Like Us On Facebook

SITAKI : SUAREZ AGOMA KUOMBA RADHI LIVERPOOL

NI kifo cha penzi. Uhusiano mzuri na wa kusisimua baina ya Liverpool na mshambuliaji wake mahiri, Luis Suarez, sasa  unatazamiwa kufa rasmi wiki hii baada ya kubainika kwamba staa huyo wa Uruguay amegoma kuomba radhi kama kocha Brendan Rodgers anavyotaka.

 
Watu wa karibu wa Suarez wamesema kwamba kwa sasa uhusiano wake na Rodgers umekata roho kufuatia mshambuliaji huyo kutengwa na wenzake katika uwanja wa mazoezi wa Liverpool, Melwood.
Kocha Rodgers alikaririwa siku chache zilizopita akisema kwamba Suarez hatarudi tena katika mazoezi ya kikosi cha kwanza mpaka atakapoiomba radhi Liverpool pamoja na wachezaji wenzake kufuatia kauli yake kwamba uongozi wa timu hiyo umemgeuka kwa kugoma kumuuza kwenda Arsenal.
Hata hivyo, nyota huyo anashikilia msimamo wake kwamba mabosi wa wababe hao wa Anfield walimwahidi kumuuza endapo timu hiyo itashindwa kufuzu Ligi ya Mabingwa Ulaya msimu huu.
Tayari Liverpool imezitolea nje ofa mbili za Arsenal ambayo ndio timu pekee inayomtaka Suarez huku ofa ya pili ikiwa imeweka mezani kiasi cha Pauni 40,000,001 ambazo Suarez anaamini zinatosha kumng’oa Anfield kwa mujibu wa mkataba wake.
Hata hivyo, Rodgers na mabosi wengine wa Liverpool wamesema hawakuwa na ahadi yoyote ya kumuuza Suarez kwa kiasi hicho cha pesa na badala yake Rodgers anaamini kuwa nyota huyo ana thamani ya Pauni 50 milioni na zaidi kama ilivyo kwa mastaa, Edinson Cavani na Radmel Falcao.
Suarez ameendelea kuwakera mastaa wakongwe waliowahi kuichezea Liverpool kama John Barnes, Jamie Carragher na wengineo, huku wengi wakitaka Rodgers amuuze nyota huyo ambaye msimu uliopita aliifungia timu hiyo mabao 29 katika michuano mbalimbali.
Kitendo chake cha kugoma kuomba msamaha kitaiweka Liverpool katika wakati mgumu, huku kocha wa Arsenal, Arsene Wenger, akiendelea kumngoja katika Uwanja wa Emirates.
Nyota huyo anatazamiwa kuitia Arsenal makali ya kutwaa ubingwa kama atafanikisha uhamisho wake.
Sasa huenda uhamisho huo ukaamuliwa katika vyombo vya sheria vya England endapo Suarez na wakala wake wataamua kuifikisha Liverpool katika kamati ya Ligi kwa ajili ya kuhitaji msaada zaidi wa kutia nguvu za kuhakikisha anacheza Arsenal msimu ujao.
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari