Like Us On Facebook

HISTORIA FUPI YA AUNT EZEKIEL...

 JINA la Aunt Ezekiel siyo geni kabisa kwa wadau mbalimbali wa burudani hapa nchini, ni staa ambaye hivi sasa ana jina kubwa kupitia sanaa yake ya uigizaji wa filamu aliyoianza miaka sita iliyopita.
Japokuwa kwa sasa ni staa, amepitia mambo mengi magumu katika safari yake ya maisha mpaka kufikia hapo alipo hivi sasa.
Aunt alizaliwa mwaka 1988 mkoani Dar es Salaam, baba yake akijulikana kama Ezekiel Grayson’ Jujuman’ ambaye alikuwa ni mchezaji hodari sana wa timu ya Simba. Alipata elimu yake ya msingi katika Shule ya Bunge mwaka 1993 hadi 1998. Alienda kumalizia darasa la saba katika Shule ya Msingi Chanzige iliyopo Kisarawe, mkoani Pwani.




Vipi maisha yalikuwaje baada ya kumaliza shule?
“Kwa kweli maisha yalikuwa ni magumu mno kwa maana nilipomaliza shule tu, alijitokeza mwanaume na kutaka kunioa kitu ambacho mimi sikukipenda kabisa lakini baba yangu alitaka hivyo kwa vile uwezo wa kunisomesha hakuwa nao tena na maisha yalikuwa ni magumu sana


 Alitoroka nyumbani kwao alfajiri
“Baada ya kuona mambo ya mimi kuolewa yanapamba moto huku yule mwanaume akizidi kuihudumia familia yangu, nikaona nikichelewa nitabebwa mzobemzobe, hivyo niliamua kutoroka alfajiri na mpaka natoroka, sikuwa najua naelekea wapi.

Aenda kufanya ‘uhausigeli’
“Baada ya kutoroka, asubuhi ile nilienda mpaka Ukonga, sehemu moja inaitwa Mazizini, nikagonga nyumba moja ya mtu na kumwambia natafuta kazi za ndani, bila kuchelewa yule dada aliniambia hata yeye anatafuta msichana, hivyo nilianza kufanya kazi nikawa namlea mtoto na kufanya kazi zote za ndani huku nyumbani kwetu wakinitafuta bila mafanikio.


 Arudi nyumbani kwao
“Baada ya kufanya kazi kwa muda wa miezi mitatu, niliamua kumpigia simu baba yangu ambapo aliposikia sauti yangu alifurahi sana na kuniambia kuwa nirudi nyumbani wala hawataweza kuniozesha tena, hivyo niliamua kumuaga tajiri wangu na kumwambia narudi nyumbani kwetu.

Aendelea na shule
“Niliporudi nyumbani bado nilimkuta yule mchumba lakini nilimwambia kama anataka kunioa anisubiri nisome, hivyo nilienda Iringa katika Shule ya Sekondari Kawawa na kuanza kidato cha kwanza mpaka cha pili, nikarudi Dar na kumalizia katika Shule ya Sekondari Makongo mwaka 2004.

Aingia kwenye urembo

“Baada ya kumaliza sekondari, nilijiunga na mambo ya computer pale Amana, lakini baadaye niliamua kushiriki mambo ya urembo ambapo niliibuka kuwa Miss Mwanza 2006 na kuingia katika shindano la kumsaka mrembo wa Tanzania lakini sikufanya vizuri na hapo ndipo nilipoingia kwenye uigizaji wa filamu ambapo filamu yangu  ya kwanza kabisa ilikuwa ni Miss Bongo, iliyokuwa ya William Mtitu.


Afunga ndoa, azawadiwa kilo moja ya dhahabu
“Ilipofika mwaka 2007 nilifunga ndoa ya bomani na mfanyabiashara maarufu Jack Pemba. Yule mchumba aliyekuwa akinisubiri mwanzo alikuwa ameshakata tamaa na kuendelea na maisha yake, hivyo nilianza kuishi na Jack kama mke na mume huku akinisaidia katika mambo yangu ya sanaa.
“Baadaye alinizuia kwani alikuwa hapendi nitoke nyumbani na baada ya muda nilipata ujauzito wake kitu ambacho kilimfurahisha sana na kunizawadia vito vya dhahabu vyenye uzito wa kilo moja, lakini kwa bahati mbaya ilipofika miezi saba nilijifungua mtoto akafariki.

Kipigo chamkimbiza kwenye ndoa

“Ndoa ilikuwa ni nzuri, nilikuwa napata kila kitu ambacho nataka na kutembelea gari za kifahari lakini kitu ambacho nilikishindwa ndani ya ndoa hiyo ni kipigo kikali nilichokuwa nakipata, kwani nakumbuka kuna siku alinipiga kiasi ambacho mashuka meupe yalikuwa kama yamepakwa rangi nyekundu, hivyo bibi yangu alikuja kunichukua na kuondoka moja kwa moja.

Aendelea na maisha yake
“Baada ya kuondoka kwa Jack, nilianza kupigana katika maisha na niliingia kwenye uhusiano na mtu mwingine na nikaanza kuingia kwenye kucheza filamu ambapo huko jina langu lilizidi kukua siku hadi siku, hivyo nikawa naweza kuyaendesha maisha yangu ya kila siku, mpaka nilipokutana na mume wangu wa sasa, Sunday Demonte ambaye alinioa mwishoni mwa mwaka jana.



Kwa nini Tanzania na si Dubai kwa mumewe?
“Unajua kazi yangu kubwa mimi ni uigizaji  ambapo huku Tanzania ndiyo kila kitu, sasa nikisema nikae Dubai muda wote ni lazima kipaji changu kitapotea, hivyo nafanya kazi zangu kwa kutengeneza filamu kama tatu, kisha narudi Dubai kidogo kukaa na mume wangu.

Nini kilichomuumiza na kumfurahisha?
“Siku zote naumia sana kuwapoteza wazazi wangu wawili, yaani baba na mama, nilitamani sana mpaka leo wawepo na waione kazi yangu na nilifurahi sana siku ambayo nilifunga ndoa yangu ya pili na Sunday Demonte,” anaeleza Aunt.


TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari