Like Us On Facebook

Gazeti la MWANANCHI lamaliza adhabu yake ya kutochapishwa kwa siku 14....Liko Sokoni kuanzia LEO



             Gazeti la MWANANCHI limeanza tena kuchapishwa baada ya kumaliza adhabu iliyopewa na Serikali ya kutochapishwa kwa wiki mbili kuanzia September 27, 2013 kutokana na mwenendo wa gazeti hilo pamoja na gazeti la MTANZANIA kuandika habari na makala za uchochezi na uhasama.
 
Kupitia mtandao wake MWANANCHI imeandika taarifa ya kutoka kifungoni, na jinsi  adhabu hiyo ilivyowapa hamasa kubwa .Ni adhabu  ambayo imewaathiri watu mbalimbali wakiwemo waandishi, vijana wanaosambaza na wengine, pia wameeleza msimamo wao baada ya adhabu hiyo. 

Isome kama ilivyoandikwa.
 
“Hatua ya kulifungia gazeti hili kwa sababu za kufikirika imesababisha maumivu kwa watu wengi. Vijana (vendors) waliokuwa wakiuza na kusambaza gazeti hili pamoja na familia zinazowategemea wameumia. Waandishi wa kujitegemea wanaolipwa kutokana na habari wanazotuma gazetini wameumia pamoja na familia zao.
 
Tumetoka kifungoni tukiwa na somo muhimu. Kwamba sheria kandamizi kama Sheria ya Magazeti ya mwaka 1976 haisimamii masilahi ya taifa, bali kundi la watu wachache.

Ni sheria kandamizi ambayo kwa umoja wetu tunaweza kuifuta. Tungependa kuwashukuru wasomaji wetu na wananchi kwa jumla kwa kuwa nasi katika kipindi kigumu tulichokuwa kifungoni. Vilevile, tunavishukuru kwa namna ya pekee vyombo vyote vya habari vya ndani na nje ambavyo vilisimama imara kupinga hatua ya Serikali kufungia magazeti.
 
Tutakuwa watu wasio na shukurani kama hatutatambua mshikamano mkubwa ulioonyeshwa na asasi za kiraia, mabalozi na watu mbalimbali kupinga matumizi ya sheria hii kandamizi. Hatujakata tamaa, bali tumetoka kifungoni tukiwa na hamasa kubwa kuendelea kuwapa habari wananchi pasipo woga wala upendeleo.
 
Hatupambani na Serikali, lakini tutaendelea kuikosoa pale inapofanya makosa na tutaipongeza pale inapotimiza wajibu wake. Tunawaomba wasomaji wetu mwendelee kutuunga mkono”.

SOURCE: MWANANCHI
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari