Baadhi ya mastaa hao wanatuhumiana kutapeliana fedha walizochangisha kwa ajili ya kukodi magari ambayo yangewabeba kutoka pale Viwanja vya Leaders, Kinondoni hadi ikulu iliyopo Magogoni, Dar.
Akizungumzia kitendo hicho kwa sharti la kutotajwa, mmoja wa wasanii hao alisema: “Baada ya kukusanyika pale Leaders (siku ya tukio) tuliamua kuchangishana kwa ajili ya kukodi magari ambayo yangetupeleka ikulu lakini wakati zoezi hilo likiendelea ndipo ulipokuja ujumbe kuwa safari hiyo imekufa baada ya Rais Kikwete kupata mgeni kutoka Marekani, Bill Clinton.
“Sikuwa na shaka na taarifa zile za kuahirishwa kwa mwaliko wa kwenda kufuturu ikulu, nilitegemea kuwa kila mtu aliyechangishwa angerudishiwa fedha zake lakini hadi tunaondoka maeneo ya Leaders hakuna aliyerudishiwa.”
Baada ya kupata maelezo hayo, mwandishi wetu alimtafuta aliyekuwa mratibu mkuu wa mwaliko huo, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’ ambapo aliposomewa mashtaka yake alikiri kutokea matatizo hayo huku akitupa lawama moja kwa moja kwa wachangishaji.
“Muulize Muhogo Mchungu (Rajab Mkumbila) au Chiki (Salum) Mchoma, hao ndiyo watakupa jibu kamili,” alisema Steve Nyerere
Kwa upande wake, Chiki alisema kuwa hapendi kuzungumzia suala hilo huku naye akimtupia mpira Muhogo Mchungu kuwa ndiye aliyekuwa na daftari la waliochangisha.
Naye Muhogo Mchungu alipotafutwa na mwanahabari wetu alisema kuwa kama kuna mtu anadai fedha zake amtafute na si kulalamika kwenye vyombo vya habari.