Mchekeshaji mkongwe wa Tanzania Rashidi Mwishehe aka Kingwendu amedai kuwa sanaa ya vichekesho Tanzania haiwalipi vizuri wasanii hao.
Akiongea kupitia Hatua Tatu ya 100.5 Times Fm, Kingwendu amesema
kutokana na kipato kidogo wanachokipata wasanii hao, hujikuta wakitengwa
na wasanii wenzao wa Bongo Movies ambao huingiza kiasi kikubwa cha pesa
kwa kucheza movies hizo.
“Kwa kweli tasnia yetu ya filamu upande wa comedy haitulipi vizuri na
ndio maana wasanii wengi wa comedy hatuna magari, hatuna nyumba nzuri,
tunachokipata tunakaa na watoto wetu hivyo hivyo tunakula. Lakini
kiukweli kabisa filamu ya comedy haitulipi vizuri, wanatulalia sana.”
Kingwendu ameongeza kuwa wasanii wa comedy wanatengwa na waigizaji wenzao kwa kuwa wao ni masikini.
“Kwa sababu sisi wanatutenga kwa sababu kama nilivyokwambia, ni
masikini. Hatuna usafiri, na usafiri wetu sanasana mtu akijitahidi kwa
comedy utakuta Kingwendu ana pikipiki. Lakini wenzetu utakuta wana
ma-Hammer, wanaendesha magari mazuri mazuri.
“Japo mashabiki wanasema kuwa wanauzia sura yale magari sio ya kwao,
lakini sisi tunaamini ni ya kwao kwa sababu filamu wanauza kwa bei nzuri
sana. Hasa kwenye soko la Steps pale wanauza kwa bei nzuri sana kama
una filamu nzuri.”
Mchekeshaji huyo amewashauri wasanii wa Bongo Movie kuwa wamoja na
kutowatenga wachekeshaji kwa kuwa ubaguzi huo utaipoteza tasnia ya
filamu Tanzania.