Like Us On Facebook

JK kumng’oa Pinda? ....Yasemekana kaandika barua ya kujiuzulu , Mbinu ya Kikwete kumnusuru yabainika


HATUA ya Rais Jakaya Kikwete kuridhia kutengua uteuzi wa mawaziri wanne, sasa ina kila dalili za kumpa nafasi ya kuchukua uamuzi wenye mwelekeo mpya ndani ya muda mfupi ujao kuanzia sasa...

Ni katika mwelekeo huo, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda, ambaye naye alitakiwa na wabunge kujiuzulu, licha ya juzi kutokuwa tayari kulizungumzia jambo hilo wakati akitangaza uamuzi wa Rais kutengua uteuzi wa mawaziri hao wanne, anaaminika kutangaza uamuzi huo huku hatma yake ya kuondoka madarakani ikiwa imezungukwa na wingu la shaka.

Ingawa hadi sasa Pinda mwenyewe amekwishasema yuko tayari kung’oka na kwamba atafurahi kama uamuzi huo utachukuliwa dhidi yake, lakini hatua iliyochukuliwa na Rais Jakaya Kikwete sasa inadhihirisha kuwepo kwa dalili za kutaka kumnusuru kiongozi huyo dhidi ya shinikizo la wabunge, ambao mara kwa mara wamekuwa wakimtaka ang’oke, wakimtuhumu kwa uzembe.

Baadhi ya wadadisi na wafuatiliaji wa mambo waliochambua uamuzi huu wa sasa wa Rais Kikwete, wanaeleza kuwa huenda kiongozi huyo akawa anatumia staili ile ile aliyoitumia mwaka mmoja uliopita kumnusuru Pinda.

Wanaeleza kuwa, mwaka 2012, Kikwete alilazimika kufanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri kwa kuwaweka kando mawaziri nane ambao wabunge walikuwa wakishinikiza wang’olewe pamoja na Pinda, baada ya kukasirishwa na ripoti ya Mkaguzi Mkuu na Mdhibiti wa Hesabu za Serikali (CAG), iliyowatuhumu mawaziri hao kwa ubadhirifu.

Hata hivyo, baada ya kufanya mabadiliko hayo, yaliyoshuhudia mawaziri wa Nishati na Madini, William Ngeleja, Maliasili na Utalii, Ezekiel Maige, Afya Hadji Mponda, Viwanda na Biashara Cyril Chami, Uchukuzi, Omari Nundu na wengine, Rais Kikwete hakumuondoa Pinda na tishio la wabunge kutaka kumuondoa kwa kura ya kutokuwa na imani naye nalo lilififishwa na hatua hiyo.

Wakati wadadisi na wachambuzi wa mambo wakiwa na mtizamo huo, zipo taarifa zinazoeleza kuwa ugumu wa Rais Kikwete kuchukua hatua ya kumuondoa Pinda unatokana na hatua yake ya kutaka kuinusuru serikali na mzigo wa gharama za kuwalea mawaziri wakuu pindi wanapoondoka kwenye nyadhifa zao.

Hatari hiyo ya serikali kubaki na mzigo mkubwa wa viongozi wakuu wastaafu, ndiyo inayotajwa wakati fulani mwaka 1994 kumlazimisha Rais Ali Hassan Mwinyi kumrudisha kwenye nafasi ya uwaziri mkuu, Cleopa Msuya, aliyepata kuhudumu kwenye nafasi kama hiyo wakati wa utawala wa Mwalimu Julius Nyerere.

Hadi sasa Tanzania ina mawaziri wakuu wastaafu watano, ambao ni John Malecela, Cleopa Msuya, Jaji Joseph Warioba, Frederick Sumaye na Edward Lowassa.

Hata hivyo, taarifa ambazo RAI Jumapili limezipata zinaeleza kuwa, Pinda binafsi yuko tayari kukabidhi madaraka, ingawa uamuzi huo haijulikani utachukuliwa namna gani na Rais Kikwete pindi atakaporejea Alhamisi wiki hii, akitokea Marekani, alikokuwa kwenye matibabu.

Kwa mujibu wa taarifa hizo zilizolifikia gazeti hili, tayari Pinda amemueleza Rais Kikwete juu ya azma yake hiyo, huku nyingine zikieleza kuwa amekwishamuandikia barua ya kujiuzulu.

Ingawa si Pinda wala Ikulu waliopatikana kuthibitisha taarifa hizo hadi tunakwenda mitamboni usiku wa kuamkia leo, ni wazi kwamba, hatua ya sasa ya Rais Kikwete inakuja kama mbinu ya serikali yake kutaka kujisafisha kupitia mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri, ili kukwepa lawama ambazo zimekuwa zikielekezwa mara kwa mara na jamii dhidi ya serikali yake kuhusu vitendo mbalimbali vya ubadhirifu na ukiukwaji wa haki za binadamu.

Tayari mawaziri wawili majina yao yameanza kutajwa kurithi nafasi ya Pinda, ikiwa ataondoka katika nafasi hiyo.

Mawaziri hao ni Waziri wa Miundombinu, Dk. John Magufuli na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Uhusiano na Uratibu, Stephen Wassira.

Aidha kitendo hicho cha Rais kuamua kutengua uteuzi wa mawaziri wa aina ya Emanuel Nchimbi wa Mambo ya Ndani, Balozi Khamis Kagasheki wa Maliasili na Utalii, na David Mathayo wa Kilimo kwa tuhuma zilizotokana na Operesheni Tokomeza, inatajwa kuliweka njia panda Baraza zima la Mawaziri, hususan wale wanaotajwa kuwa ni mawaziri mizigo.

Taarifa zilizolifikia gazeti hili zinaeleza kuwa uamuzi huo wa Rais Kikwete umewashtua mawaziri karibu wote, huku baadhi yao wakipata shaka kama wataendelea kubaki katika nyadhifa zao.

Ni hatua hiyo pia inatajwa kumpatia nafasi ya kuwaondoa au kuwahamisha wizara mawaziri wengine, wakiwamo wale waliopachikwa jina la mawaziri mizigo pindi atakapofanya mabadiliko ya Baraza la Mawaziri.

Mawaziri wanaotajwa kuwa ni mizigo na ambao tayari wamekwishahojiwa na Kamati Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) ni pamoja na Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Dk. Shukuru Kawambwa, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Tamisemi), Hawa Ghasia.

Wengine ni Waziri wa Kilimo, Chakula na Ushirika, Christopher Chiza, Waziri wa Fedha, William Mgimwa, Waziri wa Viwanda na Biashara, Dk Abdallah Kigoda, na Waziri wa Nchi Menejimenti na Utumishi wa Umma, Celine Kombani.

Katika mabadiliko hayo ya Baraza la Mawaziri yanayotarajiwa kufanywa ndani ya muda mfupi, pia huenda yakatoa nafasi kwa baadhi ya mawaziri ama kuondoka au kubaki, lakini pia kuwajumuisha wapya.

Miongoni mwa wanaotajwa kujumuishwa katika baraza jipya la Mawaziri ni pamoja na Dk. Asha Rose Migiro, ambaye hivi karibuni Rais Jakaya Kikwete alimteua kwenye nafasi ya ubunge.

-RAI JUMAPILI 
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari