Katika hali isiyo ya kawaida, shule moja wilayani Bagamoyo imekutwa ikiwa na mwalimu mmoja tu anayefundisha wanafunzi kuanzia chekechea hadi darasa la saba, wote wakifundishwa katika chumba kimoja kwa kutumia ubao mmoja.
Hata hivyo, katika matokeo ya Darasa la Saba Mwaka huu, wanafunzi wote 12 walifaulu kuingia kidato cha kwanza.
Shule hiyo ya msingi Machala, iliyokuwa na idadi ya wanafunzi 198 na imejengwa kwa majani kuanzia chini hadi kwenye paa.
Mwandishi wa habari hizi aliyetembelea shule hiyo, alimkuta mwalimu huyo akiwafundisha wanafunzi hao wa madarasa tofauti wakiwa kwenye chumba kimoja, huku ubao wa kufundishia ukiwa umechorwa mistari mitatu kutenganisha masomo ya chekechea hadi darasa la pili, mstari mwingine darasa la tatu hadi la tano na mwingine darasa la sita hadi la saba.
Mwalimu huyo, Christopher Rukutu, aliliambia NIPASHE Jumamosi kuwa shule hiyo hutumia kivuli cha mti kama ofisi.
Shule hiyo iliyopo katika kijiji cha Mihunga Kata ya Miono, Wilaya ya Bagamoyo Mkoa wa Pwani, ilianzishwa na serikali tangu mwaka 2007 ikiwa na wanafunzi 12 ambao wamemaliza darasa la saba, mwaka huu na kubahatika kufaulu wote.
Kwa mujibu wa mwalimu Rukutu, wanafunzi wote waliofaulu walipata alama za A na B isipokuwa mmoja aliyepata alama C.
Pamoja na kuwa katika mazingira magumu, shule hiyo kiwilaya ilishika nafasi ya sita na kimkoa nafasi ya 20.
Alisema shule hiyo haina vitabu vya kiada wala vya kufundishia na amekuwa akiazima kutoka shule za jirani.
“Ninafundisha kwa akili za kuzaliwa sina kitabu cha mtaala wa elimu, nguvu zangu zote nilimalizia kwa darasa la saba ili wajue kusoma, kuandika na kuhesabu.
Kwa mwaka mzima sijafundisha darasa la nne nina wasiwasi matokeo yao hayatakuwa mazuri kwa sababu niko peke yangu," alisema kwa masikitiko.
Alifafanua kuwa tangu shule hiyo ianzishwe, serikali ilikuwa imewapanga walimu wawili tu, ambao kutokana na mazingira kuwa magumu waliripoti bila kuingia darasani na kuaga baada ya kuonyesha vyeti vya hospitali vinavyonyesha kuwa afya zao haziwezi kustahimili mazingira magumu.
Aliilalamikia serikali kuanzia ngazi ya kata hadi wilaya kwa kuisahau shule hiyo bila kuipa msaada wowote.
Mbali na kukosa msaada, shule hiyo pia inatumia tundu moja tu la choo kwa wanafunzi wa kike na kiume na kusababisha wengi wao kujisaidia vichakani.Alisema kutokana na hali hiyo, wanafunzi wengi hushambuliwa na ugonjwa wa kichocho.
Aliiomba Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, kuwapangia wanafunzi wake 12 waliofaulu katika shule yake ya Machari kwenye shule za sekondari zenye mahitaji muhimu ili kuwapunguzia mateso wanafunzi hao.
Alisema wanafunzi wake hawajawahi kuona vitabu vya kujisomea na huduma muhimu za kiafya.
-NIPASHE