WAHUDUMU
baa, saluni, mama lishe na vijana wa bodaboda wilayani Sikonge mkoani
Tabora wametakiwa kujiheshimu na kuwa waadilifu wanapofanya kazi zao ili
kujiepusha na vishawishi mbalimbali wanavyokumbana navyo katika
mazingira ya kazi zao.
Watoa
huduma hao wamesisitizwa kuheshimu kazi zao kwani ni ajira inayowapa
riziki sawa na ajira zingine na sio kuendekeza tamaa za mapenzi na pesa,
jambo linalohatarisha maisha yao.
Hayo
yamebainishwa jana katika semina ya siku moja iliyofanyika katika
ukumbi wa Chuo cha Maendeleo ya Wananchi wilayani Sikonge iliyowahusisha
wahudumu wa baa, saluni, mama lishe na waendesha bodaboda.
Hali
hiyo imeelezwa itawasaidia na kuwa salama zaidi na hivyo wametakiwa
kujiheshimu, kujilinda na kujiepusha na vishawishi vya namna hiyo kwani
vinachangia maambukizi ya magonjwa ya ngono na virusi vya Ukimwi.
Akizungumza
wakati wa ufunguzi wa semina hiyo kwa niaba ya Mkuu wa wilaya,
Themistocles Byarugaba, Ofisa Maendeleo wa wilaya alisema lengo la
semina hiyo ni kuelimisha vijana wa kike na kiume namna ya kujikinga na
kujiepusha na maambukizi ya magonjwa ya zinaa na Ukimwi katika maeneo
yao ya kazi.
Alisema
kundi hilo hasa mabinti wanapaswa kuwa makini katika maeneo yao ya
kazi, kwani vishawishi vingi huanzia kwao kupitia uvaaji ambapo baadhi
yao huacha wazi eneo fulani la maumbile yao, hali inayochochea matamanio
kwa wanaume.
Alisema
katika hili akina dada hao wanatakiwa kujiheshimu wanapohudumia wateja
wao na sio kukubaliana na kila kitendo wanachofanyiwa na wateja.
"Ninyi
wahudumu wa baa, saluni na mama lishe acheni tabia ya kujirahisisha na
kuwa ombaomba mnapowaona wateja, jiheshimuni, ridhikeni na mnachopata,
jifunzeni kusema hapana msikubaliane na kudhalilishwa na wanaume,
heshimuni kazi zenu, …… mkijiheshimu mtajiepusha na maambukizi ya
Ukimwi," aliongeza.
Alisema
halmashauri ya wilaya hiyo ina mpango wa kuanza kutoa mikopo kwa akina
dada wanaofanya biashara ya ngono ili waachane na biashara hiyo, hali
ambayo itawapunguzia umasikini sambamba na kuthibiti ukahaba unaofanywa
na mabinti hao wilayani humo.
Nao
Tito Luchagula Ofisa Ustawi wa jamii, Nicholous Magoha Ofisa Maendeleo
ya jamii, Lwise Moshi Ofisa Maendeleo na Godfrey Kingamkono mhudumu wa
maabara katika hospitali ya Misheni wilayani humo wakitoa mada kwa
nyakati tofauti walibainisha kuwa semina hiyo ni muhimu sana kwa
maendeleo na ustawi wa vijana wilayani humo.
Walisema
kuwa kwa sababu wengi wao wanakabiliwa na changamoto nyingi katika
maeneo yao ya kazi hali inayowafanya wajiingize katika vitendo viovu
ikiwemo kuambukizwa magonjwa ya zinaa na Ukimwi.