Like Us On Facebook

SERIKALI YAFUTA KODI YA LINE ZA SIMU NA ITAREJESHWA KWA STAILI NYNGINE



Serikali imeondoa kodi ya kadi za simu iliyopitishwa na wabunge katika Mkutano wa 13 wa Bunge ambayo ililalamikiwa na wadau na watumiaji wa simu nchini. 
 
Hata hivyo, kodi hiyo imerejeshwa kwa staili nyingine baada ya kuongezwa katika tozo la kodi ya manunuzi iliyokuwepo kutoka asilimia 14.5 ya awali hadi asilimia 17.
 
Kauli hiyo ilitolewa juzi na Naibu Waziri wa Fedha Saada Mkuya Salumu, bungeni juzi wakati akisoma Muswada wa Sheria ya Manunuzi wa mwaka 2013, ambao uliingizwa bungeni kwa hati ya dharura.
 
Muswada huo ulipelekwa bungeni kwa hati ya dharura baada ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia upitishwe na Bunge kabla ya kuwa sheria kutokana na malalamiko yaliyokuwa yametanda kila kona.
 
Katika muswada huo ambao ulichukua muda mfupi na kuchangiwa na wabunge wachache, Serikali imesema kuwa kilio cha Watanzania kilisikika na Serikali haikuona haja ya kuendelea na kodi hiyo, badala yake ikaamua kutafuta njia nyingine.
 
“Mheshimiwa Spika, Serikali imeamua kutafuta njia nyingine ya kukusanya mapato hayo ambayo yalilengwa kupatikana kwa zaidi ya Sh170 bilioni ambayo yangepelekwa katika huduma za umeme na maji, hata hivyo tumepata njia mbadala,” alisema Mkuya.
 
Alitaja njia hiyo ni kukusanya katika mitandao ya kimawasiliano yote ambayo awali hawakuwa wameilenga na kwamba kupitia njia hizo, wanaweza kupata kiasi cha Sh140 bilioni huku kiasi cha Sh30 zikitarajia kutolewa na kampuni za  mawasiliano.
 
Katika maelezo yake,  alisema kuwa kampuni za simu nchini yalikubali kutoa kiasi cha Sh30 bilioni ili kuisaidia Serikali katika kufidia pengo ambalo lingepatikana kwani tayari bajeti ilishapangwa.
 
Mwenyekiti wa Kamati ya Bajeti ya Bunge, Andrew Chenge alisema kuwa Kamati ilikutana juzi mjini Dodoma kwa dharura na kukubaliana jinsi ya kurekebisha kodi na kutafuta njia nyingine ambayo ni kutoza kuongeza kodi katika manunuzi.
 
Kwa upande wake msemaji wa Kambi ya Upinzani kaika Wizara hiyo Christina Lissu, alilaumu mpango huo kwa madai kuwa hakuna kitu kilichoondolewa na badala yake kilichofanyika ni kiinimacho kwa Watanzania.

-Mwananchi
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari