WALIOBAKWA na kisha kuozwa kwa waume katika wilaya ya Wete mkoa wa kaskazini Pemba, wamesema ndoa za ‘mkeka’, zinachangia kwa kiasi kikubwa kasi ubakaji katika jamii.
Walisema jamii imekuwa na uharaka wa kuwafungisha ndoa mabinti zao wanapobaini kuwa na uhusiano na wanaume, wakidhani kuwa ndio sulhu ya kutokomeza matendo hayo, lakini badala yake wamekuwa wakichangia kuendelea.
Wakizungumza na mwandishi wa habari hizi katika utafiti maalum wa kuangalia hali ya kupungua kwa matendo ya ubakaji katika shehia sita wilayani humo, waathirika wa matendo hayo walisema ndoa za papo kwa hapo sio suluhisho.
Walisema jamii imekuwa na kawaida kuharakia sulhu ya ndoa hata kama shauri hilo limeshafikishwa katika vyombo vya sheria, jambo ambalo huwapa jeuri na kiburi wabakaji kuendelea na matendo hayo.
Mmoja kati ya waathirika wa ubakaji na kisha kuolewa mwenye miaka (17), mkaazi wa shehia ya Mchanga Mdogo wilayani humo, alisema binafsi baada ya kujihisi ameshapewa ujauzito, alikimbilia kituo cha polisi na kisha muhusika kukamatwa.
Alisema awali, alimueleza mpenzi wake kwamba ameshapata ujauzito na alipokataa, ndipo wazazi wake walipokimbilia kituo cha polisi Wete, ingawa kesi hiyo haikufikishwa mahakamani baada ya kufanyiwa suluhu.‘’Mimi nilitaka kesi hiyo ifikishwe mahakamani, lakini mama na kaka waling’ang’ania niolewe na kweli niliolewa, ingawa ndoa yangu ilidumu kwa siku 18 tu na kuachwa,’’alisema.
Nae muathirika mwengine wa matendo hayo, mkaazi wa shehia ya Mchangamdogo (18), ambae alikatisha masomo alisema, mara baada ya kubainika na wazazi wake kwamba ana ujauzito, harakati za kuolewa zilianza.
Alisema aliwekewa mkazo na wazazi wake na hata baadhi ya marafiki, kwamba ni vyema akakubali kuolewa na baada ya kujkifungua aliachwa.
Wazazi wa vijana hao wa kike walikiri kufanya hivyo kutokana na kuogopa usumbufu katika vyombo vya sheria na kisha kesi zao kutofikia pahala pazuri.
“Unaweza kuzifikisha mahakamani kesi hizo, lakini kutokana na taratibu za ushahidi zilivyo, baadae unaweza kuwaona wabakaji wako nje na sisi kuachiwa watoto wanaokosa matunzo,” alisema mzazi mmoja wa waathirika hao.
Aidha mzazi huyo alisema, wakati mwengine hulazimika kuwaozesha watoto wao kutokana na kuvunjika kwa ndoa na baba kumuachia mama ulezi peke yake.
Kwa upande wake Mratibu wa wanawake na watoto wa shehia hiyo, Mbeu Makame Bakari, alisema chanzo cha matendo hayo ni kwa wakosaji kukosa kutiwa adabu inayofaa.
Alieleza kuwa hata kama vyombo vya sheria vitafikishiwa makosa ya aina hiyo wamekuwa wakiwashawishi wahusika kufanyiana sulhu ikiwa ni pamoja na kuwafungisha ndoa.
Alibainisha kuwa, ili matendo hayo yaondoke ni vyema elimu kwa jamii ikaongezwa pamoja na sheria za ubakaji kutumika ipasavyo.
Sheha wa shehia ya Kinyikani wilaya ya Wete, Mussa Rashid Said alisema chanzo cha matendo hayo ni kuondoka kwa malezi ya pamoja ambayo yalikuwa katika miaka ya iliopita.
Alifafanua kuwa, malezi ya pamoja yaliokuwa yakiambatana na adhabu hadharani yalisaidia kwa kiasi kikubwa kwa vijana kuwa na nidhamu.
Mzazi katika shehia ya hiyo, Said Khalifan Ali, alieleza kwa wakati umefika kwa ndoa za mkeka kupigwa marufuku, kwani zimekuwa zikiwapa mbinu vijana wa kike na kiume kufanya matendo hayo.
Nae Mratibu wa wanawake na watoto wa shehia ya Mjini ole, Khadija Henop alisema, bado jamii haijaona hilo kuwa ni tatizo.
Nae sheha wa shehia ya Kangagani, Faki Omar Yussuf, alisema matendo hayo yanaweza kukoma, pindi sheria ya kuwalinda watoto wa kike na matendo hayo itatumika.
Mwanafunzi wa kidato cha pili skuli ya sekondari ya Kangagani, Rehema Juma Shaame (18), alisema watoto wa kike wamekuwa wakibakwa kutokana na baadhi yao kujengwa na tamaa ya maisha.
Afisa Elimu na Mfunzo ya Amali mkoa wa kaskazini Pemba, Hassan Sheha Ali, alisema chanzo cha matendo hayo, pia husababishwa na utukutu wa baadhi ya vijana wa kike.
Kwa upande wake Afisa Ustawi wa Jamii wilayani humo, Haroub Said Hemed, alisema bado jamii inahitaji elimu kwa umbapana zaidi ya athari ya ubakaji.
Afisa Mkuu wa seksheni ya wanawake na watoto, Wizara ya Ustawi wa Jamii Maendeleo ya Wanawake na Watoto, Pemba Rabia Rashid Omar, alisema kuna mambo kadha yanayochangia kuzorotesha jitihada za kutokomeza matendo hayo.