MTU
mmoja aliyefahamika kwa jina la George Maswizilo (33) amekufa papo hapo
baada ya kuangukiwa na tawi la mti. Alikuwa akikata mti huo katika eneo
la Mabambasi Kata ya Ndembezi Manispaa ya Shinyanga. Ndugu wa marehemu
wamemsusia mwili mtu aliyempa kazi hiyo ili aendelee na maziko.Tukio hilo lilitokea jana saa mbili
asubuhi, ambapo marehemu alikuwa akikata mti katika nyumba ya Magreth
Mwandu, aliyempatia kibarua cha kazi hiyo. Baada ya kuukata, mti huo
ulimwamgukia na kumbana tumboni, hatua iliyosababisha apoteze maisha
akiwa juu ya mti.Mashuhuda wa tukio hilo, walisema
walisikia sauti ya mtu akiomba msaada na walipofika eneo la tukio,
walimkuta marehemu akiwa juu ya mti amebanwa na moja ya tawi la mti
aliokuwa anaukata. Wakati wakifanya juhudi za kumwokoa, tayari alikuwa
ameshapoteza maisha.Akieleza tukio hilo, Mwandu alisema
Maswizilo alifika nyumbani hapo siku moja kabla ya tukio ; na
wakaelewana malipo ya Sh 15,000 kwa ajili ya kazi hiyo ya kukata mti na
siku iliyofuata, wakati Maswizilo akiendelea na kazi, ndipo mauti
yakamfika.Shangazi wa marehemu aliyejulikana kwa
jina la Pili Maswizilo alisema Maswizilo alikuwa anajishughulisha na
kazi ndogo ndogo za vibarua kwa kujipatia riziki katika maeneo
mbalimbali.Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Mtaa wa
Mabambasi ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Ndembezi David Nkulila alisema
tukio hilo ni kama ajali zingine zinazoweza kumpata mtu yeyote na
haifai kulaumiana.“Baada ya kuona inataka kutokea
mtafaruku kuhusu tukio hilo, sisi viongozi wa mtaa tulichukua jukumu la
kumsaidia mama huyo ambaye ni mjane na hajiwezi, tukafanya mchango kwa
wakazi wa mtaa huu na tukafanikisha mpango huo kwa ajili ya mazishi ya
marehemu,” Nkulila aliongeza.Kamanda wa Polisi Mkoa wa Shinyanga,
Evarist Mangalla alithibitisha kutokea kwa tukio hilo. Alisema hakuna
mtu anayeshikiliwa na Jeshi la Polisi kuhusiana na tukio hilo.
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.