DUNIA inakwenda na kugeuka. Yakikufika, unaweza kudhani wewe ni mja mwenye bahati mbaya kuliko wengine wote. Tafadhali usiwaze hivyo, Mungu mwenye upendo, asiye na sifa ya ubaguzi, ni mkarimu kwa kila mtu.
Gilbert Kisinde (39), akiwa kitandani.
Ila inauma sana, jaribu kufikiria kwamba mtu ni kijana mwenye nguvu zake. Mkamilifu wa viungo na akili. Ghafla anapata janga ambalo linabadili maisha yake kutoka wa kuwa mtokaji kwenda kutafuta riziki, sasa mlalaji tu. Maisha yake yote ni kitandani.
Gilbert Kisinde, 39, mkazi wa Mbezi Jogoo, Wilaya ya Kinondoni, Dar es Salaam, kwa sasa ni wa kitandani tu. Alipata ajali mbaya akiwa kazini na tangu siku hiyo amepooza kuanzia kiunoni kushuka chini.
Kinachomuumiza Gilbert moyoni ni kwamba aliumia akiwa kazini lakini kwa sasa yupo kivyake bila msaada wowote.
Gilbert wa leo, hawezi kujifanyia chochote.
Kukaa mpaka ashikiliwe, kusimama ndiyo hawezi kabisa achilia mbali kutembea. Kwa vile hana anachojiweza, muda wote anafungwa nepi (pampers) lakini pesa ya kuzinunua nayo ni majanga.
“Siyo kwamba kampuni yangu haikunisaidia kabisa, bali nilipopata ajali, ilinipeleka hospitali, baada ya kupita miezi sita ikajiweka pembeni,” anasema Gilbert mbele ya mwandishi wetu na kuongeza:
“Hiyo miezi sita iliisha nikiwa bado hospitali ya Muhimbili natibiwa. Kiukweli maisha yangu yamebadilika sana. Dunia imenigeukia sana ila namtegemea Mungu, hakuna linaloshindikana kwake.”
CHANZO CHA MATESO YAKE
“Nilikuwa mfanyakazi wa Kampuni ya Konoike. Niliumia wakati wa ujenzi wa Barabara ya New Bagamoyo. Imeshapita mwaka mmoja na miezi mitatu nikiwa kitandani. Asikwambie mtu ndugu yangu, maisha ya kitandani yanatesa sana,” anasema Gilbert.
“Siku ya tukio niliamka salama nikiwa na afya yangu timamu, nikaelekea kazini. Tukiwa eneo la Tanki Bovu (Mbezi Beach), mimi nilikuwa nimepanda kwenye gari la kumwaga maji kuondoa vumbi barabarani.
“Nilikuwa nimepanda kwa nyuma. Nilishika bomba kwa mkono mmoja, mwingine nikawa namwelekeza dereva ambaye alikuwa anafuata maelekezo yangu kwa sababu alikuwa ananiona kupitia ‘saitimira’ (side mirror).
“Kwa vile alikuwa ananiangalia kupitia saitimira, alipoteza umakini wa kutazama mbele. Kumbe mbele kulikuwa na shimo, gari liliingia kwenye lile shimo, kwa hiyo nikarushwa na kuanguka.
“Ilikuwa ngumu kujizuia nisianguke kwa sababu nilikuwa nimeshika bomba kwa mkono mmoja. Nikiwa nimeanguka, dereva alianza kutafuta naamna ya kulitoa lile gari kwenye shimo. Ikabidi arudi nyuma, kwa hiyo akanigonga na kuniburuza.
“Dereva hakujua kama nimeanguka, akawa anaendelea kuniburuza, hivyo kunisababishia maumivu makali sana. Dereva alipokuja kushtuka, tayari nilikuwa nimeshaumia sana.”
MAISHA YA MOI MIEZI SITA
Gilbert alisema, baada ya dereva kugundua kuwa alikuwa anamgonga, alisimamisha gari na bila kuchelewa alikimbizwa Hospitali ya Taifa, Muhimbili.
“Pale Muhimbili nilipelekwa Kitengo cha Mifupa na Mishipa ya Fahamu (Moi) ambako baada ya siku tatu nilifanyiwa upasuaji kisha nikaendelea kukaa wodini kwa takriban miezi sita, ndipo niliporuhusiwa kurejea nyumbani,” alisema Gilbert.
Akaongeza: “Sikukaa nyumbani kwangu, mdogo wangu alikuja kunichukua nikakae kwake kwa sababu sijiwezi, ningepata shida katika nyumba za kupanga. Nilimwacha mke wangu, mimi nikaja kuishi hapa kwa mdogo wangu ili nipate huduma zaidi kwa nafasi.”
KILIO KWA WANAYE
Gilbert anasema kuwa ana watoto wawili ambao wanaishi kijijini kwao, Kilombero, Morogoro.
“Kule wapo kwa baba yangu ambaye amekuja huku kuniuguza. Kwa hiyo sasa hivi watoto wangu bado wadogo lakini wanaishi kijijini peke yao. Mimi baba yao sina mbele wala nyuma, nategemea kuhudumiwa tu. Inaniuma sana.”
ANATAKIWA KWENDA INDIA, HANA UWEZO
Gilbert anasema kuwa hivi sasa anatumia pampers ambazo humgharimu shilingi 25,000 kwa wiki, vilevile anatakiwa kupata mipira ya kukojolea, vitu ambavyo ni ngumu kuvipata kwa sababu uwezo wa ndugu zake ni mdogo.
“Miguu yangu imekakamaa kabisa, nashauriwa angalau niwe nakwenda Muhimbili kufanya mazoezi, nashindwa kwenda kwa sababu natakiwa angalau niwe na pesa ya kukodi taksi kila siku.
“Hii inasababisha miguu yangu izidi kukakamaa, imepooza kabisa. Madaktari wanasema ili nirejee katika hali yangu ya kawaida labda niende India. Huko nitaendaje ikiwa pesa tu ya kukodi taksi kwenda Muhimbili kwenye mazoezi nashindwa? Inaniuma sana,” anasema Gilbert.
WEWE UNAWEZA KUWA NAFUU YA GILBERT
Msemo kwamba hujafa hujaumbika unagusa moja kwa moja maisha ya Gilbert kwa sasa, maana alikuwa kijana mwenye nguvu zake lakini sasa kila kitu kimebadilika. Wewe unaweza kumfaya apate nafuu au kupona kabisa kama utaamua kumchangia.
Gilbert anahitaji fedha za kumuwezesha kununua pampers na mipira ya kukojolea kila wiki, anahitaji kupata pesa za kukodi taksi kila siku akafanye mazoezi Muhimbili lakini zaidi anatafuta msaada wa mtu kumpeleka India kwa matibabu yatakayomfanya apone kabisa. Kama umeguswa, tumia namba 0754 021 301 kufikisha mchango wako na kwa hakika Mungu atakubariki.