Like Us On Facebook

DONDOSHA MKONO WA SWETA MAKETE

kuta2 e8cca

        Ni dhana potovu zimejengwa kwenye baadhi ya makabila zikizuia watu kutahiriwa Ijapokuwa tohara kwa wanaume wilayani Makete ni huduma ya bure, lakini asilimia ukubwa ya wanaume wanaonekana ni wagumu kukubali kutahiriwa, huku wakikumbatia mila na desturi potofu.Hata hivyo, inaaminika kuwa kuwepo kwa kiwango cha juu cha maambukizi ya virusi vinavyosababisha Ukimwi (VVU) na hata Ukimwi wilayani humo kunachangiwa kwa kiasi kikubwa na kiwango cha chini cha tohara kwa wanaume.
Eliud Sanga, kijana mwenye umri wa miaka 28 anaeleza namna alivyochukua uamuzi mgumu wa kwenda kutahiriwa wakati kampeni za tohara zilipofika katika kijiji chake, Ivilikinge mwaka 2012.
Anasema haikuwa kazi rahisi kwa baba yake, wajomba zake ambao walikuwa wakali mno wasiotaka kusikia kuhusu uamuzi wake huo wa kijasiri.
"Nilifanya uamuzi mgumu ambao naweza kusema ulinigharimu kwa wiki mbili nilizokuwa najiuguza, hakuna aliyenisogelea kwa madai kuwa nimepotoka kwa kuacha mila na desturi.
"Hata hivyo, kwa kuwa nilipewa elimu ya kutosha niliona ni hali ya kawaida na ingenisaidia mwenyewe katika kujikinga na VVU," anasema Eliud aliyepima virusi vya Ukimwi na kujikuta hajaathirika.
Anasema wazazi wake walimweleza kuwa katika ukoo wao na mababu wa nyuma hakuna aliyewahi kutahiriwa hivyo hapaswi kufanya hivyo.
"Niliuliza sababu za kukataliwa na je kama ningepata madhara yoyote hakukuwa na jibu la mapema, niliona ni heri nidondoshe mkono sweta, baada ya kufanya hivyo nilipokea vitisho kwani kidonda kilinichukua wiki kama tatu hivi kupona.
"Nashukuru kwani baada ya kupona niliwashauri wadogo zangu, mmoja tayari hawa wengine wawili bado wanaendelea kuamini mila za zamani," anaeleza Sanga.
Menmen Mahenge, mzee wa miaka 74 kutoka Kijiji cha Ivalalila anasema: "Nimezaa watoto wengi ingawaje baadhi yao wameshafariki, lakini walio hai bado hawajafanyiwa tohara na kama walitahiriwa basi ni ukubwani na wamenificha.
"Sitaki mtoto wangu yeyote afanyiwe tohara. Watoto wangu sita walio hai hawajathubutu hata kuniambia kwa kuwa wanajua nitakataa."Mzee Mahenge anafafanua kuwa wajukuu zake kadhaa amesikia kuwa wametahiriwa wakiwa shuleni kufuatia kampeni ya dondosha mkono sweta, ila hajali na wala hawezi kuwazuia.
Baada ya kupewa elimu kidogo kuhusu faida za tohara kwa wanaume, Mzee Mahenge anasema "Nilisikia hayo katika mkutano wa kijiji na wahamasishaji wa kampeni hiyo, lakini si kwamba ukitahiriwa asilimia ya kupata Ukimwi inapungua, mbona mimi nimeishi miaka hii yote mimi na mke wangu wazima?
"Mbona hatuna Ukimwi na wazee kama mimi kijijini hapa hawapo na vijana wametafunwa na ugonjwa huu? Mimi nadhani umalaya ndio unasababisha haya yote," anasema Mzee Mahenge.
Anasema kuwa licha ya wadogo na kaka wake kufariki kabla yake hajawahi kurithi shemeji zake.
"Mimi najilinda sijawahi kurithi mjane na sitarajii na sasa nimeshakuwa mzee, ila siwezi kumpa kibali mtoto wangu wala mjukuu wangu labda wafanye wenyewe bila kuniambia."
Efedi Eskaka Chaula anasema yeye mpaka sasa hajatahiriwa na hana mpango huo kwani anahisi anaweza kuishi pasipo tohara.
"Sifikirii kufanya tohara na bado sijaona umuhimu wake japo kuna kitu kimoja kinaweza kunisukuma hapo baadaye hasa suala la usafi ndilo ninaloona linaweza kunipa msukumo wa kufanya hivyo," anasema.
Anaeleza, "Mke wangu anajua kwamba mimi bado sijadondosha mkono sweta, si mimi tu hapa kijijini huo ni mjadala mpana tu, watu wanahoji umuhimu wake, lakini pia madhara yake."
Chaula anaongeza:
"Nimekaa Mbozi (Mbeya), lakini huko kulikuwa na tohara kwa watoto wadogo pekee wanaume hatukupata nafasi, nilihisi aibu hata kuuliza kwa wenzangu maana wangenicheka. Wakati huo tohara ilikuwa Sh 5,000."
"Kwangu mimi si woga pekee, ila wapo wanaokawia kupona unajua kuna maeneo ya mwili yakiguswa ni ngumu kuhimili maumivu mfano jicho, sikio au huku kwa wanaume ni shida, mifano niliyoiona sitamani kuifuatana hata hivyo japo wanapona, lakini kwa mila zetu wanaume kutahiriwa ni kama dhambi vile," anaeleza.
Anaweka wazi kwamba japokuwa hapendi kufanyiwa tohara, lakini anakutana na magumu hasa upande wa usafi.
"Sijawahi kupata magonjwa ya zinaa, lakini pia ninaona kero kwani hakuna usafi hapa ni shida ila wanaume wengi wanasumbuliwa na magonjwa ya zinaa ikiwemo kaswende na kisonono," anasema.Hii ni tofauti na Deo Rafael ambaye amefanyiwa tohara mwaka 2012 ambaye anasema: "Nimefanyiwa tohara mwaka 2012 niliamua kwenda katika kituo cha afya Makete, huko nilikutana na washauri ambao walinielekeza namna ya kufanya ni jinsi gani ningejitunza mpaka kupona kwangu."
Rafael anasema kampeni kijijini hapo zimepita kwa wingi tu, lakini watu wazima ni wabishi hivyo serikali inatekeleza mpango huo kwa watoto wa shule ya msingi ambao bado hawajakua.
"Nadhani ni vyema serikali ikatilia mkazo suala la tohara kwa hawa vijana wadogo ambao bado wanakaa kwenye makundi hii itasaidia kwa wao kuwa na mwamko, ikiwa kijana hatofanyiwa atachekwa na wenzake mwisho wa siku ataamua tu kufanyiwa," anasena Deo Rafael.
Mratibu wa Ukimwi Wilayani Makete, Dk Shadrack Sanga anasema licha ya kwamba tohara imekuwa ni bure bado wananchi hawajitokezi kwa wingi hata hivyo kumekuwa na taarifa zilizozagaa kwamba mwanaume akishafanyiwa tohara hawezi kupata virusi vya Ukimwi tofauti na yule ambaye hajatahiriwa.
"Naomba hili lieleweke wazi, mwanaume ambaye hajafanyiwa tohara na yule aliyefanyiwa wote wanaweza kupata vvu, lakini aliyefanyiwa tohara ana upungufu wa asilimia 60 kupata vvu lakini si kwamba hatapata" alisema.
Katika hatua nyingine Dk Sanga anasema tangu kampeni ya tohara ya wanaume maarufu kama 'dondosha mkono sweta' ianze rasmi wilayani Makete mwaka 2011, jumla ya wanaume 9,669 wamefanyiwa tohara.
Anasema mwitikio ni mzuri lakini bado idadi ya wanaume ambao hawajafanyiwa tohara ni kubwa hivyo anatoa wito kwa wanaume kuacha woga na aibu ya kwenda kufanyiwa tohara ambayo inatolewa bure.
"Hivi sasa Mkoa wa Njombe unaongoza kitaifa kwa kuwa na maambukizi makubwa ya virusi vya Ukimwi, ambapo imegundulika kuwa wanaume wengi wa mkoa huo kutofanyiwa tohara ni miongoni mwa sababu kubwa zinazosababisha maambukizi hayo kuwa juu.
Ofisa Ustawi wa jamii wilayani humo, Leoncek Panga anasema vijiji mbalimbali vimeshatembelewa kwa ajili ya kupewa mafunzo mbalimbali kuhusu tohara na umuhimu wake lakini bado mwamko ni mdogo.
"Tumefundisha na tumepita katika vijiji vingi tukifundisha suala hilo na faida zitokanazo na tohara kwa wanaume lakini mpaka sasa idadi ya wanaume waliofanyiwa tohara ni ndogo ukilinganisha na idadi ya wanaume waliomo katika wilaya hii.
Anasema mwamko bado ni mdogo hasa kwa wanaume walio vijijini "Kitakwimu wanaume wa hapa wilayani wamejitokeza kwa wingi zaidi tofauti na vijijini ambako bado kuna mwamko mdogo mno:
chanzo mwananchi.
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari