Like Us On Facebook

SHEHA ALIYEKUTWA NA BANGI ATIMULIWA HUKO UNGUJA



SERIKALI katika mkoa wa Kusini Unguja, imemtimua kazi Sheha wa Kitumba, Mtwana Kificho, ambaye wiki iliyopita nyumbani kwake alikutwa na majani makavu yanayosadikiwa kuwa bangi baada ya polisi kufanya ukaguzi.
 
Mkuu wa Mkoa wa Kusini Unguja, Dk Idrissa Muslim Hijja, jana aliwateuwa masheha wawili na kuwaapisha kuongoza shehia hizo, pamoja na sheha mpya wa Kitumba, Makame Chum.

 

Akizungumza na masheha hao katika eneo la Tunguu katika mkoa wa Kusini Unguja, Dk Hijaa, aliwataka masheha hao kutekeleza majukumu yao ya kuongoza kwa busara katika maeneo yao kwa mujibu wa sheria.
 

Alisema masheha ni watendaji na wasimamizi wa majukumu ya wananchi, ambapo matatizo yao wanatakiwa kuwasilishwa mbele ya Serikali Kuu kupatiwa ufumbuzi.
 

“Majukumu ya kazi kwa masheha ni kusimamia matatizo ya wananchi na kuyaelekeza kwa Serikali Kuu kwa ajili ya kupatiwa ufumbuzi na sio kuchochea mifarakano katika jamii,” alisema.
 

Kwa mfano Mkuu wa Mkoa aliwataka masheha hao kuacha kujiingiza katika migogoro ya ardhi na mashamba ya wananchi katika sehemu zao. Alisema Serikali imepiga marufuku masheha kujiingiza katika migogoro ya ardhi pamoja na kuuza mashamba ya wananchi.
 

“Serikali imepiga marufuku masheha kujiingiza katika migogoro ya ardhi na kuuza mashamba ya wananchi...sheha atakayebainika kufanya vitendo hivyo, atachukuliwa hatua za kinidhamu,” alisema.

 

Malalamiko makubwa ya wananchi wa Kitumba wilaya ya Kati Unguja ni wizi wa mazao kwa wakulima, pamoja na mifugo na uvamizi wa ardhi katika maeneo ya kilimo.
 

Masheha waliokula kiapo mbele ya Mkuu wa Mkoa ni Makame Chum kuongoza shehia ya Kitumba na Foum Ali Foum, shehia ya Marumbi wilaya ya Kati.
 

Akizungumza katika sherehe fupi mara baada ya kula kiapo, Foum alisema atahakikisha anayapatia ufumbuzi na kuyashughulikia matatizo yanayowakabili wananchi wa eneo lake, ikiwemo kupambana na uvuvi haramu.
 

“Katika shehia ya Marumbi, tunakabiliwa na tatizo moja la uvuvi haramu ambalo nimekusudia kulifanyia kazi kwa karibu zaidi na kuishauri Serikali kadri ya matatizo yanavyojitokeza,” alisema.


TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari