MTANGAZAJI aliyewahi kufanya kazi Runinga ya Channel Ten ambaye kwa sasa ni Mkurugenzi Mtendaji wa Gazeti la ‘Africa Leo,’ Cyprian Musiba amemshukuru Rais Jakaya Kikwete kwa kumtolea mahari kisha kufunga ndoa na mkewe Deborah John.
Ndoa ya mtangazaji huyo iliyohudhuriwa na mastaa, wafanyabiashara pamoja na viongozi wa serikali, ilifanyika Septemba 1, mwaka huu jijini Dar.
Akizungumza na paparazi wa Ijumaa aliyehudhuria harusi hiyo, Musiba alisema anamshukuru Rais Kikwete aliyemtolea mahari inayozidi shilingi milioni 3.
Aliongeza kuwa, anamshukuru pia Mama Salma Kikwete pamoja na kijana wake Ridhiwani kwa mchango wa hali na mali walioutoa kufanikisha harusi yake.
“Nashindwa namna ya kumshukuru JK, mke wake na Ridhiwani aliyekuwa mhusika mkuu wa kamati ya maandalizi ya ndoa yangu kwa kila kitu walichonifanyia, hakika Mungu atawalipa,” alisema Musiba.
Musiba aliongeza kuwa, pamoja na mchango wa fedha za mahari alizotoa, JK alimpatia ukumbi wa bure aliofanyia sherehe yake.
Mtangazaji huyo alisema ukiacha ‘kampani’ nzuri aliyopewa na familia ya Rais Kikwete, anawashukuru watu wote waliochangia kufanikisha harusi yake kwa njia moja ama nyingine.
Harusi ya Musiba na mkewe ambayo iliteketeza mamilioni ya shilingi, ilifanyika katika Ukumbi wa Karimjee jijini Dar baada ya ndoa kufungwa kwenye Kanisa la SDA (Wasabato) la Sinza jijini Dar.
-GPL