Like Us On Facebook

JENEZA LA MTOTO MCHANGA LAKUTWA MLANGONI MWA JENGO LA MFANYABIASHARA

JENEZA lenye mwili wa mtoto mchanga, limezua taharuki kwa wananchi na wakazi wa Mtaa wa Ihago, Kata ya Mahina, Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza.
 Tukio hilo la  kushangaza na la aina yake, lilitokea Agosti 29, mwaka huu, majira ya saa 12:00 asubuhi baada ya kugunduliwa na mfanyabiashara Ester Musa (28) likiwa limetelekezwa kwenye mlango wa mgahawa wake.
 Jeneza hilo linaaminika kufukuliwa na watu wasiofahamika kwenye moja ya makaburi eneo la Mahina jijini hapa.
 Akizungumza na paparazi wetu kuhusiana na tukio hilo, Ester anayemiliki na kuendesha mgahawa alisema, alifika katika eneo lake hilo la biashara, ghafla akapigwa na mshangao baada ya kuona jeneza likiwa mbele ya mlango wa mgahawa wake.
  “Nashindwa kujua nini maana ya tukio hili sababu hivi karibuni nilikuta barua imebandikwa ukutani ikinitaka nihame kutoka eneo hili, vinginevyo nitaona nitakachofanyiwa. Leo nimekuta jeneza mlangoni,” alisema Ester na kuongeza;
 “Tukio hili nalihusisha na imani za kishirikina lakini kubwa linachangiwa na wivu wa kibiashara.Tangu nizaliwe sijawahi kuona jambo kama hili. Hapa sijawahi kugombana na mtu yeyote nashangaa kufanyiwa kitendo cha namna hii katika eneo la biashara yangu.”
 Mwenyekiti wa mtaa huo, Anthony Deus alisema kitendo cha kufukua mwili wa marehemu tena mtoto mchanga, si cha kibinadamu na ni tukio la kusikitisha katika jamii, hivyo watakaobainika watachukuliwa hatua za kisheria.
 Kaimu Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mwanza, ACP Christopher Fuime, alikiri kuwapo kwa  tukio hilo na kusema hakuna mtu aliyekamatwa akihusishwa nalo.
 “Tunaendelea na uchunguzi lakini hadi sasa hakuna aliyekamatwa akihusishwa na tukio hili la kusikitisha… wananchi wameuzika upya mwili wa mtoto huyo,” alisema.
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari