SAKATA la maofisa wanne waliotajwa na Waziri wa Uchukuzi, Dkt. Harrison Mwakyembe kuhusika na kupitisha dawa za kulevya kilo 150 katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNIA) limeendelea kutekelezwa baada ya maofisa hao kukabidhiwa barua zao rasmi.
Mkurugenzi wa JNIA, Moses Malaki aliyathibitisha hayo jana kuwa, maofisa wanne waliotajwa kuhusika katika sakata la kupitisha kilo zaidi ya 150 za dawa za kulevya zenye thamani ya sh.bilioni 6.8 wamepewa barua zao za kusimamishwa kazi.
Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, Malaki alisema hilo ni agizo la Waziri, lakini pia ni la Serikali hivyo tayari maofisa hao wanne wamepewa barua zao kama walivyoagizwa.
Alisema, hatua zingine zitafuata baada ya tume kukamilisha kazi yake na kutoa mapendekezo yake ambapo kisheria hawawezi kumfukuza mtu kienyeji bila kufuata taratibu za kikazi.
"Ni kweli tumekwishawapa barua zao, lakini na wao ni binadamu na ni lazima sheria zifuatwe, kwani mtu unayemfukuza lazima umpe siku 14, lakini sisi ni siku saba tu tumewapa barua hizo, hivyo kwa sasa tunaomba mtuache kwanza ili uchunguzi uendelee na wao wajieleze mbele ya tume na hatua zingine zifuatwe," alisema Malaki.
Maofisa waliopewa barua zao, ambao walitajwa na Waziri Mwakyembe kuhusika na sakata hilo ni Yusufu Daniel Issa, Jakson Manyoni, Juliana Thadei na Mohamed Kalungwana ambapo wote wanadaiwa kuhusika na sakata hilo.
Mbali na hayo pia Waziri Mwakyembe aliitaka Idara ya Usalama wa Utaifa kuwachukulia hatua maofisa wa idara hiyo, kwa kuchelewesha mbwa ambao walitakiwa kuwepo wakati mizigo hiyo ilipokuwa ikipitishwa akiwemo pia askari polisi kumchukulia hatua askari wake ambaye naye alihusika katika sakata hilo.
Mtu mwingine ambaye alitajwa katika sakata hilo ni mbeba mizigo wa uwanja huo, Zahoro Mohamed Seleman ambaye anapaswa kukamatwa na kufukuzwa kazi ikiwemo kufunguliwa mashtaka ili kuunganishwa na wenzake aweze kujibu mashtaka ya jinai