STRAIKA wa Yanga, Reliants Lusajo ndiye mchezaji msomi kuliko wote ndani ya kikosi hicho lakini amekiri kwamba ana changamoto kubwa ya kupata namba ya kudumu.
Lusajo amemaliza masomo
yake ya Shahada (digrii) katika Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi kilichopo
mkoani Kilimanjaro alikokuwa akisoma Shahada ya Ugavi (Bachelor of Arts
in Procurement).
Mchezaji huyo amekosa
michezo 10 ya ligi msimu huu kwa kuwa alikuwa akimalizia ripoti yake ya
Utafiti (Research) kama sehemu ya masomo yake na mwezi ujao atatunukiwa
shahada yake ya kwanza kwenye mahafali ya chuo hicho.
Lusajo anakuwa mchezaji
raia wa Tanzania, mwenye elimu zaidi ya wachezaji wote wanaocheza Ligi
Kuu kwa sasa ingawa anazidiwa kidogo na kipa wa Toto Africa, Erick
Ngwegwe ambayo iko Ligi Daraja la Kwanza.
Uchunguzi wa Mwanaspoti
umebaini kwamba wachezaji wengi wa klabu za Ligi Kuu wameishia darasa la
saba, kidato cha pili, kidato cha nne na wachache wana elimu ya cheti.
“Nlifurahi kucheza kwa
mara ya kwanza Ligi Kuu baina ya Yanga na Mgambo JKT, ligi ni ngumu na
inahitaji mtu kufanya kazi kwa juhudi kubwa. “Yanga ina wachezaji wazuri
na wenye uzoefu mzuri, nafikiri kwa kwa sasa nimemaliza masomo yangu
hivyo nitahakikisha nafanya kazi yangu ya mpira kwa kujituma,” alisema
Lusajo. CHANZO MWANASPOTI