Shamra shamra na nderemo zilitawala jana kwenye Ukumbi wa Mikutano wa Mlimani City wakati Miraji Kikwete, mtoto wa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete alipofunga ndoa na Alma Mahmoud.
Sherehe hizo zilianza saa 7:00 mchana baada ya ndoa kufungwa na maharusi hao kuingia ukumbini hapo wakiongozana na Rais Kikwete.
Hali nje ya ukumbi huo ilikuwa tulivu ingawa
uwanja ulikuwa umefurika magari ya polisi, viongozi na wageni waalikwa.
Huku kikosi cha kudhibiti ulinzi na usalama kikiwa kimefunga mitambo
ndani na nje ya ukumbi huo.
Ulinzi katika eneo hilo ulikuwa ni mkali kupita
kiasi ambapo hakuna yeyote aliyeruhusiwa kuingia ukumbini humo bila kadi
maalumu, hata angeomba kwa kupiga magoti.
“Hata sisi tumetoka Bagamoyo hadi hapa tuna undugu
kabisa na mkubwa (Rais Kikwete), lakini wametunyima kwa sababu hatuna
kadi,” alilalamika mwanamke mmoja aliyeongozana na wanaume wawili.
Hakuna waandishi wa habari walioruhusiwa kuingia
ndani ya ukumbi huo, isipokuwa waandishi na wapiga picha maalumu wa
Serikali ambao walipewa vitambulisho maalumu na tisheti.
Wengine walioonekana wakipiga picha ni wanafamilia
ambapo watoto wa kiume wa Rais Kikwete, walionekana wakiwa na kamera
huku wamevalia kanzu nadhifu.
Mfanyakazi mmoja wa Ikulu alipomwona Mwandishi wa
gazeti hili, alimfuata na kumwambia kuwa sherehe hiyo ni ya kibinafsi na
haruhusiwi mwandishi yeyote kufanya kitu chochote.
“Tumenyimwa kuruhusu waandishi kwenye sherehe hii,
sawa wewe ni mwandishi lakini hii ni sherehe binafsi na ya kifamilia,
huruhusiwi kupiga picha yeyote,” alisema mfanyakazi huyo, jina
linahifadhiwa.
Hata hivyo, mwandishi alitumia mbinu kupata picha
za maharusi hao pamoja na matukio mengine yaliyokuwa yakiendelea
ukumbini hapo.
Wageni wengi waalikwa walianza kuingia ukumbini humo majira ya mchana na wengine waliendelea kuwasili hadi saa 11 za jioni.
Wengine waliokuwepo ni Mkuu wa Jeshi la Polisi Mstaafu, Inspekta
Jenerali Omari Mahita, Mkurugenzi wa Mashindano ya Urembo ya Miss
Tanzania, Hashim Lundenga, Sheikh Mkuu wa Tanzania Mufti Issa Shaaban
Simba na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Mecky Sadicky.
Muda wa chakula ulianza mida ya saa kumi jioni
ambapo baada ya bwana na bibi harusi kuchukua chakula, wageni waalikwa
nao walianza kuitwa kwa makundi na kwa ustaarabu wa hali ya juu kuchukua
chakula.
Hata hivyo kutokana na wingi wa watu waliofurika
ukumbini hapo, msururu wa chakula haukumalizika hadi Miraji na mke wake
mpya wanaondoka ukumbini hapo.
Rais Kikwete ambaye alikuwepo katika sherehe hiyo
alikuwa wa kwanza kuondoka ukumbini hapo muda wa saa 11:30 jioni
akifuatiwa na Rais Mwinyi na viongozi wengine wa kitaifa.
Maharusi walikuwa wa mwisho kutoka ukumbini baada
ya viongozi wote wa kitaifa kuondoka huku wimbo maarufu wa “Aiya iyaaa
kuolewa utarudi nyumbani kutembea” ukiwasindikiza jambo ambalo bila
shaka lilimuumiza bibi harusi huyo ambaye alianza kulia huku Miraji
akionekana kumbembeleza.
Baada ya Alma kuingia kwenye gari, Miraji naye aliingia akiwa anacheza kwa furaha huku Ridhwani akimfungulia mlango.