Huwezi
kuamini lakini huu ndio ukweli, kwamba watu kadhaa wamekuwa
wakimiminika kupata msaada wa tiba, ushauri wa kitabibu na wengine
masomo ya udaktari kwa mtu ambaye imethibitika kwamba hivi sasa ana
matatizo ya akili.
Huyu si mwingine bali ni Mark Paulo
Kishiwa ambaye kitaaluma ni daktari, aliyewahi kufanya kazi Hospitali za
Kasulu, mkoani Kigoma na Bugando mkoani Mwanza, lakini sasa mvua na jua
humwishia akiwa maeneo ya Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH).
Ukimwona mara kadhaa utamkuta akiimba
nyimbo zisizo rahisi kuzielewa kutokana na hali anayonekana kuwa nayo
ya matatizo ya akili, lakini anapokuwa sawa, hugeuka kuwa msaada kwa
wengi; madaktari wa MNH ambao huomba ushauri kwake, wanafunzi wa Chuo
Kikuu cha Sayansi za Tiba Muhimbili (MUHAS) na wagonjwa ambao hutaka
ushauri pia.
Dk Kishiwa anasema: “Naikumbuka
Aprili 26, 1981, ilikuwa Jumatatu ya Pasaka, ndipo nilianza kuugua.
Nilijikuta nikifanya vitu visivyo vya kawaida.
Nilimwaga maji ovyo ndani, nilimwaga
nguo na vitu mbalimbali, kila kitu kilikuwa ovyo. Baada ya muda
niligundua kufanya vitu siyo vya kawaida…Hivyo ndivyo nilivyoanza
kuchanganyikiwa na hali hii imenitokea mara kwa mara.”
Aliongeza: “Yaliponitokea hayo,
nilikuwa nikifanya kazi mkoani Kigoma katika hospitali iliyopo wilayani
Kasulu (hakuitaja jina) ndipo kilikuwa kituo changu cha kazi.”
Pamoja na Dk Kishiwa kuwa na matatizo
ya akili, imethibitika kuwa baadhi ya madaktari wa MNH wamekuwa
wakikimbilia kwake kupata ushauri, lakini kubwa ni lile la kufundisha
masomo ya ziada kwa baadhi ya wanafunzi MUHAS.
Pia amekuwa akifuatwa na watu
wanaomfahamu hasa wanawake wakimwomba ushauri hata kuwaandikia dawa
kutokana na maradhi waliyonayo. Mwandishi wa habari hii ni mmoja wa
waliopata ushauri wa kitabibu kutoka kwa Dk Kishiwa.
Tiba na ushauri
Uchunguzi wa wiki kadhaa katika eneo
la MNH, nyumbani kwake Chamazi na hata katika familia yake,
umethibitisha kwamba Dk Kishiwa licha ya kuwa mgonjwa wa akili bado ni
msaada mkubwa kwa watu wengi.
Gazeti hili lilishuhudia daktari huyo
akimwelekeza mmoja wa madaktari wa MNH namna ya kumsaidia mgonjwa wake.
Kwa mujibu wa mazungumzo yao, hali ya mgonjwa husika ilimchanganya
daktari huyo, hivyo kutaka kupata msaada kwa Dk Kishiwa.
Uchunguzi pia ulibaini kuwa wakati
fulani, Dk Kishiwa anakuwa katika hali ya kawaida na kuweza kutoa
ushauri, hata kutibu kwa kuwaandikia dawa wagonjwa akiwa eneo hilo la
Muhimbili.
Jioni moja gazeti hili lilishuhudia
wanawake wawili waliobeba watoto mgongoni wakiwa na Dk Kishiwa,
aliyekuwa akiwaandikia kitu kwenye karatasi. Baada ya tukio hilo
mwandishi aliwauliza iwapo wanamfahamu, na walijibu; “Tunamfahamu, ni
daktari alikuwa akituandikia dawa.”
Hata hivyo, uchunguzi ulibaini kuwa
mambo yanapobadilika, Dk Kishiwa huwa mkali asiyetaka kuwa karibu na mtu
au kuzungumza naye, huku akifanya vioja vinavyothibitisha hali yake ya
matatizo ya akili. Hali hiyo ilimlazimisha mwandishi kuendelea
kumfuatilia kwa siku kadhaa katika eneo hilo la MNH na kufanikiwa
kuzungumza naye.
Kwa mujibu wa watu wanaomfahamu hasa
madereva teksi wa eneo hilo, walisema Dk Kishiwa hushinda hapo na kwamba
pamoja na kuwepo kwa wafanyabiasha na madereva wengi, daktari huyo
humsikiliza dereva mmoja anayepatana naye na mara nyingi hutekeleza
anayomweleza.
Kwa msaada wa dereva huyo, Dk Kishiwa
anaeleza historia ya maisha yake kuwa alizaliwa Desemba 25, 1954,
alipata elimu katika Shule ya Msingi Tumbi mkoani Tabora hadi darasa la
nane na kuendelea na masomo kupitia shule kadhaa ikiwemo Sekondari ya
Busonga na Sekondari ya St Mary’s ya Tabora.kwamba katika elimu ya
sekondari alipata daraja A kwa masomo yote 11.
“Sikuwahi kufeli, nilipata daraja A
katika masomo yote 11 niliyosoma yakiwemo kemia, baolojia, hisabati na
civics. Baada ya hapo nilijiunga na jeshi kwa mujibu wa sheria kwa miezi
sita katika kambi ya Mafinga,” anasema Kishiwa bila kutaja miaka
aliyosoma.
Anakumbuka kuwa 1974 ndipo alijiunga
na Chuo cha Tiba Muhimbili, ambapo alisoma kwa miaka mitano na kumaliza
1979, bila kufeli somo hata moja na baada ya hapo alipangwa kwenda
Hospitali ya Bugando, Mwanza kikiwa ni kituo chake cha kazi cha kwanza.
Anasema alikaa Bugando kwa mwaka
mmoja tu na mwaka uliofuata akapelekwa Wilaya ya Kasulu, Kigoma kama
Mganga Mfawidhi na huko ndipo lilipoanzia tatizo alilonalo hadi sasa.
Kuugua akili
Anaeleza kuwa tangu Aprili 26, 1981
alipopatwa na tatizo la akili, amekuwa akipelekwa hospitali mara kadhaa
na tatizo hilo kutulia, lakini bado hali haikuwa nzuri ingawa bado
aliendelea kufanya kazi.
Anasema kuugua kwake kunahusishwa na imani za kishirikina, jambo ambalo si kweli na hajui nani aliyezusha.
Dk Kishiwa anasimulia kuwa baada hali
yake kuwa nzuri hakuendelea kukaa Kigoma bali alirudishwa Bugando,
Mwanza na anadai kwamba kati ya 1986 na 1994 alifanya kazi Muhimbili,
lakini alisimamishwa kwa sababu ambazo hadi leo hazifahamu.
“Nililipwa Sh3.4 milioni ambazo nilizitumia kununua shamba eneo la Chamazi na kujenga nyumba ninayoishi sasa,” anabainisha.
Anaendelea kueleza kuwa licha ya
kufanya kazi Muhimbili, pia aliwahi kufanya katika Hospitali ya Vikuruti
na Chamazi wilayani Ilala, Mkoa wa Dar es Salaam, ambapo alikuwa
akilipwa posho na Wizara ya Afya.
“Nilipokuwa nikifanya kazi Vikuruti,
nilitakiwa nipewe maharage na unga na vitu muhimu bure, lakini nilipewa
mara moja tu,”analalamika Kishiwa.
Kauli ya MHN
Hata hivyo, Ofisa Uhusiano wa
Hospitali ya Taifa ya Muhimbili, Aminiel Eligaesha, anasema Kishiwa
hakuwahi kufanya kazi katika hospitali hiyo licha ya kusikia kuwa
aliwahi kuwa daktari.
“Kwenye kumbukumbu za hapa Muhimbili
hakuna daktari kama huyo ingawa kuna habari kuwa aliwahi kuwa daktari na
kuna maprofesa ambao alisoma nao darasa moja. Niliwahi kusikia kuwa
anawafundisha masomo ya ziada wanafunzi wa MUHAS,”anasema Eligaesha.
Profesa Victor Mwafongo MNH
anathibitisha kwamba alisoma darasa moja na Dk Kishiwa, lakini hakuwahi
kufanya naye kazi hospitalini hapo.
Anasema kuwa alipotezana na Kishiwa
kwa muda na hakufuatilia alipo, lakini baadaye alipata taarifa kuwa ana
matatizo ya akili na kufikishwa MNH kwa ajili ya matibabu.
“Namafahamu Kishiwa na nimesoma naye
katika Chuo Kikuu cha Muhimbili, lakini sikuwahi kufanya naye kazi hapa
Muhimbili. Kwa sasa humwona mara nyingi akizunguka hapa MNH, hukutana na
kuzungumza naye kwa kuwa ananikumbuka vizuri na mimi
namkumbuka,”anasema Mwafongo.
Anafafanua kuwa anachofahamu kuhusu Kishiwa ni kwamba anapata tiba hospitalini hapo inayomsaidia hata kuwa kama alivyo sasa.
Mwananchi!!