Hatimaye, Jeshi la Polisi nchini, limeanzisha operesheni maalumu ya kuwabaini na kisha kuwachukulia hatua za kisheria wale wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii kama vile Twitter, Facebook pamoja na laini za simu.
Jeshi
la Polisi limeamaua kuchukua hatua hiyo baada ya kuona teknolojia hizo
zinatumiwa vibaya na watumiaji ikiwa ni pamoja na kuhamasisha vitendo
vya uvunjifu wa amani ya nchi, kutishia usalama wa maisha ya watu na
kutengeneza njama ovu za matukio ya kijambazi.
Baadhi
ya hatua ambazo jeshi hilo limepanga kuwachukulia wote watakaobainika
kutumia vibaya mitandao hiyo ni pamoja na kuwapeleka mahakamani.
Akizungumza
na NIPASHE jana, Mratibu Msaidizi wa Polisi kutoka Makao Makuu ya Jeshi
hilo, Kitengo cha Cyber Crime, Joshua Mwasungasa, alisema operesheni
hiyo ni endelevu kwa nchi nzima, lakini kwa sasa wameanza na Jiji la
Dar es Salaam kuanzia mwezi huu hadi Aprili, mwakani.
Alisema
jeshi hilo linafanya operesheni hiyo kwa ushirikiano na kampuni
mbalimbali za simu pamoja na Mamlaka ya Mawasiliano nchini (TCRA), na
kwamba wote watakaobainika kutumia mitandao hiyo kwa matukio yoyote ya
kiuhalifu, watachukuliwa hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kupelekwa
mahakamani bila kujali hali au mahali alipo mtuhumiwa.
Kwa
mujibu wa Mwasungasa, wanayo idadi ya watuhumiwa wanaotumia vibaya
teknolojia hizo za mawasiliano, lakini alisema asingeweza kuiweka wazi
ili isivuruge zoezi hilo ambalo wanaendelea nalo kwa sasa na kwamba
wameamua kuanzisha operesheni hiyo mapema kwa ajili ya kuzuia athari
kubwa ambayo ingeweza kujitokeza hapo baadaye baada ya kuonekana kwa
dalili za vitisho vya uvunjifu wa amani kutokana na watu wanaotumia
vibaya teknolojia hizo.
“Zoezi
hili si la muda mfupi, ni la muda mrefu. Hatuwezi kusubiri mpaka
uharibifu utokee ndipo tuanze. Tumeona vyema tuanze sasa kwani kuna
‘threats’ (vitisho) mbalimbali vinakuja kutokana na matumizi mabaya ya
laini za simu na mitandao ya kijamii. Ni lazima tuwe na ‘Line Patrol’
kabla ya kitu kutokea na kuleta uvunjifu wa amani,” alisema na kuongeza:
“Kutumia
laini za simu kwa mambo ya kiuchochezi ni kosa kisheria, na Sheria ipo
ya EPCO inayosimamia matumizi ya mtandao hiyo. Kama mtu anatumia mtandao
wa simu kwa kukashifu mtu ni kosa, na siyo simu tu bali hata mitandao
ya kijamii.
Kutokana
na hili, tumeanzisha operesheni maalumu inayoitwa ‘Line Patrol’ kwenye
simu na mitandao ya kijamii na endapo tutakutana na kitu ambacho
kinakiuka sheria ya matumizi ya mitandao hiyo, tutamchukulia hatua za
kisheria ikiwa ni pamoja na kupelekwa mahakamani mhusika.”
Aliongeza
kuwa mtu yeyote atakayetuma meseji za uchochezi kwa mwingine kupitia
mitandao hiyo ya mawasiliano, atakuwa hatiani na yule atakayepokea na
kurusha kwa mwingine bila kuifuta, naye pia atakuwa ameshiriki vitendo
hivyo vya uhalifu kwani atakuwa ameingizwa na kuonekana kuwa ni mmiliki
wa meseji hizo za kiuhalifu.
Alitaja
baadhi ya matumizi mabaya ya mitandao hiyo kuwa ni pamoja na kuzungumza
au kuandika ujumbe wa uchochezi, kukashfu, kutengeneza njama za matukio
ya uhalifu na kuchochea uvunjifu wa amani.
Aliwaasa
Watanzania kuwa makini na matumizi ya teknolojia hizo kwani kwa mujibu
wa sheria zinazosimamia matumizi ya mitandao hiyo ya EPCO, mtu yeyote
akipokea ujumbe wa uchochezi bila kuufuta na kuurusha kwa mwingine,
tayari ameshakuwa mmiliki wa kosa hilo.
Alisema
baada ya kumalizika kwa awamu ya kwanza ya uchunguzi huo katika Jiji la
Dar es Salaam ifikapo Aprili, mwakani, watafanya tathmini na kisha
kuwachukulia hatua za kisheria wote watakaobainika, na kisha kuendelea
na maeneo mengine.
Aliongeza
kuwa katika zoezi hilo, pia wanalenga kutoa elimu kwa Watanzania na
watumiaji ambao hawana uelewa wa kutosha kuhusu matumizi ya mitandao
hiyo kwani wengi wameingizwa kwenye matukio ya uhalifu kwa sababu ya
kutokuwa na elimu hiyo.
Kutolewa
kwa taarifa hiyo ya Jeshi la Polisi, kunafuatia malalamiko mengi kutoka
kwa watumiaji wa mitandao nchini kutokana na kukashfiwa, kutishiwa
usalama wa maisha yao na kudhalilishwa.
Baadhi
ya viongozi ambao kwa siku za hivi karibuni walipewa vitisho kupitia
mitandao hiyo ni pamoja wabunge akiwamo Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless
Lema; Mbunge wa Viti Maalum, Esther Bulaya; Spika wa Bunge, Anne
Makinda na Naibu wake, Job Ndugai.
NIPASHE
lilizungumza na Cyber Crime baada ya TCRA hivi karibuni kusema kuwa
wanaoshughulika na udhibiti wa mitandao ya mawasiliano ikiwamo hiyo ya
kijamii, ni Jeshi la Polisi.
-NIPASHE