Askari polisi wa Kituo Kidogo cha Polisi cha Mabibo, wanatuhumiwa kuwapiga na kuwavunja miguu na mikono, wakazi wawili wa eneo la Jitegemee.
Tukio hilo lilitokea Oktoba 17 mwaka huu saa 5
usiku wakati wakazi hao, Maulid Yahaya na Willium Six, wakiwa wanakunywa
vinywaji kwenye duka lililopo eneo la Mabibo Mwisho.
Habari zilisema wakati watu hao wakijiburudisha,
alijitokeza mtu mmoja na kuaanza kuwafanyia fujo jambo lililosababisha
wote wawili kupelekwa kwenye Kituo Kidogo cha Polisi Mabibo.
Akizungumzia tukio hilo, Yahaya alisema wakati
tukio hilo likiendelea kufanyika, mtu huyo alichukua filimbi na kuanza
kuipiga ndipo walijitokeza watu na kuwapeleka kwenye kituo hicho.
Alisema walipofikishwa kituoni, ilitolewa amri na
polisi kuwa wapigwe kabla ya kuingizwa mahabusu ndipo alipojitokeza
askari polisi mwingine akiwa na mgambo ambao walianza kuwashambulia kwa
kutumia visu na virungu huku wakiwa wamefungwa pingu.
Alisema ilipofika saa 9 usiku walifuatwa na gari
la polisi na kuhamishiwa kwenye Kituo cha Polisi cha Urafiki ambako
walikaa mahabusu siku mbili bila ya kupelekwa hospitali.
Yahaya alisema wakiwa mahabusu waliwaomba askari
polisi, ili waweze kupelekwa hospitalini kwa ajili ya kupatiwa huduma
kutokana na majeraha waliokuwa wameyapata.
"Tunataka
kujua sheria ipi inamruhusu askari polisi kumpiga raia akiwa mahabusu
bila ya kusikiliza maelezo yake,” alisema Yahaya.
Kwa upande wake, Six alisema Oktoba 19 mwaka huu
saa 8 mchana waliruhusiwa kutoka kituoni baada kesi yao kufutwa na mtu
aliyewafanyia fujo wakati wanakunywa vinywaji.
Alisema baadaye walimfuata mmoja wa askari na
kumweleza kuwa walipigwa na askari wa Kituo Kidogo cha Polisi Mabibo
lakini alikataa kuchukua maelezo yao.
Six alisema walipelekwa Kituo cha Afya cha Sinza
ambako walipigwa picha ya X-ray na kugundulika kuwa mguu wake wa kushoto
umevunjika mara mbili huku Yahaya akiwa amevunjika mkono.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Kinondoni, Camilius Wambura, alisema hajata taarifa na kwamba anafuatilia.