Habari za kuaminika zilizotua mezani mwa gazeti hili kutoka katika chanzo chetu makini zinatonya uwepo wa biashara hiyo ufukweni mwa bahari ya Hindi na katika mahoteli makubwa ya jijini Dar es Salaam.
“Najua mliwahi kuandika, lakini wamesharudi, kwa macho yangu nimewaona (anataja jina la hoteli) wakipiga mzigo kama kawaida.
“Yaani wapo wengi sana, ukitaka kuamini nenda (anataja jina la fukwe) uone uchafu wao,” kilisema chanzo hicho ambacho kiliomba hifadhi ya jina lake.
Dawati la Risasi Mchanganyiko lilipokea kwa mikono miwili tuhuma hizo na kama kawaida, ikaundwa timu ambayo ilivinjari katika maeneo yote yaliyotajwa na chanzo chetu na kubaini ukweli wa uchafu unaofanywa na makahaba hao wa Kichina.
Kwa kutumia mtego wa kujifanya wateja, waandishi wetu waligundua kuwa, machangudoa hao wanatoa huduma ya ngono ya chapchap kwa kiwango cha shilingi 20,000 hadi 30,000 kwa ufukweni na 50,000 hadi 60,000 hotelini.
Akiongea na Risasi Mchanganyiko kwa sharti la kutoandikwa jina lake gazetini, mhudumu wa hoteli moja kubwa jijini Dar ambayo baadhi ya machangu wamepanga hapo, alisema hafurahishwi na uchafu unaofanywa na Wachina hao.
“Mimi inaniuma sana kuona hawa Wachina wanakuja kuharibu nchi yetu. Huu ni uwekezaji gani? Sisi wenyewe ukahaba tunaupiga vita, wao wageni ni akina nani?” Alisema kwa mtindo wa kuhoji.
Alipoulizwa ni kwa nini wanaruhusu kufanyika kwa biashara hiyo hotelini kwao, alijibu:
“Unajua si kwamba wana danguro hapa, hapana. Wanaishi wanne katika vyumba tofauti, lakini kuna wakati wanaume wanakuja kuwachukua au kulala nao vyumbani.
“Sasa huwezi kuingilia mambo binafsi ya mteja. Kwa kuwa wamepanga hapa, wana uhuru wao. Ila mimi kama mtu mzima nafahamu kinachofanyika, hasa kwa jinsi wanaume wanavyopishana,” alisema.
Ismail Tidego mkazi wa Sinza ya Mori, Dar, alipozungumza na gazeti hili katika mahojiano maalum alisema yeye anapeleka lawama kwa serikali kupitia Idara ya Uhamiaji, maana wao ndiyo wanaotoa vibali vya Wachina hao kuingia nchini.
“Mimi nalia na Idara ya Uhamiaji, kwani huwa hawafuatilii kujua wanaingia kufanya kazi gani? Kwa nini tunajidhalilisha kiasi hiki? Yaani nchi yetu inawekezwa hadi katika biashara ya uchangudoa? Inatia uchungu sana,” alisema Tidego.
Awali machangudoa hao waliingia matatani baada ya uchunguzi wa muda mrefu kufanywa na gazeti damu moja na hili la Ijumaa na kuwanasa kwa kushirikiana na askari wa Kituo cha Polisi Oysterbay jijini Dar es Saalam.
Baada ya kukamatwa wakifanya biashara hiyo haramu huku wakitumia kivuli cha ‘business’ ya huduma ya ‘massage’, walizolewa hadi katika Kituo cha Polisi Oysterbay na kufunguliwa shauri lao.
Upepo ukiwa umetulia, hivi sasa wamerudi na wanaendelea kufanya biashara kama kawaida tena wakiwa wametanua wigo tofauti na awali ambapo walikuwa na vituo vichache.
Kutoka kwa mhariri;
Hivi karibuni, Naibu Waziri wa Viwanda na Biashara, Lazaro Nyalandu aliwahi kutamka kuwa, serikali inatoa muda kwa Wachina waliopo nchini wakifanya shughuli za umachinga kuondoka mara moja.
Akasema wanaotakiwa kubaki ni wale waliowekeza katika biashara kubwa, lakini sasa inashangaza hata makahaba wapo, biashara kubwa ni zipi? Au hawakuondoka licha ya muda uliotolewa na serikali kumalizika?
-GPL