Like Us On Facebook

WAATHIRIKA WA UKIMWI WAGOMA KUTUMIA DAWA ZA ARV'S..



WAGONJWA 272,939 wameacha kutumia dawa za kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARV’s). Kutokana na hali hiyo, virusi vya ugonjwa huo vimeanza kuwa sugu kwa kuwa havipati dawa za kupambana navyo. 
Taarifa hiyo ilitolewa na Makamu wa Rais, Dk. Mohamed Gharib Bilal wakati wa maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani yaliyofanyika kitaifa jijini Dar es Salaam.

Tafiti zinazoendelea kufanyika zimeonyesha kuwa, mtu anayetumia ARV’s inavyostahili uwezekano wa kumwambukiza mwenzake unapungua hivyo nawashauri watu waendelee kuzitumia, naomba wasiache kwa sababu sasa tunaambiwa theruthi moja ya walioandikishwa hawatumii ARVs, ”alisema Dk. Bilal.

Pia alizitaka mamlaka husika kuchukua hatua kali kwa watu wanaosambaza dawa bandia za ARV’s.

Kulingana na takwimu za Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii hadi kufikia Juni mwaka huu watu milioni 1.2 walikuwa wamesajiliwa kwa ajili ya tiba na matunzo na kati yao waliokuwa wameanzishiwa ARV’s ni 736,664 lakini wanaotumia ni 463,725.

Kwa upande wa watoto waliosajiliwa kwa ajili ya ARV’s ni 91,283 na wanaoutumia ni 60,572.

Dk. Bilal alisema tayari serikali imeanza kuchukua hatua dhidi ya mikoa yenye maambukizi makubwa ya Virusi vya Ukimwi kwa kuangalia vichocheo vinavyosababisha maeneo hayo kuwa na maambukizi hayo makubwa.

Pia, alisema wamekamilisha taratibu za uanzishwaji wa mfuko maalum wa ukimwi ambao unalenga kuongeza fedha na kupunguza utegemezi kutoka kwa wahisani.

Katika maadhimisho hayo, Dk. Bilal pia alizindua mkakati wa awamu ya tatu wa kudhibiti ukimwi nchini ambao umejikita katika kutokomeza maambukizi mapya, unyanyapaa na vifo vitokanavyo na ukimwi.

Naye Naibu Waziri wa Afya na Ustawi wa Jamii, Dk. Seif Rashid, alisema mwaka jana wajawazito 73,955 waligundulika kuwa na virusi vya ukimwi na kati yao 44,799 walipewa ARV’s ili kuzuia maambukizi kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto.

Hata hivyo, alisema karibu asilimia 50 ya wajawazito wanajifungulia majumbani na kwamba imekuwa ni sababu kubwa ya kutoanzishiwa dawa.

Pia alisema kiwango cha maambukizi ya virusi vya ukimwi kwa wachangiaji damu kwa hiyari kimeshuka kutoka asilimia saba hadi kufikia chini ya asilimia moja.

Kwa mujibu wa Dk. Rashid, kati ya mwaka 2007 hadi Juni mwaka huu, zaidi ya watu milioni 19.1 walipima virusi vya Ukimwi kwa hiyari.

Wakati huo huo, Naibu Waziri huyo alisema jumla ya wanaume 676,225 wametahiriwa katika mikoa 12 ambayo ilionekana kuwa na kiwango kikubwa cha maambukizi ya ukimwi na kiwango kidogo cha tohara ya wanaume.

Naye Mwenyekiti wa Baraza la Watu Wanaoishi na Virusi vya Ukimwi Nchini (NACOPHA), Vitalis Makayula, alisema unyanyapaa bado upo na hivyo akawataka watunga sera, watoa maamuzi na vyombo vya habari kuepuka kutoa lugha ya unyanyapaa kwani inarudisha nyuma juhudi za kupambana na VVU.

Pia aliitaka Serikali kuwahakikishia uwepo wa dawa za kutosha na zenye ubora unaozingatia viwango vilivyowekwa ili kila anayehitaji aweze kuzipata kwa wakati.


TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari