Gari likiwa limepinduka bondeni. |
Mwimbaji anayetamba na
wimbo wa "Zawadi gani nitamtolea BWANA" ambaye pia ni mtume akichunga
kanisa jijini Dar es Salaam John Komanya amepata ajali mbaya juzi mchana
maeneo karibu na daraja la Mto Wami akiwa njiani kuelekea mkoani Arusha
kukutana na viongozi wanaohudumu na mwalimu Christopher Mwakasege, kwa
ajili ya mkutano wa injili ambao utakuwa na lengo la kuombea taifa kwa
siku nne mwezi Disemba.
Akizungumza na GK mtume
Komanya amesema lengo lilikuwa ni kupeleka barua kwa viongozi hao ili
wamfikishie mwalimu Mwakasege kwaajili ya mkutano huo. Amesema akiwa
njiani katikati ya Msata na Wami na wakati huo hakuwa amefunga mkanda wa
gari, ndipo akasikia sauti ya Roho Mtakatifu ikimwambia kwa upole
afunge mkanda lakini akawa anapuuzia na kuanza kujiuliza kwanini, sauti
ikarudia tena kwa upole ikimwambia afunge mkanda akiwa bado anajiuliza
ndipo anasema akasikia sauti ya Mungu ikizungumza kwa haraka na ukali
"John funga mkanda" ndipo akafunga mkanda.
Mtume Komanya amesema
akiwa anateremka kuelekea wami akiwa katika mwendo wa 180 wakati akipita
katika kona kulikuwa na malori matatu mbele yake kukawa na lori lingine
likifuatiwa na mabasi matatu yakipandisha kutoka Arusha kuja Dar, kwa
wakati huo aliona malaika saba ambapo walishuka mithili ya makomandoo
washukavyo kutoka kwenye kamba ya helikopta, mmoja akiwa amekaa kwenye
boneti mbele, mwingine kulia, kushoto na mwingine nyuma yake ambaye
alimwambia Komanya afuate maelekezo yake, anasema akiwa anamwangalia
malaika aliyekaa karibu naye katika kiti cha dereva aliambiwa afuate
maelekezo anayopewa na malaika wa nyuma yake.
Alipokuwa akiangalia
mbele akaona gari linayapita mengine kwa spidi hali iliyomfanya Komanya
kutaka kuingia katikati ya magari mengine lakini malaika akamwambia
afuate maelekezo yake na kuambiwa aachie uskani jambo ambalo alilipinga
kwakuwa aliona kifo mbele yake na kutaka kuingia katikati ili kukwepa,
lakini malaika akamwambia ukiingia katikati utakufa, wewe achia usukani
kama ninavyokwambia kwakuwa wametumwa kumlinda, akawa bado anatafakari
kutokana na kuliona korongo kubwa upande wake huku malaika wakimwambia
asiguse kitu chochote ikiwemo kutokanyaga breki lakini bila kusikia
akakanyaga na kusababisha gari kuyumba sana, malaika akamwambia tena
aachie breki na kuweka mikono yake kifuani. Anasema alipoweka mikono
kifuani aliona wakiligonga lori huku malaika akiwa ameshika usukani na
kuonyonga sana huku yeye akisema alijikuta akiwekwa kwenye kitu kama
chupa ya maji, na yeye kwa wakati huo kuona kama vile yupo ndani ya
glasi ya maji, ila anaona kinachoendelea.
Kisha baada ya hapo,
upande wake wa usukani ndio uliogongwa, mara baada ya malaika kuchezesha
usukani kidogo ili kuepusha madhara zaidi, na kisha ile semi-trailler
ikamtupia kwenye korongo na kubinuka mara tatu hewani kabla ya kutua
chini kwa mara ya nne, ambapo gari ilikuwa juu chini, yaani matairi
yakiwa yanatazama juu.
Baada ya hapo
kilichofuata ni kuendelea kusikiliza malaika wasemacho, ambapo hapo
alisikia sauti ikisema fungua mkanada utoke, na kwa wakati huo kulikuwa
na moshi ullioanza kutoka kwenye gari - na hapo akapewa dakika 12
kuchukua baadhi ya vitu alivyokuwa navyo kwenye gari. Maajabu ya Mungu,
hakuna kitu chochote kilichogusa mwili wake, na wala hakuna damu
iliyovuja kutokana na gari hilo kupindukia kwenye korongo.
Hakika utukufu ulimrudia
Mungu kwa wakati huo kwani baadhi ya mashuhuda walikiri hapohapo ya
kwamba hakuna mtu anayeweza kusalimika kwenye ajali hiyo, bali ni lazima
tu mkono wa Mungu umehusika hapo kuokoa.
Baadhi ya mashuhuda
ambao walikuwapo kwenye mabasi ya mkoa (hadi mkoa) walimtambua mtumishi
wa Mungu ya kwamba ni John Komanya na hatumaye kumshukuru Mungu
hapohapo, ambapo baadae Polisi walifika kwa ajili ya kazi yao - lakini
hilo halikumzuia Mchungaji Komanya kupiga magoti na kumshukuru Mungu
licha ya umati wa watu - na tukio hilo liliambatana na yeye kuisikia
sauti ya Mungu ikimwambia "Nimekupa kazi ya kutengeneza kanisa langu,... usiogope nitakulinda, ila kuwa mwaminifu na nitakuweka kwenye uaminifu"
Sauti hiyo ilitoka kwa
kiumbe ambacho kilikuwa na muonekano wa malaika, Pastor Komanya
anaieleza GK na kusema kuwa sauti yake ilikuwa ya tofauti, na mavazi
yake yalikuwa ni meupe na kwamba alielezwa dhahiri kuwa hiyo semi
trailer ilikuwa imetumwa kummaliza, lakini ndio maana malaika walitumwa
kumlinda.
"Zawadi Gani" kama
ambavyo alikuwa akiitwa akiwa hospitali ya Muhimbili, alifanyiwa vipimo
na kuonekana ya kwamba hana shida yoyote. Na hili linadhihirika hata
pale alipotoka kwenye gari lililopiinduka, kwa kuwa alitoa vifaa vyake
na kuanza pia kupiga picha, picha ambazo kama mtu akiziona zote, hakika
hawezi kuamini kama kuna kusalimika hapo.
Mwisho wa yote Mchungaji
Komanya anakiri kuwa amepona kwa rehema ya Mungu, na baada ya hapo
amemuahidi kumtumikia kwa kazi aliyompa licha ya kwamba ni ngumu na ina
vikwazo vingi. Jumapili hii, Mchungaji Komanya ataimba wimbo mpya
kumshukuru Mungu kutokana na kumuepusha na kifo. Kwa wasafiri wote, hapa
kuna funzo la kujikabidhi mikononi mwa BWANA kila mara safari
inapotokea, katu tusienende kwa mazoea.PICHA ZOTE NA GOSPEL KITAA BLOG