HATIMAYE serikali imesalimu amri na kuamua kuwalipa mishahara ya miezi minne wafanyakazi wa Mamlaka ya Reli ya Tanzania na Zambia (TAZARA) waliogoma wakishinikiza kulipwa stahiki zao.
Uamuzi wa kuwalipa wafanyakazi hao ulitangazwa jana bungeni na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, alipokuwa akitoa kauli ya serikali kuhusu mgomo wa wafanyakazi hao ulioanza Agosti 23 mwaka huu.
Dk. Mwakyembe alisema serikali ilifanya mazungumzo na serikali ya Zambia ambayo imeshatuma dola milioni tano ambazo ni zaidi ya sh bilioni nane huku Tanzania ikitoa sh bilioni mbili kwa TAZARA.
Alisema fedha hizo zilizopatikana pamoja na dola milioni 3.17 ambazo TAZARA inazidai kutoka kwa wateja wake mbalimbali zinatosha kurejesha hali ya kawaida katika mamlaka hiyo.
“Tayari wafanyakazi wameshalipwa mshahara wa Mei mwaka huu, ifikapo Septemba 9, watakuwa wameshalipwa mishaahara yao ya Juni, Julai na Agosti,” alisema.
Mwakyembe alisema serikali inatarajia wafanyakazi wote wa TAZARA watakuwa wamerejea kazini siku hiyo.
Alibainisha hasara zilizopatikana katika kipindi hicho cha mgomo kuwa ni dola milioni 1.4 (zaidi ya sh. bilioni mbili).
Dk. Mwakyembe pia alisema serikali za Tanzania na Zambia zimebaini kuwa licha ya mizigo inayosafirishwa na TAZARA kuongezeka bado mapato ni madogo kulinganisha na matumizi.
Alisema katika kipindi cha miezi sita iliyopita mapato ya TAZARA yalikuwa wastani wa dola milioni 1.53 kwa mwezi huku matumizi yao ni dola milioni 2.5 kwa mwezi.
Aliongeza kuwa mishahara na mafuta vinachukua wastani wa dola milioni 1.9 kwa mwezi na sehemu iliyobaki ni matumizi mengine ya uendeshaji.
Mwakyembe alisema pamoja na mgomo huo kutofuata sheria wala kuwepo mazungumzo yoyote kati ya uongozi wa TAZARA na wenzao wa chama cha wafanyakazi wa reli Tanzania, serikali imeagiza zisichukuliwe hatua zozote
-Tanzania daima