NYOTA katika utangazaji Bongo, Julius Nyaisangah aliyefariki dunia
Oktoba 20, mwaka huu katika Hospitali ya Mazimbu mjini hapa, amepitia
kipindi cha mateso cha takribani siku 1460 katika kupigania uhai wake.
“Kama alikuwa nayo kabla hatujui lakini tuligundua kuwa mume wangu mpenzi ana sukari mwaka 2009 na baadaye ikagundulika pia alikuwa na shinikizo la damu, tangu hapo amekuwa akiteseka sana,” alieleza mama huyo akijitahidi kuzuia machozi.
Marehemu Nyaisangah enzi za uhai wake.
Alisema, licha ya kuugua mumewe alikuwa hodari wa kufanya kazi na
kuendelea na majukumu yake muda wote katika Kampuni ya Abood Media
aliyokuwa akifanya kazi mpaka mauti yalipomkuta.“Kwakweli alijitahidi sana, alikuwa baba bora kwa familia yetu lakini Mungu amempenda zaidi. Namuombea makazi mema,” alisema.
MIEZI MITATU YA MATESO
Bi. Leah alisema, mumewe alikuwa akipatiwa matibabu katika hospitali mbalimbali mjini hapa na kuendelea na dawa lakini miezi mitatu iliyopita hali ilikuwa mbaya zaidi na alipumzika kwenda kazini kwa kipindi chote cha miezi mitatu.
“Lakini alipata nafuu na kurudi kazini, hadi wiki iliyopita alikuwa kazini kama kawaida ila sasa sukari ikapanda tena ghafla, halafu na presha nayo ikawa juu huku akiwa na malaria, ndipo akafariki,” alisema kwa uchungu.
RATIBA YABADILIKA
Awali, ratiba ilikuwa aangwe mjini hapa jana Jumanne kisha wasafari kwenda Tarime kwa maziko yaliyotarajiwa kufanyika leo Jumatano lakini ilibadilika baada ya serikali kuomba mwili wake upelekwe Dar kwa ajili ya kuagwa na viongozi wa serikali pamoja na jamaa zake wa Dar.
Ujumbe kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo ulioagizwa na Naibu Waziri, Amos Makalla ulifika nyumbani kwa marehemu na kueleza nia ya wizara ambapo ulikubaliwa baada ya kushauriana na bosi wa Nyaisangah, Aziz Abood, ambaye pia ni Mbunge wa Morogoro Mjini.
MAMIA WAMUAGA MORO
Baada ya makubaliano hayo ambayo yalipata baraka kutoka kwa kamati ya mazishi, ililazimika kubadilisha ratiba haraka ambapo mwili ulichukuliwa Hospitali ya Mkoa Morogoro kwa ajili ya kuagwa ili usafirishwe kwenda Dar.
Wakazi wa Morogoro na vitongoji vyake walijitokeza kwa wingi juzi Jumatatu nyumbani kwa marehemu Kihonda na kutoa heshima zao za mwisho kabla ya safari ya kwenda Dar ambako mwili ulifikishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili.
DAR VILIO TUPU
Jijini Dar es Salaam, jana Jumanne, umati wa watu ulifurika kumuaga marehemu Nyaisangah, kabla ya kusafirishwa kwa ndege kwenda Tarime kwa maziko yaliyotarajiwa kufanyika leo.
Nyaisanga ameacha mjane, Leah na watoto watatu ambao ni Samuel, Noela na Beatrice.