Like Us On Facebook

MAMA SALMA KIKWETE ATOA WOSIA MZITO KWA WANAFUNZI WA KIKE...


           MKE wa Rais Mama Salma Kikwete amewataka wanafunzi wa kike kujiepusha na 'mafataki' wanaotaka kuwarubuni kwa vitu mbalimbali ili kujikinga na hatari ya kupata ujauzito na ugonjwa wa Ukimwi na kusababisha kutofikia malengo katika maisha yao.
Pia amewataka wanafunzi wa kiume kuachana na tabia ya kuvaa suruali milegezo na uvutaji wa sigara ambao utawasababishia kupata ugonjwa wa saratani ya koo na mapafu.
Mama Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) alisema hayo hivi karibuni wakati akizungumza na wanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Msimbu iliyopo Kata ya Msimbu Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.
“Kama wazazi wenu hawawasimamii kufuatilia mienendo yenu mjisimamie nyinyi wenyewe kwa kukanyana na kutoa taarifa kwa walimu wenu pale ambapo mtaona mwenzenu ana tabia ambazo ni kinyume na maadili ya mwanafunzi kwa kufanya hivyo mtaepukana na tatizo la mimba za utotoni’, alisema Mama Kikwete.
Kuhusu madai ya wanafunzi hao kuwa wazazi wao wanakabiliwa na tatizo la umasikini jambo ambalo linawafanya waweze kuingia katika vishawishi mbalimbali Mama Kikwete alisema umasikini isiwe ni kigezo cha mtu kufanya mambo yasiyofaa ili aweze kupata fedha wakati ni hatari katika maisha yake.
“Ni muhimu wazazi wakatafuta mbinu mbadala ya kuweza kukabiliana na hali hii ikiwa ni pamoja na kufanya kazi kwani mtu akifanya kazi kwa bidii ni lazima atafanikiwa na kuweza kupambana na hali ya umasikini kwani atalima mazao na kuuza, atafanya biashara ndogondogo na kuweza kujipatia kipato”, alisema Mama Kikwete.
Aidha Mama Kikwete pia aliwataka wanafunzi hao kuitumia teknolojia vizuri katika kujiletea maendeleo ikiwa ni pamoja na kujitafutia nyaraka za kusoma kwa ajili ya masomo yao.
Akisoma taarifa ya shule hiyo, Mwalimu Mkuu Renatus Rweyemamu alisema tangu shule hiyo ilipoanzishwa mwaka 2007 hadi sasa idadi ya wasichana waliopata ujauzito ni 34 na wahusika wameshafikishwa kwenye vyombo vya dola na hivi sasa suala hilo linasimamiwa na watendaji wa vijiji husika.
Alitaja changamoto zinazoikabili shule hiyo kuwa ni wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata shule jambo ambalo linasababisha kuingia darasani wakiwa wamechoka.
Alisema pia wasichana wanakutana na vishawishi vingi wakiwa njiani kutokana na hosteli moja haitoshi kwa kuwa ina uwezo wa kuchukua wanafunzi 48 pia haina vitanda wala magodoro ya kulalia.
Mwalimu Rweyemamu alisema, “Changamoto nyingine ni wazazi kutofuatilia kwa ukaribu mienendo ya watoto wao pia kutokutoa ushirikiano wakati wa kuwafuatilia wahusika waliowapatia ujauzito watoto wao”.
Aliitaja mikakati waliyojiwekea kuwa ni kufanya mikutano na wazazi ili kuwapa ushauri jinsi gani wanaweza kufuatilia mienendo ya watoto wao na kutafuta wafadhili watakaowasaidia kujenga hosteli ikiwa ni pamoja na kununua vitanda, magodoro na kuweka umeme jua.
“Pamoja na majukumu mengi yanayokukabili ombi letu kubwa kwako kwa sasa ni tunaomba kama itawezekana utununulie vitanda na magodoro kwa hosteli yetu”, alisema Rweyemamu.
Shule ya Sekondari ya Msimbu ni shule ya kata ambayo ina jumla ya wanafunzi 463 wasichana wakiwa ni 250 na wavulana 213 ambao wanatoka katika vijiji sita vilivyopo katika Kata ya Msimbu.
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari