Like Us On Facebook

MADHEHEBU YA DINI SASA KUCHUNGUZWA KUTOKANA NA KUJIHUSISHA NA BIASHARA YA MADAWA YA KULEVYA

SERIKALI imesema itaanza kuchunguza madhehebu ya dini kutokana na migogoro na malalamiko ya waamini dhidi ya viongozi wao kuongezeka.
Viongozi hao ni hasa wa kigeni kutokana na vitendo vyao vya kitapeli wanavyodaiwa kuvifanya, vikiashiria kujihusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya kwa kivuli cha dini.
0 By Mwandishi WetuImesomwa mara: 355
Aidha, baadhi ya viongozi wanaolalamikiwa ni wachungaji na wanadaiwa baadhi yao kumiliki ardhi (mashamba) na migodi ya mamilioni ya fedha nchini kinyume cha sheria na wamejiandikisha katika mchakato wa kupata vitambulisho vya Taifa kama raia wa Tanzania.
Waziri wa Mambo ya Ndani, Dk Emmanuel Nchimbi
Ingawa malalamiko yapo mengi serikalini, lakini ya hivi karibuni (barua na nyaraka za malalamiko tunazo) ni ya waamini wa Kanisa la The Bible Believers Church (BBC Mission) la Pugu Kajiungeni linalomhusisha pia Mchungaji wa Kanisa la Cornerstone la Tabata, yote ya Dar es Salaam.
Wanadai pia kuwa baadhi ya wachungaji walianza kuhubiri usiku wa manane katika mitaa ya Dar es Salaam wakidai wameagizwa na Mungu kuiteka Dar es Salaam na muda mzuri ni usiku, jambo linalowapa wasiwasi wafuasi wao zaidi wa aina ya Injili wanayohubiri.
Wanadai wachungaji wao (majina tunayo), raia wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) wamekuwa sababu ya migogoro ya kifedha na mali za Kanisa isiyokwisha kwa kile walichodai wameshindwa kutoa taarifa za fedha kwa waamini pale walipotakiwa kufanya hivyo.
Aidha, waamini hao kwa barua zao walizoandika kwa nyakati tofauti kwenda Wizara ya Mambo ya Ndani (nakala tunazo), wanadai na kulalamika kuwa wachungaji hao wamejiandikisha kupata vitambulisho vya Taifa kama raia wa Tanzania waliozaliwa Kigoma na Mbeya, wakati wakijua wazi kuwa si raia.
Walidai kuwa hofu kubwa ya hatima ya usalama na makanisa yao imetanda kwao na wanaiomba Serikali ichunguze wachungaji hao haraka iwezekanavyo, kuwa huenda wanatumia kivuli cha Kanisa kufanya utapeli nchini, kwa kile walichodai wanahubiri usiku wa manane katika mitaa ya Dar es Salaam.
“Tunaiomba Serikali iwachunguze watu hawa haraka, wana vibali vya kimisionari vya kufanya kazi nchini kwa muda, lakini tunashangaa kwamba wamejiandikisha kupata vitambulisho vya Taifa kama raia, hatujui nia yao hawa watu, sasa hivi wanajimilikisha ardhi kutumia watoto wao, hali si shwari kabisa,” alisema muamini mmoja ambaye hakuwa tayari kutaja jina lake gazetini.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili baada ya malalamiko ya waamini hao wiki chache zilizopita umebaini kuwa, wapo wachungaji katika makanisa kadhaa jijini humo, wameanzisha mtindo wa kuhubiri usiku wa manane katika mitaa ya Jiji la Dar es Salaam na kufanya vikao katika majumba ya starehe (baa) na katika kuhubiri huko, hutumia magari wanayoyabadili rangi mara kwa mara.
Hali hiyo ya mashaka inahusishwa pia na matukio ya kihalifu yanayokithiri nchini, ambayo baadhi yanahusisha mpaka viongozi wa kidini ikiwamo biashara haramu ya kuuza dawa za kulevya, ukahaba na ujambazi.
Kwa mujibu wa nyaraka tulizonazo, Mchungaji wa Kanisa la BBC Mission lenye namba za usajili SA 7446 anayelalamikiwa inaonesha kuwa Kanisa hilo humkatia vibali vya kufanya kazi vya muda mfupi wa miaka miwili, kwa mujibu wa taratibu za Uhamiaji lakini amejiandikisha kama raia mzaliwa wa nchini.
Askofu wa Kanisa hilo la BBC Mission, Frank Mwangende alipoulizwa kuhusu jambo hili, alikiri kuwepo kwa mgogoro katika Kanisa lao tawi la Pugu-Kajiungeni na kueleza kwa ufupi kuwa, uongozi wa Kanisa unalifanyia kazi.
Pia, Askofu Mwangende alikiri waamini wake kuandika barua ya malalamiko serikalini wakitaka Serikali iingilie kati suala hilo, lakini alisema wao Kanisa, wanayafanyia kazi malalamiko hayo kwa kuzungumza na pande zote mbili husika.
Wachungaji wanaolalamikiwa walitafutwa na gazeti hili kwa zaidi ya wiki tatu sasa, bila kupatikana na baadhi yao walituma wasaidizi wao kuzungumza na gazeti hili na kudai kuwa malalamiko hayo yana lengo la kuwachafulia huduma yao nchini na kwamba hakuna ardhi yoyote wala mgodi wanaomiliki kinyume cha sheria.
Lakini nyaraka tulizonazo zinaonesha kuwa, wachungaji hao wanamiliki mashamba Morogoro na wamejiingiza katika biashara ya kuchimba madini mkoani humo, kwa zaidi ya miaka miwili sasa, na kwa kuwa wameoa Watanzania, wamerithisha watoto wao ardhi baadhi zikiwa mali ya makanisa.
Aidha, wanalalamikiwa kuwa wanatumia mgongo wa uchungaji kutapeli baadhi ya waumini wanaowafanyia kazi majumbani bila kuwalipa, huku waumini wenye fedha wakiwapa uongozi wa juu ndani ya Kanisa fedha na mali zao.
Namba za simu zilizoachwa kwa gazeti hili ili kupata wachungaji hao haziwezi kupatikana kwa takribani wiki tatu sasa na eneo la Kanisa wachungaji hao hawapo kwa kipindi sasa wakidaiwa wapo nje ya mkoa kwa kazi ya utumishi.
Mkurugenzi wa Sheria wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Justus Mulokozi akizungumza kwa niaba ya Wizara, alikiri kupokea malalamiko ya waamini wa makanisa hayo mawili na mengine mengi, wakiwalalamikia wachungaji wao wa ndani na nje ya nchi kuhusu masuala ya fedha na mali za makanisa.
“Ni kweli, tumepokea malalamiko ya waamini wa makanisa hayo, lakini niseme si hayo tu, yapo makanisa mengi wachungaji wanalalamikiwa, Serikali tumeona ipo haja kuchunguza makanisa na madhehebu ya dini zote yanayofanya kazi hapa, upo uhuru wa kuabudu lakini, kuna mambo yanatupa wasiwasi juu ya mwenendo wa wanaotoa huduma hizo za kiroho,” alisema Mulokozi.
Alisema tayari Wizara imepeleka nyaraka hizo katika Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (NIDA) na Idara ya Uhamiaji kwa ajili ya uchunguzi zaidi kutokana na malalamiko ya waumini kudai wachungaji hao wamejiandikisha kama raia wakati ni wageni na alisema ikibainika, sheria itachukua mkondo wake.
Msemaji wa Idara ya Uhamiaji nchini, Abbas Irovya aliliambia gazeti hili kuwa idara yake inashirikiana na Wizara kushughulikia suala hilo na kwamba, wameiandikia Wizara kuomba nyaraka muhimu, ili kufuatilia uraia wa wachungaji hao walioatajwa na waamini wao.
-HABARI LEO
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari