akizungumza baada ya kukabidhiwa zawadi hizo jana, Kibanda alisema kitendo cha kukabidhiwa tuzo hiyo ni uthibitisho kuwa aliteswa na kujeruhiwa kutokana na masuala ya kikazi na si vinginevyo.
“Nawashukuru majaji waliotambua na kunichagua kupata tuzo hii ambayo ni ushahidi tosha kuwa tukio lililonipata pasipo shaka linatokana na kazi yangu ya uandishi.
Uchunguzi wa jambo hili umekuwa kimya hadi leo na badala yake maneno yamekuwa yakisambazwa kwenye balozi kwamba niliteswa kwa mambo binafsi,” alisema Kibanda, baada ya kukabidhiwa tuzo hiyo na Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications, Tido Mhando.
”Ifike wakati waandishi wote tufikirie kwa makini kuwa viongozi wa siasa waliopo madarakani na wengine walishatoka, ndiyo wamekuwa wakitutangaza kama wasaliti, wachochezi na kama maadui na ndiyo maana wanapeleka miswada kandamizi bungeni wakati wamekuwa wakitutumia katika mambo yao mengi, tujiulize kama tunajitendea haki,” alisisitiza.
Kibanda alisema pia kifo cha Mwangosi na kipigo alichopata yeye na Said Kubenea kinapaswa kuwafanya waandishi kuchukulia kama sababu kubwa ya kuwafanya wasonge mbele na kuendelea kutekeleza majukumu yao huku wakiweka pembeni maumivu na mateso waliyoyashuhudia kwa wenzao.
Kibanda aliamua kutoa asilimia 10 ya fedha alizopewa kanisani wakati nusu ya fedha itakazobaki itakwenda kwa mke wa Mwangosi.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited, Tido Mhando, alisema kuwapo kwa matukio ya kufungiwa kwa magazeti ya Mwananchi, Mtanzania Mwanahalisi pamoja na kujeruhiwa na kuuawa kwa waandishi, ni kielelezo cha kuminywa kwa uhuru wa habari.
Alisema hata hivyo matukio haya hayapaswi kuwavunja moyo waandishi wa habari katika kutimiza wajibu wao.
Pia aliwataka kusimamia taaluma yao na maadili ya kazi zao ikiwa ni pamoja na kuwajibika katika uandishi huku wakizingatia weledi. Mhando aliwataka waandishi wa habari kutokubali kutumiwa na wanasiasa.
CHANZO: Mwananchi