Watu 69 waliuawa na 107 kujeruhiwa wakati magaidi walipovamia juzi kwenye eneo la maduka jijini Nairobi.
Bado askari wa Kenya wakisaidiwa na maofisa wa Shirika la Upelelezi la Marekani (FBI) na wale wa Shirika la Ujasusi la Israel (Mossad) wanapambana na magaidi hao.
Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nchi za Nje, John Haule alisema jana kuwa Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk Batilda Buriani alikutana na maofisa wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya lakini hadi jana hakukuwa na taarifa zozote za Watanzania kuwepo kwenye tukio hilo.
“Tunaendelea kuwasiliana na ubalozi wetu Nairobi kujua hali ilivyo, lakini hadi sasa hatuna taarifa rasmi kuhusiana na raia wetu kuwepo kwenye tukio hilo. Nimezungumza na balozi wetu ameniambia bado anaendelea kukutana na wenzetu wa Mambo ya Nje wa Kenya,” alisema Haule.
Akihutubia taifa kwenye Ikulu ya Kenya jana, Rais Kenyatta alisema Serikali yake haitarudi nyuma katika kupambana na ugaidi mahali popote, huku akisema ugaidi si tatizo la Kenya pekee, bali la kimataifa na kwamba litamalizwa kwa nchi kushirikiana.
“Tunatakiwa kuwa kitu kimoja na mpaka sasa Idara ya Usalama inaendelea kuimarisha ulinzi eneo husika, magaidi waliopo katika jengo ni kati ya 10 hadi 15. Tutashinda vita hii ya ugaidi kwa umoja wetu na tuweke tofauti zetu pembeni,” alisema.
Awali, Waziri Mkuu wa zamani wa Kenya, Raila Odinga aliwataka Wakenya kutokuifananisha vita ya ugaidi na udini wala ukabila na kusisitiza kuwa matukio kama hayo yametokea hata katika nchi za Ulaya.
“Mataifa ya kigeni yasisitishe safari za kutoka ndani na nje ya Kenya, tusigawanyike kwa njia yoyote ile,” alisema Odinga.