Like Us On Facebook

HII KALI:Mchungaji GWAJIMA kutangaza Injili kwa kutumia Helicopter

Wakati viongozi wa madhehebu ya dini ya Kikristo nchini, wakionekana kushindana kwa utajiri, hali inayowafanya waishi `kifalme’ na kufungua miradi, Mchungaji Kiongozi wa Kanisa la Ufufuo na Uzima, Josephat Gwajima amesema hana mpango wa kufungua biashara, zaidi ya kujikita na mahubiri ya Injili.

Aidha, amesema Mungu anaendelea kumbariki katika kazi yake, ndiyo maana mambo yake yanamnyookea, akitolea mfano kuwa baada ya kumiliki nyumba, magari na fedha za kutosha, sasa amembariki na kumpa helikopta atakayoitumia kufikia waumini wake wa ndani na nje ya nchi.
Usafiri huo wa angani, utaongeza idadi ya vyombo vya usafiri vya Mchungaji huyo, ambaye anatajwa kuongoza kwa utajiri miongoni mwa viongozi wa madhehebu ya Kikristo nchini, kwani anamiliki magari kadhaa, likiwamo la kifahari aina ya Hummer lenye thamani ya zaidi ya Sh milioni 200.
Akizungumza na mwandishi hivi karibuni kwa simu, Gwajima ambaye alikuwa anaendesha mikutano ya kueneza Neno la Mungu katika mikoa mbalimbali ikiwamo Kilimanjaro na Tanga, alisema helikopta  imeshanunuliwa na matarajio yake ni kwamba, baada ya kukamilika taratibu zote za kisheria nchini, itawasili.
“Sipendi kusema mambo yangu sana, lakini kwa kuwa umeuliza  naweza kugusia kidogo, ni kweli nina mpango wa kuanza kuhubiri Injili kwa helikopta, na kama ilivyo kwa gari, nayo hii nimepewa na watu wa Mungu walioguswa na huduma yangu Japan.
Itafika nchini wakati wowote mambo ya kisheria yakikamilika, huu si wakati wa kuizungumzia sana maana bado haijafika,” alisema Gwajima ambaye gari lake aina ya Hummer liliwahi kuzua gumzo, wengine wakimhusisha na biashara haramu ya dawa za kulevya, ingawa anapuuza madai hayo.
Mchungaji Gwajima, alieleza wazi kuwa utajiri wake unatokana na baraka anazopewa na anaowahudumia ndani na nje ya nchi na pia kazi yake ya kufundisha anayoifanya ughaibuni.
Aidha, kutokana na utajiri anaosema unatokana na baraka za Mungu, Mchungaji Gwajima anamiliki nyumba ya ghorofa nne eneo la Mbezi Beach katika Manispaa ya Kinondoni, ingawa haijakamilika.
Pia, amewanunulia wachungaji wake 40 magari ya kutembelea kwa bei tofauti, yakiwamo ya chini ya Sh milioni 10 na mengine ya zaidi ya Sh milioni 20.
Lakini nina wachungaji wa ngazi mbalimbali, hawa ni wale wa juu, wengine wachungaji wadogo wapo zaidi ya 670, hawa ni watenda kazi muhimu na wanatofautiana kwa ngazi zao, ndiyo maana kazi ya Mungu inasonga mbele hata nisipokuwapo,” alisema.
Mbali na magari ya wachungaji, pia amenunua mabasi 20 ya kubeba waumini kutoka na kwenda kanisani, yakianzia maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam. Alithibitisha kuwa, kila moja limegharimu kati ya Sh milioni 80 na 100.
Josephat Gwajima.
Mbali ya Mchungaji Gwajima, viongozi wengine wa makanisa wanaotajwa kuwa na utajiri mkubwa wa mali na fedha ni Nabii na Mtume JosephatMwingira wa Kanisa la Efatha anayemiliki benki, mashamba makubwa na mali nyingine, Mchungaji Gertrude Lwakatare wa Mikocheni B Assemblies of God anayemiliki mtandao wa shule za St. Mary’s nchini.
Wengine ni Askofu Zachary Kakobe wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship, Anthony Lusekelo `Mzee wa Upako’ wa Kanisa la Maombezi `GRC’ na Mtume Onesmo Ndegi wa Kanisa la Living Water Center ‘Makuti Kawe’.
TOA MAONI YAKO KUHUSU HABARI HII
KAMA UMEGUSWA NA HABARI ZETU, TUNAOMBA UUNGANE NASI KATIKA PAGE YETU YA FACEBOOK HAPO CHINI. BOFYA "LIKE" KAMA BADO HUJA LIKE PAGE YETU.
 

KILELE CHA HABARI Copyright © 2014 -- Template created by Mbatta -- Powered by Kilelechahabari